NA ABDI SULEIMAN, PEMBA
MDHAMINI wa shirika la Biashara la Taifa Zanzibar (ZSTC) Pemba Abdalla Ali Ussi, amewashauri wakulima wa zao la karafuu Kisiwani humo, kuendelea kupokea fedha zao za mauzo ya karafuu kwa kutumia mtandao wa TigoPesa.
Alisema asilimia 85 ya wakulima kisiwani hapa, bado wanapokelea fedha zao mkononi, jambo ambalo linasababisha upotevu wa fedha kwa shirika na baadhi ya wateja kuibiwa fedha zao.
Mdhamini huyo aliyaeleza hayo katika hafla ya kuwakabidhi zawadi kwa wakulima bora wa karafuu, ambao wametumia huduma ya TigoPesa wakati wakupokea malipo yao kwa kipindi cha mwezi wa Agosti 2023.
Alisema ZSTC inatumia njia tatu za kulipa fedha kwa wakulima baada ya kuuza karafuu zao katika shirika hilo, moja Bank, TigoPesa na pesa mkononi kwa wale wenye Pishi moja hadi gunia moja.
“Niseme ukweli TigoPesa ni ya urahisi zaidi na haichelewi, baada ya kumaliza taratibu zako hufiki nyumbani mzigo umesoma nivizuri tukatumia njia hii kwa sasa kupokea malipo ikizingatiwa makato yamepunguzwa,”alisema.
Aidha alisema bado wanamasikito makubwa kutoka kwa wakulima Pemba, kuendelea kupokea fedha mkononi jambo ambalo linasababisha hasara kwa shirika kutokana na ufatiliaji wa fedha na ulinzi.
Hata hivyo aliipongeza kampuni ya Tigo Zantel, kwa uamuzi wao wa kuwapa hamasa wakulima wa zao la kafaruu kwa kuwapatia zawadi, wakulima wanaofanya vizuri kwenye uzaji wa karafuu kwa kutumia huduma ya tigopesa.
“Kitendo hichi kitawafanya baadhi wakulima wengi kuhamasika, kutumia huduma ya TigoPesa kupokelea fedha zao baada ya kuuza karafuu zao,”alisema.
Kwa upande wake meneja wa Tigo Zanzibar Salum Nassor Mohamed, aliwashukuru wateja hao kwa uamuzi wao wa kutumia tigopesa kupokelea fedha zao, kwani wameisadia Serekali gharama za upotevu wa fedha, na fedha zao kuziweka sehemu salama.
“Leo tumeamua kuwatambua wale ambao wametumia huduma ya tigoPesa, kwa kupokea fedha zao za mauzo mara nyingi zaidi au kiwango kikubwa, sisi tumeamua kuwapa hamasa na kutahmini maamuzi yao,”alisema.
Aidha aliwataka wakulima wa karafuu ambao bado hawatumia huduma ya tigopesa, watumie kwani ni mwanzo na mategemeo yao ni kutoa zawadi nyingi zaidi.
Nae mkulima wa zao la karafuu kutoka Kengeja Mohd Abdalla Mohd, amelitaka shirika la Biashara la Taifa (ZSTC) msimu unaokuja kutoa bei mapema kabla hawajakodi mashamba, ili kuondosha usumbufu baina ya mkulima na mwenye mashamba.
Alisema matajiri wengi wa karafuu wanakodi mashamba kutoka kwa wakulima, pale bei inapopanda ya karafuu hupelekea msuguwano nao kutaka kuongeza bei ya mashamba ilhali tayari wameshayakodisha.
Akizungumzia kuhusu upokeaji wa fedha zake, alisema TigoPesa ni njia rahisi, isiyochelewa kwani fedha zao wanazipata kabla ya kurudi majumbani kwao.
Nae mkulima Shehe Saleh Sultan, aliwataka wakulima wa zao la karafuu kupokelea fedha zao kwa kutumia huduma ya TigoPesa, wakati wanapokwenda kuuza zao la karafuu, kwani huduma hiyo inaondosha foleni na kuepusha vibaka na upotevu wa fedha.
Zaidi ya wakulima 10 wa zao la karafuu kisiwani Pemba, ambao wametumia huduma ya Tigo pesa kupokelea fedha zao, kwa msimu wa mwezi wa Augost 2023 na kupatiwa zawadi mbali mbali kutoka kampuni ya Tigo Zantel.
MWISHO.