Makamu Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Zanzibar, Mheshimiwa Othman Masoud Othman ametoa wito kwa Viongozi wa Ngazi mbalimbali kuelewa dhima waliyonayo ili kuhakikisha Watu wote wa Nchi hii wanarudisha Imani ya kuishi kwa heshima na matumaini.
Mheshimiwa Othman ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, ameyasema hayo leo katika Mkutano Maalum wa Viongozi Wapya wa Chama hicho wa ngazi ya Majimbo na Matawi, kutoka Mikoa ya Chake Chake na Mkoani kichama, huko katika Ukumbi wa Samael Gombani, Mkoa wa Kusini Pemba.
Amesema kuwa lazima Safu za Viongozi Wapya wa Chama hicho zijipange na zijitathmini kwa udhati kwa kuzingatia haja ya kutumikia umma wa watu wa Nchi hii, kwa misingi ya Amani, umoja, utulivu, maridhiano na mshikamano, pamoja na kuzingatia dhima ya kuivusha Nchi pahala ilipo.
Akitolea mfano hali halisi ya maisha ilivyo katika visiwa vya Unguja na Pemba, Mheshimiwa Othman ametaja mazingira magumu yanayowakabili vijana, wazee, akinamama na watoto, pamoja na udhaifu katika mifumo ya utoaji wa huduma muhimu za kijamii, ambapo wananchi wanakosa uhakika wa mahitaji yao ya msingi ya kila siku, na hivyo kulazimika kuishi kwa kugombea sadaka.
“Haya hatukuyachagua; Nchi hii si Maskini, bali ni kutokana na kukosekana kwa Viongozi wenye maono; kukosekana kwa Viongozi walio-makini ambao ni wenye azma njema ya kuwaongoza watu kwa misingi ya haki na uadilifu pamoja na kupigania heshima na maendeleo ya watu wote”, ameongeza Mheshimiwa Othman.
“Madola mbalimbali yalipanga na yalikaa pamoja kutaka Zanzibar idhibitiwe; hayo siyo siri yapo hadharani kwani yameandikwa katika Nyaraka, na hao waliofanya hivyo sasa hawana tena haja ya kuona Zanzibar inadhibitiwa; kila zama na kitabu chake”, amefahamisha Mheshimiwa Othman akibainisha hatua mbalimbali ambazo dunia imepita pamoja na kuidhoofisha Nchi hii kiuchumi.
Akiongelea haja ya kukaa pamoja na kuwanasihi Viongozi Wapya kupitia Kikao hicho maalum, Mheshimiwa Othman amesema kuwa Chama hicho hakikuendesha Uchaguzi wa Ndani wa hivi karibuni kwa lengo la kuwapatia watu nafasi za kugombea Ubunge, Uwakilishi na Udiwani, wala kujiwekea safu ya kuungwamkono kwa chaguzi zijazo, bali ni kutokana na kuaminiwa na umma na hivyo wajitathmini juu ya dhima ya kuwatumikia watu wote ipasavyo.
“Tuwatazameni Watu ambao walikubali kusamehe kila kitu, kwaajili kupigania maslahi ya umma na Mamlaka kamili ya Nchi; sisi kuwasaliti hata Mwenyezi Mungu hatokuwa radhi” amesisitiza Mheshimiwa Othman.
Amekaririwa akisema, “kuna waliouwawa, kuna watu waliodhulumiwa, kuna watu waliokimbilia Nje ya Nchi kwasababu ya Madhila, kuna Watu waliovunjiwa Makaazi yao; kuna Watu Waliofukuzwa kazi na Wanaodai kutokana na dhulma mbali mbali; hivyo hayo yote ndugu zangu yanaashiria tuna kazi kubwa na dhima ya kiasi gani ya kuwaongoza na kupigania heshima ya watu wote, na wala lengo siyo kujitafutia vyeo na maslahi binafsi”.
Aidha amesema, “ieleweke kwamba haya siyo ya kisiasa bali ni kutokana na ukweli kwamba maisha ya watu ndani ya Nchi hii yanakoelekea hayaleti matumaini kutokana na ukosefu wa kujipanga, kushindwa kuzingatia haki na uadilifu, na pia kukosekana kwa hisia za kujali dhamana na maadili ya uongozi”.
“Na sasa kwamba tunajiandaa kwa safari lazima tufahamishane tunakotoka ni wapi, na wapi tunajipanga kuelekea”, ameongeza Mheshimiwa Othman akipongeza mwitikio wa Viongozi Wapya wa Chama sambamba na Wagombea walioshindwa kupitia zoezi la Uchaguzi huo.
Akifahamisha juu ya mazingatio muhimu kupitia Zoezi la kuwapata Viongozi hao Wapya, baada ya Uchaguzi huo wa Ndani ya Chama hicho wa hivi karibuni, Mheshimiwa Othman amekariri ile Kaulimbiu isemayo, “tuchague mmoja tubaki wamoja”, kwa azma aliyoitaja kufuta machungu na hisia za kukata tamaa miongoni mwa Wagombea walioshindwa.
Mheshimiwa Othman amechukua fursa hiyo kuwapongeza Wanachama waliojitokeza kwa wingi kugombea Nafasi mbalimbali za Uongozi wa Chama hicho, kupitia Mchakato wa Uchaguzi wa Ndani ya chama wa hivi karibuni, na pia kueleza matumaini aliyonayo kutokana na umoja, mshikamano na maridhiano ya wanachama, hali inayoashiria mwendelezo wa uimara, hasa baada ya matokeo ya kushinda na kushindwa.
“Tutoke na Misingi hii ya Uongozi mimi naamini tutafanikiwa; kwa kufanya hivyo, sisi tumefanya darasa la demokrasia kwani safari hii tunataka tuonyeshe vipi viongozi wa kuwaongoza watu wanapatikana na vipi Nchi inaongozwa; nawaomba sote Viongozi tuwe na dhamira njema ya kuwatumikia watu ambao wametuamini”, amesema Mheshimiwa Othman akitangaza kuwa yeye binafsi hana Mgombea wa ‘mbeleko’ ndani ya Chama hicho huku akikemea tabia ya ‘double face (sura mbili)’.
Hivyo amesema wajibu wa kiongozi ni kuepusha na kutatua tatizo kwa umoja, Imani, mashirikiano, nia safi na kuvumiliana, wala siyo kulalamika na kufitinisha, huku akikariri ule usemi kwamba, “ukiona giza washa mshumaa kwani giza haliondoki kwa malalamiko”.
Naye, Kaimu Naibu Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo Zanzibar, Bw. Salim Bimani, amesema Safu Mpya ya Uongozi wa Chama hicho ni nyenzo muhimu kuelekea safari ya kutetea heshima ya Visiwa vya Unguja na Pemba, kupitia Uchaguzi hapo ifikapo Mwaka 2025, na kuunda Serikali ambayo Viongozi wake watajali thamani na maslahi ya watu wote bila ubaguzi.
Akikumbusha hatua mbambali za Historia ya Harakati za Mageuzi Nchini, na Machungu ambayo Wapinzani wameyapata, Bimani ameitumia fursa ya kuihutubia hadhira hiyo kubwa kuwakumbusha Viongozi hao Wapya na kuwataka waelewe kwamba, kama ilivyokuwa kwa Waasisi wa Siasa za Kutetea Mamlaka na Heshima ya Zanzibar, akiwemo aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais, Marehemu Maalim Seif Sharif Hamad na Wenzake, dhamira siyo kupigania vyeo na nafasi za kuongoza, bali kuweka kando tamaa, fitna na ubinafsi, kwaajili ya Umoja wa Kitaifa na Maslahi ya Umma.
Mratib wa ACT-Wazalendo kisiwani Pemba, Bw. Said Ali Mbarouk akitoa Ripoti ya Kisiasa ya Chama chake amefahamisha kuwa hali ya kujitolea kwa hali na mali kwa wanachama, wapenzi na wafuasi wake, ni ishara ya kuendelea kwa uimara, uthibiti na utayari wa Wapemba katika kuipigania Mamlaka Kamili ya Zanzibar.
“Pemba tupo tayari Waheshimiwa, tunachosubiri ni maelekezo na miongozo ya viongozi wetu, na tunachongojea ni ushindi ifikapo Mwaka Elfu Mbili na Ishirini na Tano”, amesema Mbarouk.
Kwa upande wake, Naibu Katibu wa Chaguzi wa ACT-Wazalendo, Bw. Muhene Said Rashid amerudia kauli yake kwamba Zoezi la kuwapata Viongozi wa Ngazi zote wa Chama hicho, kuanzia Matawi yote takriban 678 na Majimbo 50 ya Unguja na Pemba, lililoanza mwezi wa Agosti, Mwaka huu, limeendelea vyema na kufikia asilimia 93.8, licha ya dharura ndogo ndogo za kibinaadamu zilitatuliwa hatimaye katika maeneo machache, ikiwemo Jimbo la Mkoani.
Mkutano huo maalum ulioanza kwa Dua iliyosomwa na Sheikh Mohamed Mbwana kutoka Chambani, sambamba na Burudani mbalimbali za Kisiwani hapa, zikiwemo za Wasanii Mashuhuri, akiwemo Vuale Omar Vuale ‘Walanlahoa’ na Yahya Hilal, umelenga katika Kuwakusanya baadhi ya Watendaji Wakuu wa wakiwemo Wenyekiti na Makatibu wa Matawi, Majimbo na Mikoa, Wabunge, Wajumbe wa Kamati Kuu na Halmashauri Kuu, pamoja na Kuwahutubia Viongozi Wapya wa Mikoa ya Chake Chake na Mkoani, Mkoa wa Kusini Pemba, waliopatikana kupitia Mchakato wa hivi karibuni wa Uchaguzi, ndani ya Chama hicho.
Mheshimiwa Othman ambaye ameambatana na Mke wake, Mama Zainab Kombo Shaib, yupo Kisiwani Pemba, kwa Ziara Maalum ya Siku 4 kwaajili ya Shughuli za Chama na Serikali, tangu aliopowasili mapema Ijumaa, na kupokelewa na Viongozi mbalimbali wa Serikali pamoja na Wakuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama.
Kitengo cha Habari,
Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar,