Friday, October 18

MHANDISI ZENA ASEMA UTOAJI WA TAARIFA ZA SMZ NI JAMBO LA MSINGI KATIKA KUKUZA UTAWALA BORA WA ZANZIBAR KIMATAIFA

Katibu Mkuu Kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mhandisi Zena Ahmed amesema kuwa Ripoti za Tathmini za Utawala Bora ambazo zinaandaliwa na Taasisi ya Mpango wa Hiyari wa nchi za Umoja wa Afrika (APRM Tanzania) kujitathmini katika vigezo vya utawala Bora zinasaidia sana kutoa mrejesho kwa wananchi hivyo wanaopaswa kutoa taarifa wahakikishe kuwa ni taarifa za uhakika.

Hayo ameyasema Mhandisi Zena katika kikao cha Makatibu Wakuu na Wasaidizi Makatibu Wakuu kilichofanyika katika Ofisi za Katibu Mkuu kiongozi na Katibu wa Baraza la Mapinduzi Maisara, ambapo APRM Tanzania walifanya uwasilishaji kuhusu APRM na maandalizi ya Ripoti ya Pili ya Tathmini ya Utawala Bora Tanzania.

Mhandisi Zena ameongeza kuwa,ni vyema kwa kila Wizara kutafuta muakilishi ambae atafanya kazi ya kutoa taarifa zinazohusiana na Wizara ambazo zitatumiwa na APRM Tanzania kwa lengo la kuingizwa taarifa hizo katika Ripoti hiyo ya Pili ya Tathmini ambayo inalenga kuonesha dunia Utawala Bora Tanzania, na wahakikishe kuwa taarifa hizo zinafanyiwa uhakiki kwa ngazi ya Mawaziri na Makatibu Wakuu kwa vile Ripoti itakayotolewa itasomwa Kimataifa ambayo itatoa picha ya Tanzania.

Katibu Mtendaji wa APRM Tanzania Lamau Mpolo, wakati akifanya uwasilishaji amesema kuwa dhumuni kuu la APRM Tanzania ni kukuza dhana ya Utawala Bora kwa kutekeleza sera, viwango na taratibu zitakazopelekea kuimarika kwa siasa,kuongeza kasi ya ukuaji wa uchumi, uhakika wa maendeleo endelevu na kuharakisha mtangamano wa kikanda na Bara zima la Afrika kwa kubainisha maeneo ambayo zinafanya vizuri na kubadilishana uzoefu katika maeneo ambayo yana changamoto.

Kwa niaba ya Makatibu Wakuu wengine waliohudhuria katika mkutano huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo umwagiliaji, maliasili na mifugo Ndg Seif Shaaban Mwinyi amesema kuwa wamenufaika sana na elimu walioipata kutoka APRM Tanzania, na kuwasisitiza kufanya kazi kwa weledi na ukaribu na Taaasisi nyengine zinazosimamia masuala ya Utawala Bora Tanzania.