Thursday, February 27

Ukiukwaji wa maadili ya uandishi wa habari umetajwa kuwa chanzo cha kuminya demokrasia nchini

LEO KATIKA KILELE CHA MAADHIMISHO YA SIKU YA DEMOKRASIA DUNIANI
NA UTPC TANZANIA
Wakati dunia ikiadhimisha siku ya demokrasia, vyombo vya habari nchini vimeonekana kuwa moja ya sababu ya kudidimiza demokrasia kwa kutoa upendeleo kwa baadhi ya vyama vya siasa kwa maslahi binafsi.
Wakizungumza katika mdahalo ulioandaliwa na Umoja wa klabu za waandishi wa habari nchini (UTPC) kwa njia ya mtandao, uliolenga kutathimini mchango wa vyombo vya habari katika ukuaji wa demokrasia, baadhi ya waandishi wa habari wamesema kutanguliza maslahi binafsi ndicho chanzo cha kudidimiza juhudi za vyombo vya habari katika kustawisha demokrasia nchini.

Deogratuis Nsokolo Rais wa Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kigoma Press Club amesema vyombo vya habari vina wajibu wa kutoa nafasi sawa kwa vyama vya siasa kusikika sauti zao katika vyombo vya habari badala ya kuegemea upande mmoja.
Aidha, Frank Leonard, Mwenyekiti wa Iringa Press Club amesema baadhi ya vyama vya siasa kutopewa nafasi kwenye vyombo vya habari kumepelekea waandishi wa habari vikubwa kutoaminika na kutoa nafasi kwa vyombo vya mitandao ya kijamii ambavyo vingi havizingatii maadili ya uandishi wa habari.
Lulu George, Mwenyekiti wa Tanga Press Club kwa apande wake amesema waandishi wa habari wamekuwa sehemu ya dhulma kwa kuwanyima wananchi nafasi ya kupata habari kwa sababu ya posho.
Naye mweka hazina wa Mwanza Press Club Paulina David akichangia maoni yake katika mjadala huo, amesema hali halisi inaonekana kuwa baadhi ya wamiliki wa vyombo vya habari nchini wamekuwa wakianzisha vyombo hivyo kwa maslahi binafsi na kutotilia maanani lengo kuu la kuwapatia wananchi haki ya kuhabarika, na hivyo kupelekea kudidimiza juhudi za vyombo vya habari kustawisha demokrasia nchini.
Mdahalo huu ulikuwa unaongozwa na mwandishi mkongwe Lawrence Kilimwiko pamoja na mwandishi mbobezi kwenye masuala ya Demokrasia na Utawala bora, Jimmy Luhende.