Friday, February 28

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe Hemed Suleiman Abdulla azungumza na wadau wa Bandari.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe Hemed Suleiman Abdulla amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imemkabidhi muwekezaji kusimamia huduma za uendeshaji wa Bandari ya Zanzibar ili kurahisisha upatikanaji wa huduma bora kwa wafanayabishara na wananchi.

Ameyasema hayo alipokutana na wadau wa Bandari wakiwemo Mawakala wa ushushaji na upakiaji wa mizigo, wamiliki wa meli na wamiliki wa majahazi pamoja na wafanyabiashara katika kutathmini utendaji na uendeshaji wa shughuli za bandari.

Mhe. Hemed amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inayoongozwa na Rais Dkt. Hussen Ali Mwinyi ina dhamira njema ya kuleta mabadiliko ya kiutendaji katika Sekta ya Bandari kwa lengo la kuleta ufanisi wa huduma za bandari.

Amefahamisha kuwa lengo la kupewa Muwekezaji kuiendesha Bandari ya Zanzibar ni kujenga nidhamu hasa katika ufanyaji wa kazi na kuwaondoshea usumbufu wadau wa bandari jambo ambalo litaongeza pato kwa Serikali na kuwapunguzia gharama za bidhaa wananchi wake.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amewataka Wadau wa bandari kukubaliana na mabadiliko yatakayojitokeza mara baada ya kuanza kazi kwa kampuni ya AGL na kuhakikisha kuwa Serikali kupitia Shirika la Bandari itafanya kazi na Muwekezaji huyo kwa kumpa miongozo ili kufanikisha utendaji wake.

Amewahakikishia Mawakala na wadau wa Bandari kuwa changamoto ya huduma za fedha na mfumo wa malipo unaotumika sasa zitafanyiwa kazi kwa haraka ili kuenda sambamba na azma ya Serikali.

Ameeleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar ni sikivu na inapokea maoni na ushauri kutoka wananchi hivyo, ni vyema wadau hao kutumia busara na kufuata taratibu na Sheria kwa kuwasilisha changamoto zitazojitokeza.

Nae waziri wa  Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Mhe.  Dkt Khalid Salum Muhamed  amesema ili nchi ipige hatua kimaendeleo na iuchumi uzidi kukuwa na kuimarika lazima kuwepo na ufanisi katika utendaji kazi hasa katika Sekta muhimu kama Bandari hivyo, kuwepo kwa Muwekezaji katika Bandari ya Zanzibar kutaleta ufanisi mkubwa wa kazi na kuondoa changamoto za kusuasua kwa utendaji kazi na malalamiko yaliyokuwepo kwa muda mrefu.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Fedha na Mapingo Mhe. Dkt. Saada Mkuya Salum amesema ipo haja ya kutolewa elimu kwa wadau na wananchi katika utoaji wa huduma za bandari.

Amesema wapo baadhi ya wafanyabiashara wameanza kupandisha bei za bidhaa kwa kisingizio cha kupanda kwa tozo na kodi na kusema yoyote atakaebainika kufanya hivyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake.

Akizungumza kwa niaba ya Mawakala wenzake Omar khamis Mussa Mwenyekiti wa wakala wa forodha amesema changamoto kubwa iliyojitokeza ni kukosa uelewa na taarifa sahihi juu ya muwekezaji huyo hali inayowapa ugumu wadau wengi wa Bandari kukabiliana na mabadiliko yaliyojitokeza mara tu baada ya kuanza kazi kwa Muwekezaji huyo.

Amesema mfumo uliopo sasa Bandarini hautoshelezi kulingana na wingi wa wateja, ugeni wa mfumo huo na watendaji wasio na kasi katika kuwahudumia wateja hivyo, ipo haja Serikali kuiangalia umakini chamgamoto hiyo.

Ndugu Omar amewataka wafanyabishara wenzake kukubaliana na mabadiliko yoyote yatakayojitokeza na kuendelea kuwa watulivu katika kipindi hiki ambacho serikali inazifanyia kazi changamoto hizo.

Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya AGL Group Bwana Nicolas David Es-calin  ameeleza kuwa lengo la kuwekeza katika bandari ni kurahisisha huduma za bandari pamoja kuifanya bandari ya malindi kuwa na huduma za hadhi ya kimaitaifa.

Baada ya kikao hicho Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitembelea maeneo mbali mbali bandarini hapo ikiwa ni pamoja na maeneo ya kuegesha Madau.

Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR)