Monday, November 25

Wadau wa sekta ya bima wametakiwa kukuza, kuboresha  na kuendeleza uwezo wa Bima.

Wadau wa Sekta ya Bima nchini wametakiwa kushirikiana katika kukuza, kuboresha na kuendeleza uwezo wa Bima katika kujikinga na majanga Makubwa.

Akifungua maadhimisho  ya siku ya bima kwa mwaka 2023 kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi, yaliyofanyika ukumbi wa Hotel Verde Mtoni Zanzibar, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema  Serikali ya Mapinduzi  ya Zanzibar inaamini kwamba sekta ya bima ni miongoni mwa sekta za kiuchumi ambazo zitasaidia kuimarisha uchumi wa Zanzibar hasa katika sekta ya Viwanda, Uwekazaji na Uchumi wa Bluu.

Amesema Serikali inatambua na inathamini mchango wa Sekta ya Bima katika kuchochea ukuwaji wa uchumi na ustawi wa Tanzania kwa kuwaletea wananchi maendeleo hivyo, Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi na taratibu bora za uwekezaji ambazo zitasaidia katika kuwavutia wawekezaji katika sekta hiyo.

Ameeleza kuwa dhamira ya Serikali zote mbili ni kuweka usalama kwa wananchi hasa wanapokutwa na Majanga hivyo, Serikali itaendelea kuchukua hatua ya kuendeleza ujuzi kwa wataalamu wa sekta hiyo na uelewa wa bima kwa wananchi wote ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.

Rais Dkt. Mwinyi ameipongeza Mamlaka ya usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA) kwa mabadiliko ya kimuundo,  kisheria na usimamizi wa Sekta hiyo yaliyopelekea biashara ya Bima kuzidi kustawi na kuleta matokeo chanya katika Sekta ya Bima kwa kuwa  nguzo muhimu ya ukuaji wa Uchumi na  kutoa mchango mkubwa kwa maendeleo ya Sekta ya Fedha.

Akimkaribisha Mgeni Rasmi Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mipango Mhe. Ali Suleiman Ameir amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeweka mazingira wezeshi kwa kuifanya Biashara ya Bima kuwa huru na yenye ushindani.

Aidha ameeleza kuwa Sekta ya Bima Zanzibar inakuwa kwa kasi na kutolea mfano kuanzishwa kwa huduma ya Bima ya Kiislamu (ZIC Takaful), Bima ya kina mama (Queen ZIC) hatua ambayo imesaidia kukuza uelewa wa wananchi juu ya Sekta hiyo.

Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR)