Thursday, November 14

SMZ itaendelea kusimamia mila, silka na tamaduni za Kizanzibari-Mh Hemed.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Alhajj Hemed Suleiman Abdulla amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kusimamia mila, silka na tamaduni za Kizanzibari ili Zanzibar izidi kusifika na Maadili mema.

Alhajj Hemed ameyasema hayo wakati akiwasalimia waumini wa Mskiti wa Ijumaa Malindi Jongeani alipojumuika nao katika Ibada ya Sala ya Ijumaa.

Amesema ni wajibu wa wananchi kusimamia Maadili mema yaliyoisifia Zanzibar na kuacha kuiga Maadilli ya Mataifa mengine ambayo yanakwenda kinyume na urithi wa Utamaduni wa Mzanzibari.

Amesema Serikali itaendelea kuchukua hatua mbali mbali ili kusimamia Maadili na kusaidia kuondoa Mmong’onyoko wa Maadili na vitendo viovu vinavyoendelea katika Jamii.

Mhe. Hemed amesema umefika wakati wazanzibari kuungana katika malezi ya watoto kwa kuzingatia miongozo ya Qur-an na Hadithi za Mtume Muhammad (S.A.W) ili kupata watoto watakaoleleka katika maadili mema watakaosaidia kuleta maendeleo nchini kwa kuwa na hofu juu ya Allah (S.W)

Sambamba na hayo Alhajj Hemed amewasisitiza waumini hao na wananchi kwa ujumla kuiunga Mkono Serikali katika kudumisha Amani na Utulivu ili kutka fursa kwa Serikali kuweza kuwaletea maendeleo wananchi wake.

Akitoa Khutba katika Sala hiyo ya Ijumaa Ustadh Said Abubakar Said Al Abbasy amewataka waumini wa Dini ya Kiislamu kuiombea Dua nchi ya Morocco ambayo imekumbwa na tetemeko la Ardhi na kuwakumbusha kuwa mtihan huo ni mazingatio kwa kila Muumini kujikaribisha na Allah Mtukufu.

Amesema miongoni mwa dalili za kiama ni kutokea kwa mtetemeko wa ardhi, kufa kwa walimu na wanazuoni, kukithiri kwa fitna na kutokea kwa machafuko duniani hivyo, ni vyema kuzidisha Ibada na Dua ili kupata mwisho mwema.

Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR)
15 Septemba, 2023