Wednesday, January 8

Utoaji huduma bora kwa watoa huduma za afya utapunguza vifo vya mama na mtoto-Mdhamini Afya

 

NA ABDI SULEIMAN, PEMBA.

AFISA Mdhamini Wizara ya Afya Pemba Khamis Bilali Ali amezitaka kamati za mashauriano za jamii, wahudumu wa afya ya jamii (CHV), na wakunga wa jadi (TBAs), kushirikiana katika utendaji wao wa kazi, ili kuondosha vifo vinavyotokana na mama na Mtoto.

Alisema ili kuondokana na vifo hivyo, kila mmoja afanye wajibu wake, ili kumshawishi mama mjamzito kuanza kuhudhuria vituo vya afya tokea  mapema, mpaka atakapofikia muda wakujifungua kujifungulia kwenye kituo cha afya.

Mdhamini huyo aliyaeleza hayo, wakati alipokua akizungunza watoa huduma za afya kwa jamii, wajumbe wa kamati za mashauriano za shehia, wakunga wa jadi na watendaji kutoka Milele Zanzibar Foundation, katika hafla ya uzinduzi wamuongozo wa CHV mkutano uliofanyika ukumbi wa baraza la Mji Chake Chake.

“Milele ni wadau walioleta miongozo itakayo tusaidia, katika utendaji wa kazi zetu, kuwaongoza wahudumu wa kujitolea hizi kazi zinazofanywa lazima wapate nguvu kutoka katika kamati za mashauriano za afya,”alisema.

Mdhamini Khamis alisema suala la afya hakuna litakaemuacha, kila mmoja litamgusa na anaweza kuisababisha jamii kutoka sehemu moja kwenda nyengine kufuata huduma za afya.

Alisema muhimu ni kufanya kazi kwa pamoja, lengo ni kuondosha vifo vinavyotokana na mama na mtoto, hivyo kila mmoja kufanya wajibu wake ili mama mjamzito kwenda kujifungulia vituo vya afya.

“Vituo vya afya vinajengwa kwa gharama kubwa, lazima tuvitumie kwenda kujifungulia kwani wakati wa kujifungua mama hupoteza damu kwa wingi na wataalamu wanataka kujuwa mapema wingi wa damu wa mama husika,”alisema.

Aidha aliishukuru taasisi ya Milele Zanzibar Foundation, kwani lengo ni kutoa huduma bora kwa kila mtu na kupata matibabu sahihi, huku wakitambua wanadhima kuona watendaji wa vituo wanatoa huduma bora, kuendelea kuwakindga watu kupata maambukizi.

Hata hivyo alisema Wizara inania ya kuboresha vituo vya afya, kujengwa vipya, miradi ya afya inaendelea kutekelezwa, ikiwemo nyumba za kuwaweka wafanyakazi, ili kutoa huduma kwa ufasaha.

Hata hivyo aliwataka wananchi kufahamua kuwa ujenzi wa chumba cha kuwekwa wagonjwa mahututi katika hospitali ya Abdalla Mzee Mkoani muda sio mrefu utaanza, huku hospitali ya Wilaya ya Chake Chake na kinyasini muda wowote mwezi huu zitafunguliwa.

Mapema afisa uendeshaji idara ya kinga na Tiba Pemba Msanifu Othman Masoud, aliipongeza taasisi ya Milele Zanzibar Foundation kwa kuwapatia nyenzo zitakazotoa mwanga wa kufanya kazi vizuri katika maeneo ya afya ya mama na mtoto.

Alisema taasisi ya MZF imeefungua njia kwa kushirikiana na wizara ya Afya, huku akiahidi watakua bega kwa bega ili kuhakikisha huduma za afya kwa jamii zinatolewa na kupunguza madhara yanayoweza kujitokeza ikiwemo vifo vya mama na mtoto.

“Serekali kupitia wizara ya afya ina mkakati mkubwa, kuhakikisha huduma za afya ndani ya jamii zinatolewa ipasavyo, ili kusaidia kupunguza matatizo mbali mbali kuanzia ngazi ya jamii,”alisema.

Mapema mratibu wa afya kutoka taasisi ya milele Zanzibar foundation Mwanaali Haji Ali, alisema mashirikiano baina ya Wizara ya Afya na Milele, kutaifanya wizara hiyo kushirikiana na jamii katika kutekeleza shughuli zote zinazohusiana na afya.

Alisema dhamira ya Milele ni kuona jamii inasimama wenyewe na kutatua matatizo yao, yanayowakabili hususani yanayohusiana na afya.

Akitoa neno la shukurani afisa miradi kutoka milele Zanzibar foundation Fatma Khamis Suleiman, alisema milele  haiwezi kufanya kazi peke yake, hivyo aliwataka wadau hao kuhakikisha wanashirikiana ili jamii iweze kupata huduma bora na kwa wakati.

Kwa mujibu wa bajeti ya Wizara ya Afya Zanzibar 2023/2024, imesema katika jitihada za kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi na vifo vya watoto wachanga Zanzibar, inaendelea na hatua mbali mbali ikiwemo kufanya uhakiki wa vifo vya mama na mtoto kwa madhumuni ya kubainisha sababu zilizopelekea kutokea kwa vifo hivyo.

Katika hilo inaekuhamasisha kina Mama kuhudhuria kliniki mapema na kujifungulia katika hospitali na vituo vya afya, ambapo katika kipindi cha Julai, 2022 hadi Machi 2023, jumla ya vifo vya mama 46 na vifo vya watoto wachanga chini ya siku saba 1,567 viliripotiwa.

Aidha Vifo vya mama 46 na vifo vya watoto wachanga 840 vilihakikiwa, matokeo ya uhakiki huo yamebainisha sababu za vifo hivyo ni pamoja na watoto kukosa hewa wakati wa kuzaliwa, uzito pungufu, matatizo yatokanayo na mtoto njiti, kupoteza damu na maambukizi kwa watoto wachanga.

Kwa upande wa vifo vya mama ni kifafa cha mimba, upungufu wa damu na kutokwa au kupoteza damu nyingi wakati wa ujauzito, kisukari pamoja na maradhi mengine sugu.

Hata hivyo Mama na Wajawazito 52,891, walihudhuria kliniki ya upimaji mimba kipindi cha ujauzito, kati yao Mama 9,017 walihudhuria kliniki wakiwa na ujauzito chini ya wiki, huku  Wajawazito 38,097 (Unguja 26,405 na Pemba 11,692) wote walijifungulia Hospitali.

MWISHO

Abdi Juma Suleiman

Journalist/Photographer

Zanzibarleo newspaper
Chake Chake -Pemba
+255774565947 or +255718968355