Sunday, November 24

Mkurugenzi Jamali awashauri wafanyakazi kujiandaa mapema

NA ABDI SULEIMAN, PEMBA.

WAFANYAKAZI wa Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA) Ofisi ya Pemba, wameshauriwa kujiandaa mapema kimaisha, ili muda wa kustaafu unapofika sio kuanza kufikiria ataishi vipi mitaani.

Ushauri huo umetolewa na Mkurugenzi wa mamlaka hiyo Pemba Jamal Hassan Jamali, wakati wa hafla ya kuwaaga na kuwakabidhi zawadi waliokua wafanyakazi wa taasisi hiyo, baada ya kumaliza muda wao wa utumishi serikalini, halfa iliyofanyika katika ofisi za Mamlaka hiyo Gombani.

Alisema mfanyakazi anapaswa kujiwekea hakiba au kujiandalia mazingira yake mapema, kabla ya kustaafu kwani muda wa utumishi wake serikali unapomalizika, kinwamgongo chake aweze kukitumia kwa shuhuli nyengine za kimaisha.

“Haipendezi kumuona mfanyakazi wa serikali mpaka anamaliza muda wake wa utumishi, hana alichojiandalia huko mbele na kuanza kupita na kuomba omba, vizuri tukaanza sasa mipango yetu ya baadae,”alisema.

Aidha suala la kustaafu ni moja ya masomo muhimu katika maisha ya mwanaadamu, lazima kuzingatia na kujua nini unataka kufanya, huku akiwatakia kilala kheri na mafanikio katika maisha yao ya kuishi nje ya ZRA.

“Tulikuwa na nyinyi miaka mingi sana, utaratibu utafanya kazi mwisho wake utaondoka na kwenda kuanza maisha mapya, unapokua sehemu yoyote lazima hili lizingatiwe kuna siku tutakua njee ya ofisi zetu,”alisema.

Kwa upande wake Mstaafu Khamis Juma aliwashukuru Viongozi walioteuliwa kushika nafasi hizo, kuhakikisha wanaendelea kuishi vizuri na wafanyakazi wenzao muda wote ili malengo ya serikali yaweze kufikiwa.

Alisema katika kutekeleza kazi hizo kunachangamoto nzito, kila siku majukumu yanapanda juu, hivyo aliwasihi kuendelea kushikamana, kuheshimiana na kuaminia muda wote wa kazi.

“Sina cha kuwapatia zaidi kuwapongeza kwa kupata nafasi mpya, nafasi yetu ya kazi ni nzuri huko nje ukionekana, lakini matatizo yaliyopo kwenye kazi makubwa, tunapaswa tuendelea kutoa huduma nzuri kwa watu tunaowahudumia,”alisema.

Nae Mstaafu Mussa Abdalla, aliwataka viongozi walioteuliwa kutambua kuwa wanamajukumu mazito katika utendaji wa kazi zao, kwa kuhakikisha wanafikia malengo yao

“Sisi saivi tumeshamaliza muda wetu lakini mukitutaka muda wote tupo tayari kuwasaidia mawazao, fikra ili yale malengo muliopewa yaweze kufikiwa,”alisema.

Hata hivyo aliwashukuru wafanyakazi wenzake kwa kuwapatia mashirikiano muda wote wa utumishi wao katika mamlaka hiyo, huku akiwataka kusamehana kwa waliokoseana.

Wafanyakazi hao wameweza kukabidhiwa mafriji kila mmoja kutoka,ikiwa ni utaratibu kwa wafanyakazi wa mamlaka hiyo kila anapostaafu kuagana na kupeana Zawadi.

MWISHO