Friday, October 18

Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amefanya ziara ya kukagua matengenezo  ya MV. Mapinduzi II Bandarini Malindi Mjini Zanzibar 

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amefanya ziara ya kukagua matengenezo  ya MV. Mapinduzi II Bandarini Malindi Mjini Zanzibar ili kujionea na kujiridhisha hatua iliyofikia ya utengenezaji wa Meli hiyo.

Mhe. Hemed amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoongozwa na Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi imeamua kwa makusudi kuifanyia matengenezo MV. Mapinduzi II ili kuwawezesha  wananchi hasa wa  Pemba na Tanga  kupata usafiri salama na wa uhakika.

Ameeleza kufurahishwa kwake kuona matengenezo ya meli hiyo yanaendelea vizuri na yameshafikia asilimia 70 ambapo inatarajiwa kukamilika ndani ya miezi michache ijayo.

Aidha amefahamisha kuwa kukamilika kwa matengenezo ya Meli hiyo kutaondoa tatizo la usafiri linalowakabili Wazanzibari hasa wakaazi wa Kisiwa cha Pemba ambao hutegemea usafiri wa meli kwa shuhuli zao za usafiri na  biashara.

Mhe. Hemed Amewaagiza wahandisi na wataalamu elekezi kusimamia kwa umakini matengenezo ya meli hiyo na kuheshimu makabuliano ya mkataba ili kuhakikisha wanafanya kazi nzuri na kwa ubora wa hali ya juu.

Ameeleza kuwa Serikali inatumia gharama kubwa katika kuifanyia matengenezo Meli hiyo hivyo, ni wajibu kwa Wakandarasi kuhakikisha wanatumia Vifaa vilivyo bora na vitakavyodumu kwa muda refu.

Amesema Serikali itaendelea kufuatilia kwa karibu na umakini wa hali ya juu kuhakikisha Meli hiyo inakamilika kwa wakati uliopangwa na kwa ubora wa hali ya juu na kuahidi endapo kutatokea changamoto yoyote katika matengnezo hayo hatua za haraka zitachululiwa kuondosha changamoto hizo.

Mhe. Hemed amewaomba wazanzibari kuendelea kuwa wavumilivu katika kipindi kidogo kilichobakia na kuwahakikishia kuwa tatizo la usafiri kati ya Unguja n Pemba litaondoka kipindi kifupi kijacho.

Nae Waziri wa Ujenzi,  Mawasiliano na Uchukuzi Mhe. Dkt. Khalid Salum Muhamed ameeleza kuwa Wizara kupitia Shirika la Meli Zanzibar inafatilia kwa karibu matengenezo hayo ili Meli hiyo ikamilike Mwezi Disemba mwaka huu na kwa ubora uliokusudiwa.

Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR)