Monday, December 30

 SMZ na SMT zimekubali Utekelezaji wa Technolojia ya JUNCAO 

Serikali ya mapinduzi Zanzibar na Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania zimekubali Utekelezaji wa Technolojia ya JUNCAO kuwa ni miongoni mwa teknolojia zitakazosaidia kukuza kilimo na kua endelevu.

Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo, Shamata Shaame Khamis, amesema hayo huko katika Ukumbi wa Wizara hiyo Maruhubi wakati alipokua akifungua warsha ya utambulisho wa mradi wa kuimarisha mfumo wa chakula kupitia tenolojia ya JUNCAO Tanzania.

Alisema lengo la warsha hiyo ni kutambua andiko la utekelezaji wa teknolojia hiyo inayoenda sambamba kuimarisha na kuongeza upatikanaji wa malisho ya mifugo, uzalishaji wa uyoga pamoja na kuhifadhi mazingira.

Shamata alieleza kuwa uzalishaji wa uyoga na upatikanaji wa malisho utaongeza uzalishaji wa mifugo na mazao ya mifugo yatakayosaidia kupunguza umaskini  na kuongeza pato la taifa nchini.

Aidha alifahamisha kuwa mifugo ni miongoni mwa sekta inayokuwa kwa kasi kubwa kutokana na watu wengi kujikita katika shughuli za ufugaji kama ni fursa kubwa ya ajira japokua inakumbana na changamoto kubwa za ukosefu wa upatikanaji wa malisho ya kutosha na athari za mabadiliko ya tabia ya nchi

“Naamini matarajio ya warsha hii yatawafunza na kupata uzoefu ambao utawasidia kupunguza baadhi ya changamoto juu ya upatikanaji wa malisho ya mifugo kwa muda wote hasa katika kipindi cha ukame”, alieleza Shamata.

Sambamba na hayo alisema kuwa matumizi ya uyoga yatafanikisha malengo na mipango ya maendeleo ya serikali kuhusiana na uhakika wa chakula ifikapo mwaka 2030.

Kwa upande wake Mkurugenzi Idara ya maendeleo ya mifugo, Asha Zahran Mohamed, alisema kuwa ana matarajio makubwa kuwa teknolojia hiyo itasaidia kupatikana malisho ya kutosha kwa wanyama hususani ng’ombe wa maziwa.

“Asilimia 70 ya ng’ombe wa maziwa wanahitaji malisho ya majani, hivyo teknolojia ya Juncao inazalisha  malisho kwa wingi na pia yanastahamili ukame hivyo itakua ni mkombozi kwa wafugaji wa Zanzibar”, alifahamisha Asha.

Mapema Mhadhiri mwandamizi na mtaalam wa teknolojia ya Juncao kutoka Chuo cha Sokoine cha Kilimo (SUA), Dk. Elly Ligate, alisema wanategemea kuendelea na majaribio ili kupata majibu ya kisayansi kwenye uzalishaji wa uyoga, malisho ya wanyama na kutunza mifumo ya kiikolojia.

Aidha aliongeza kuwa teknolojia hiyo itaongeza uelewa wa manufaa kwa wadau wengi zaidi ambao ni wakulima, wafugaji na vikundi vinavyojihusisha na utunzaji mazingira kwani kufanya hivyo kutachangia uzalishaji wa mifugo na mazao ya mifugo

“Tunatengeneza ajira na kuongeza kipato kupitia kilimo cha uyoga na malisho bora kwani tutapunguza migogoro kati ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi sambamba na kuibadilisha ardhi iliyochoka kwa kuzalisha malisho ya jamii kwa kuwa nyasi hizi zinastawi hata kwenye ardhi isiyo na rutba”, alisema Dk. Elly.

Msaidizi Malisho wa Shamba la Mbegu na Malisho ya Mifugo Kizimbani,  Ummy Mussa Khamis, aliwataka wafugaji kujitokeza kwa wingi kuchukua mbegu za Juncao kwa ajili ya malisho kwani kufanya hivyo wataondokana na usumbufu wa malisho kwa wanyama wao.

Warsha hiyo ya siku moja imewashirikisha makundi mbali mbali kutoka Tanzania bara na Zanzibar wakiwemo watunga sera, wawezeshaji, watafiti, wataalamu wa fani tofauti, wakulima wa uyoga, wafugaji na wahitimu wa vyuo vikuu.