NA AMINA AHMED-PEMBA.
WADAU wa sheria kutoka Taassisi mbali mbali za Serikali pamoja na taasisi binafsi kisiwani Pemba wameshiriki katika mkutano maalumu wa kujadili na kutoa Maoni katika rasimu ya sheria ya kuanzishwa mahakama maalum ya rushwa na uhujumu uchumi uliondaliwa na ofisi ya mwanasheria mkuu Zanzibar wenye lengo la kuboresha na kupatikana kwa sheria bora itakayosimamia masuala hayo.
Wakitoa maoni yao mara baada ya kufanyiwa mapitio ya rasimu hiyo baadhi ya wadau hao akiwemo Muhammed Ali Muhammed kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka, Simba Khamis Simba kutoka kikosi cha kuzuia magendo Zanzibar (KMKM) wameiomba kamati inayosimamia rasimu hiyo kuongeza Vifungu vya sheria ambavyo vitaweza kusimamia suala la usafirishaji haram wa magendo ya karafuu, mazao ya baharini pamoja na usafiriahaji haramu wa binaadamu.
Wamesema miongoni mwa mapungufu ambayo yamejitokeza katika rasimu ya sheria hiyo ni kukosekana kwa vifungu vinavyoonesha masuala ya rushwa na uhujumu wa uchumi katika zao la karafuu na mazao mengine ya baharini pamoja na Usafirishaji wa binaadamu ambapo kuingizwa vipengele hivyo kutasaidia kuisaidia serikali ya Zanzibar kutimiza azma yake kukuza na kuimarisha zaidi sekta ya uchumi wa buluu pamoja na biashara.
Aidha kwa upande wao Asya Issa Hemed , Neema Juma pamoja na Seif Muhammed Khamis hakimu mahakama ya mkoa Kaskazini hakimu mahakama wilaya pamoja na Wakili wa Seriki kutoka ofisi ya mkurugenzi wa mashtaka Wameiomba kamati hiyo kuondoa vipengele vilivyoweka ukomo wa kusikilizwa kesi na badala yake kutoweka ukomo huo kuongeza faini kubwa isiyopungua Milioni 100 badala ya milioni 50.
Awali akizungumza na wadau hao kaimu Mrajisi wa Mahakama Kuu Pemba Faraji Shomari Juma amesema lengo la kuwakutanisha wadau hao wa masuala ya kisheria kutoka taassisi mbali mbali ni kuongeza maboresho kwa kupata mawazo bora zaidi katika kuimarisha rasimu hiyo ambayo yatasaidia kupatikana kwa sheria bora itakayoweza kusimamia masuala ya rushwa na uhujumu wa uchumi.
Akizungumza mara baada ya kutolewa maoni hayo katibu wa kamati maalumu ya kukusanya maoni juu ya sheria ya kuanzishwa mahakama maalum ya kuzuia Rushwa na Uhujumu wa uchumi Zanzibar Said Salum Said ambae pia ni wakili wa Serikali kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu Zanzibar ameahidi kuyafikisha maoni hayo yaliyotolewa na wadau hao ili kuweza kufanyiwa kazi.
Mkutano huo uliofanyika katika ukumbi wa baraza la mji Chake Chake umejumuisha wadau wa sheria kutoka Taasisi mbali mbali ikiwemo Mamlaka ya kuzuia Rushwa na uhujumu uchumi, Jeshi la Polisi mahakimu wa mahakama za Wilaya na Mkoa , Mawakili wa kujitegemea kutoka taasisi za serikali na binafsi, waendesha Mashtaka wa Serikali, Waasheria wa Serikali, wadau kutoka mamlaka ya kudhibiti dawa za kulevya, pamoja na KMKM, ambapo Kujadiliwa kwa rasimu hiyo ya kuanzishwa kwa mahakama maalum ya kupambana na rushwa na uhujumu uchumi Zanzibar ni utekelezaji wa agizo la rais wa Zanzibar Dk Hussein Ali Mwinyi alilolitoa Siku ya sheria juu ya kuanzishwa kwa mahakama hiyo maalumu.