Wednesday, January 15

Maabara ya Afya ya Jamii Pemba ni ushirikiano tosha wa Serikali ya Marekani na Tanzania

BAKAR MUSSA , PEMBA

Uwepo wa Maabara ya Afya ya Jamii Pemba ni mfano mzuri wa mabadiliko ya ubunifu na ushirikiano baina ya Serikali ya Marekani na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Hayo yalielezwa na Balozi wa Marekani nchini Tanzania , Michael Battle huko katika ukumbi wa Maabara ya Afya ya Jamii Pemba, wakati akizungumza na Watendaji wa maabara hiyo wakiongozwa na Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Hassan Khamis Hafidh mara baada ya kumaliza ziara yake katika maabara hiyo.

Alieleza Serikali ya Marekani sio tu inathibitisha dhamira ya kusaidia mfumo wa Afya wa Tanzania lakini pia inaangazia umuhimu wa maabara ya Pemba kama kielelezo cha utafiti na maendeleo ya afya ya Umma.

Balozi wa Marekani nchini Tanzania mheshimiwa Michael Battle alipongeza maboresho na Maendeleo yaliofikiwa katika Maabara ya Afya ya jamii iliopo Wawi Kisiwani Pemba kutokana na utendaji wake mkubwa.

“Maboresho haya yaliofanyika yametokana kwa ufadhili wa fedha za mpango wa uokoaji wa Marekani wa mwaka 2021(ARPA) kupitia kituo cha Kudhibiti na Kuzuwia Magonjwa (CDC) na Shirika la MDH,” alisema.

Alieleza kuwa kuanzishwa kwa Maabara ya Afya ya jamii Zanzibar, kunaboresha utafiti na upatikanaji wa vipimo vya COVID -19 na hivyo kunasaidia utafiti wa maradhi mbali mbali.

Aidha kuwepo kwa Maabara hiyo Zanzibar kunapunguza muda wa kusubiri majibu ya vipimo,kunaimarisha udhibiti na mbinu za kukabiliana na Magonjwa kwa zaidi ya wakaazi million 1.8 wa Zanzibar na Watalii zaidi ya 390,000 wanaotembelea visiwani humo kila mwaka.

“Watalii zaidi ya 390,000 wanaotembelea visiwani Zanzibar kila mwaka hupata udhibiti na mbinu za kukabiliana na Magonjwa kupitia Maabara hii,’ilielezwa.

Mkurugenzi wa Maabara ya afya ya Jamii Pemba Dk, Said Mohamed Ali alisema  kuwa Maabara ya Afya ya Umma ni kituo cha kisiasa kinachojishuhulisha na upimaji na utafiti wa Magonjwa ya mripuko na ya kuambukiza ili kusaidia tiba na kutengeneza suluhu za kibunifu za kukabiliana na Magonjwa hayo.

“Maabara hii inateknolojia ya kisasa na ina timu ya Wataalamu waliobobea ,wanaolenga kuboresha Afya na kuokoa maisha ya wakaazi wa Pemba na maeneo mengine”, imeelezwa.

Alifahamishwa kuwa Shirika la Menejimenti na Maendeleo ya Afya MDH  limesaidia ununuzi wa mashine za kisasa ,vitendanishi na vifaa tiba pamoja na kutowa Ushauri wa kitaalamu na mafunzo kwa Wataalamu wa Maabara.

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Afya Zanzibar Hassan Khamis Khafidh  alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi  Zanzibar  itaendeleza mashirikiano na Serikali ya Marekeni na Serikali ya Jamhuri ya Mungango wa Tanzania kutokana na juhudi wanazozichukua za kuiletea maendeleo Nchi yao katika miundo mbinu mbali mbali ikiwemo sekta ya afya .

Alieleza kuwa Wizara ya Afya Zanzibar imefuarahi vya kutosha    baada ya kukamilika kwa ziara ya Balozi wa Marekani anayefanyia kazi zake Tanzania kufika katika  Maabara hiyo  kuangalia maendeleo ya kazi zinazofanyika kwa vile ni wadau wakubwa wanao jitolea kusaidia maabara hiyo kwa shughuli za kiuchunguzi.

Naibu Waziri huyo alisema Serikali ya Marekani imekuwa ikifanya juhudi kubwa kukifanya kituo hicho kiendelee zaidi katika kazi zake za utafiti  wa magonjwa ya milipuko na yale yasioambukiza kama kichocho na minyoo.

Alifahamisha kuwa Serikali ya Marekani mbali na shuhuli hizo  pia imekuwa ikitowa huduma za mradi wa kuwapitia akina mama wajawazito majumbani kwa kuwapima afya zao na kuwapatia matibabu kwa lengo la kuepusha vifo vitokanavyo na uzazi .

“Kuanzishwa kwa Maabara hii kwa Visiwa vya Zanzibar kunaboresha huduma mbali mbali za kiutafiti na imekua ni kituo kimoja wapo cha kutoa elimu kutoka Nchi mbali mbali duniani kwa kupata uwelewa kwa mambo ya kiuchunguzi”, alisema .

Alisema Ushirikiano baina ya Serikali ya Marekani na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia  ziara hii kwao imewadhihirishia mashirikiano mazuri ya Udugu uliopo baina yao.

Kwa Upande wake Dr,David Sando,Afisa Mtendaji Mkuu  wa Shirika la (M D H) alisema shirika lao limekua likisaidia Serikali mbili ya Tanzania bara na  Zanzibar  hivyo wameanza kuipatia Maabara hivyo vifaa tiba vya Uchunguzi kikiwemo kipimo cha uchunguzi wa damu (DNA) na maradhi mbali mbali .

Aidha alifafanua kwamba vifaa vilivyo katika Maabara hiyo vina  uwezo mkubwa wa kufanyia kazi za Uchunguzi na vipimo kwani vina hadhi ya kimataifa na kutambulika kwake kwa  ubora wake.

“Ninawaomba  wananchi kuitumia maabara hii kwa  kuweza kupata urahisi wa magonjwa yao na kutibiwa juu ya maradhi yanayowasumbuwa”, alieleza.

Alieleza kwamba shirika lao la MDH kupitia CDC ,ARPA, limekuwa ikisaidia huduma na matengezo ya vifaa vyenye usalama kwa ajili ya kujikinga na ugonjwa wa miripuko ukiwemo wa magonjwa kama vile Ebola, Monkey Pox, Homa ya Manjano na maradhi mengine yanayoweza kuzuilika bila ya kusababisha miripuko.

Katika ziara hiyo Balozi alitembelea Maabara hiyo ya kisasa na kujionea vitendea kazi muhimu vya kuifanyia kazi katika kukabiliana na changamoto mbali mbali za Afya ya jamii.

Hata hivyo Balozi alikutana na timu ya Wataalamu kutoka MDH na PHL pamoja na Wawakilishi kutoka CDC na Wizara ya Afya Zanzibar na Tanzania bara, Maabara ya Afya ya Umma Pemba mfano mzuri wa mabadiliko ya ubunifu na ushirikiano kati ya Serikali ya Marekani na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

  

MWISHO.