PICHA KWA HISANI YA MTANDAO WA BBC
NA FATMA, HAMAD PEMBA
KUPANGA kutamka au kufanya jambo kunasaidia kupata mafanikio mazuri au kupunguza hatari na athari za matatizo.
Umuhimu huu wa kupanga pia unaonekana katika uzazi kwa vile uzazi wa mpango umethibitisha kuwa na faida nyingi kwa mama, mtoto, familia na taifa kwa jumla.
Uislamu umeeleza wazi kuwa uzazi wa mpango sio unaplekea kuwa na afya njema ya mzazi na mtoto tu, bali pia furaha, amani na mapenzi katika familia.
Baadhi ya watu katika jamii wamekuwa na imani potofu kwamba, uzazi wa mpango unapunguza kizazi na kusababisha matatizo kama vile kansa na kutokwa na damu nyingi wakati wa hedhi.
Hili halina ukweli kwa sababu utafiti na ushuhuda wa wanawake waliojiunga na mpango huu unathibitisha kwamba hio ni dhana isiyokuwa na mshiko.
Asha Khamis wa Micheweni, Pemba, anafurahia uamuzi wake wa kujiunga na auzazi wa mpango na kueleza kwamba ulimsaidi kupata muda wa kulea vyema watoto na kufanya biashara yake ya kuuza uji na mandazi.
‘’Nilikuwa nikinyonyesha mtoto wangu kwa muda wa miaka miwili, na hii ilinipatia muda wa kufanya shughuli zangu za biashara kwa ajili ya kuendesha maisha yangu,’’alisema huku akitabasamu.
Amina Omar Mselem aliyejipatia watoto 7 waliozaliwa kwa kupishana muda mrefu kidogo alisema uzazi wa mpango ulimpa fursa ya kushiriki katika harakati mbali mbali za kijamii.
‘’Nilikua nikitumia uzazi wa mpango na hii ilinipa muda wa kupumzika vizuri na kwenda harusini, msibani, Kwenye vikoba na huku nikufurahia kulea , kucheza na watoto na kuwa na maisha ya furaha na mume wangu,’’alieleza Amina.
Maryam Said mama wa watoto wa 4, alisema alianza kutumia uzazi wa mpango mara tu baada ya kupata mtoto wake wa kwanza.
‘’Nimekuwa nikitumia uzazi wa mpango kwa muda mrefu na sjapata tatizo lolote la kiafya,’’ alieleza Maryam.
Utafiti na ushuhuda unaonyesha wazi kuwa uzazi wa mpango unamsaidia sana mzazi na watoto na ndio maana wataalamu wa afya wanaishajiisha jamii kutumia mpango huu kwa vile ni salama na hauna madhara.
Picha kwa hisani ya mtandao.
WATALAMU WA AFYA.
Mtaalamu wa afya wa ofisi ya huduma za mama na mtoto katika Hospitali ya Chake chake, Fatma Suleiman Daud, alisema njia za uzazi wa mpango hazina madhara bali ni tiba kwa afya ya binadamu.
‘’Mtu yoyote atakaeugua ugonjwa wa Kansa dozi yake ya mwanzo anayotakiwa kutumia ni dawa ya uzazi wa mpango,’’alifafanua.
Alisema uzazi wa mpango pia unasaidia kuwa na mzunguko mzuri wa hedhi kwa akina mama ambao hawaingiii kwenye siku zao.
Uzazi wa mara kwa mara unapelekea kushuka na kupasuka fuko la uzazi na hii huhatarisha maisha ya mama.
‘’Hali za wanawake wengi wanaozaa papo kwa pao huwa na upungufu mkubwa wa damu,’’alieleza.
Alisema yeye pia anatumia uzazi wa mpango na kwa sasa anao watoto wawili, wa kwanza ana miaka 7 na wa pili mwaka mmoja na nusu.
‘’Mimi nilijiunga na uzazi wa mpango kwa kuanzia njia ya kijiti na sasa ninatumia Kitanzi.’’alieleza.
Alisikitishwa kuona ndoa nyingi za watu wa Zanzibar zinapelekea mwanamke kujikuta na mke wenza kutokana na mwanamke kuzaa mara kwa mara, jambo ambalo hupelekea kutokuwepo amani katika nyumba na hubidi mume aongeze mke mwengine,’’ alifahamisha.
Mengi yanasemwa na kutumia visingizio mbali mbali, lakini ukweli ni kwamba uzazi wa mpango ulikuwepo tokea enzi za Mitume.
Maryam Ali Said , Mratibu wa huduma za mama na mtoto Pemba, amesema maradhi humpata mtu yoyote, na pasitafute kisingizio cha kusema sababu ni uzazi wa mpango.
‘’Tunao watu wengi walioutumia uzazi wa mpango mpaka walipofikia umri wa uzee na hawajapata tatizo lolote la kiafya,’’ amesisitiza.
Amesema wanaume wengi wanapata ugonjwa wa kansa na jee hii utasema sababu yake ni uzazi wa mpango, aliuliza.
Alifahamisha kuwa maziwa ya mama ndio chakula bora pekee kinacho mjenga mtoto kuwa na afya bora na kukuwa kimwili na kiakili.
‘’Kitaalamu mtoto anatakiwa anyonye maziwa ya mama kwa miaka 2, kwani maziwa ya mama ndio yenye virutubisho vinavyohitajika kwa ukuaji mzuri wa mtoto,’’amefahamisha.
Baadhi madhara ya uzazi wa mpango yanayotajwa na wanawake ni pamoja na kupata ugumu wa kushika mimba baada ya kutumia uzai wa mpango, kutokwa damu mara kwa mara, kupungua au kuongezeka kwa mwili, kuongezeka hamu ya kula, kupotea kwa hamu ya tendo la ndoa, mabadiliko ya siku za hedhi na maumivu ya kichwa.
Lakini utafiti wa kitaalamu umeonyesha sababu zote hizo ni zaidi za nadharia kuliko hali halisi.
MTAALAMU WA AFYA YA UZAZI
Rahila Salim Omar, mtalamu wa afya ya uzazi, amesema zipo njia nyingi za kupanga uzazi ambazo zote ni salama na miongoni mwao ni zile za kisayansi na za kisasa ambazo hazina madhara.
Alisema miongoni mwa njia hizo ni kutumia Kitanzi [Kijiti] kwa mama ambaye hajazaa sana, sindano, vipandikizi, mipira ya kiume na ya kike [Kondom] na zote hizi ni salama, na hutolewa kulingana na afya ya mama.
‘’Sio kweli kwamba ukipanga uzazi unapata matatizo, Tusidanganyane kwani kitaalamu hilo halipo’’, alisistiza.
Wapo ambao hutumia njia za asili za uzazi, kama ya kutegemea kalenda. Hii hufuata mzunguko wa hedhi au kumwaga mbegu za kiume nje ya njia ya uzazi.
KIONGOZI WA DINI.
Sheikh Abdalla Nassor Abdalla kutoka Jumuia ya Maimamu Pemba (JUMAZA) amesema Uislamu unaukubali uzazi wa mpango na kisheria mtoto anatakiwa anyonye maziwa ya mama kwa miaka 2 na hapo ndipo mama abebe ujauzito mwengine.
Mwenendo huu, amesema, unasaidia kuimarisha afya ya mama na mtoto,.
Sheikh Abdalla alifahamisha kwamba njia za kufunga uzazi zipo kwa wanawake na wanaume, na sio kwa wanawake tu. Kwahivyo ni vyema wanaume nao pia wazitumie.
Kwa mujibu wa takwimu za kituo cha huduma za mama na mtoto Pemba wa kipindi cha Januari hadi Juni mwaka huu, watu 4020 walijiunga na uzazi wa mpango. Kati yao wanaume ni 63 na wanawake 3957.
Katika Hospitali ya Mkoani wanawake ni 711, wanaume 17, Chake chake wanawake 1228, wanaume 18,Wete wanawake 1085, wanaume 13, na kwa Micheweni wanawake ni 873 na wanaume 18.
Ripoti ya Umoja wa Mataifa juu ya matumizi ya uzazi wa mpango imeonyesha ongezeko katika baadhi ya nchi, ikiwemo Tanzania. Takwimu zinaonyeha kwa sasa ni asilimia 27 ya Watanzania wanatumia njia hizo, zikiwemo sindano, vipandikizi na mipira ya kiume na ya kike.
Hofu ya njia za uzazi wa mpango.
Utafiti mpya wa Shirika la afya Duniani (WHO) umebaini kuwa theluthi mbili ya wanawake wenye uwezo wa kubeba mimba na ambao wana nia ya kuchelewesha kupata ujauzito au kudhibiti idadi ya watoto huacha kutumia huduma za uzazi wa mpango kwa hofu ya madhara ya huduma hizo.
Uzazi wa mpango sio tu ni suala la haki za binadamu bali pia ni kitovu cha uwezeshaji wa wanawake, kupunguza umasikini na kufikia malengo ya maendeleo endelevu – SDG’s (Uzazi wa mpango ni haki ya binadamu: UNFPA- 11 Julai 2018 ).