NA FATMA HAMAD, PEMBA
KUKOSEKANA kwa huduma ya maji safi na salama, katika kituo cha Afya Wesha wilaya ya Chake chake, Pemba kunawalazimu wajawazito kujifungulia majumbani, jambo ambalo linahatarisha maisha ya mama na mtoto.
Wakizungumza na waandishi wa habari kituoni hapo, wajawazito hao walisema wamekuwa wakipata shida hususani wakati wanapokwenda kujifungua, kwani hulazimika kwenda na ndoo zao za maji.
Walisema, wanategemea maji kutoka Mamlaka ya maji Zanzibar ‘ZAWA’
lakini ni zaidi ya miezi mitatu, hakuna huduma hiyo, hali inayopelekea usumbufu kwa wajawazito na kushindwa kujifungulia kituoni hapo.
Mmoja kati ya mama hao Asha Omar alisema wengi wao huona ni bora tu wajifungulie majumbani, kwa kuhofia kutokuwa na maji ya kujisafishia, baada ya kujifunguwa kwani kwa hali ya kawaida maji ya kwenye kidumu au ndoo kwa mzazi ni adhabu.
‘’Tunapokwenda kujifunguwa waume zetu wanalazimika wabeba madumu ya maji, kupeleka hosptali na wala hayatutoshelezi, maana baada ya kujiweka usafi inakuwa ni kufanya uchafu,’’alisema.
Nae Subira Iddi Ali, alisema tatizo hilo la ukosefu wa maji katika kituo hicho, linachangia kukosa vipimo muhimu kama cha mkojo na hivyo hulazimika kwenda hospitali ya wilaya ya Chake chake kufuata huduma hiyo.
“Tumekuja cliniki kupima kipimo cha mkojo hatukupata kwani maji hapana, hivyo inatubidi tuende Chake chake, nauli yenyewe ya kwenda huko ni shida tunateseka,’’alieleza.
Said Mohamed Ali na Juma Bakar walisema wanalazimika kubeba madumu ya maji, wanapowasindikiza wenza wao kituo cha Afya, wakati wa kujifungua, jambo ambalo ni gumu kwao kwa vile wakati mwengine wanakuwa hawapo.
Kwa upande wake Muuguzi mkunga wa kituo hicho Amina Ali Abdi, alisema ili mzazi aweze kuzalishwa kituoni hapo, ni lazima aende na maji yake kutoka nyumbani kwake.
Alisema iwapo tatizo hilo halikupatiwa ufumbuzi, linaweza likawapelekea wauguzi wa kituo hicho, kupata maradhi hatarishi ya mambukizi kama vile homa ya ini.
‘’Hata aje na hayo maji kwenye dumu, hayatoshi kumsafishia mzazi, linalobaki ni kupakizana vimelea vya mzazi,’’alisema.
Daktari mkuu wa kituo cha Afya Wesha Abdulnassir Hemed Said alieleza kwa mwezi mmoja, wamekuwa wakizalisha wajawazito kati ya wanane (8) hadi 10, idadi ambayo ingeongezeka kama huduma ya maji yengekuwepo.
“ Wazazi wa eneo hili, wamekosa imani na kituo hicho, kutokana na kadhia hiyo inayowakabili kwa sasa na ndio maana wengi hukikimbia kituo hicho kuzalia”,alisema.
Akitaja matatizo anayoweza kuyapata mama anaejifungulia nyumbani afisa ufuatiliaji na tathmini Tume ya ukimwi Zanzibar ofisi ya Pemba Abdi Nassor Abdi, alisema ni kutokwa na damu nyingi pamoja na kunyemelewa na maambukizi ya maradhi mbalimbali ikiwemo ukimwi.
Afisa uhusiano wa Mamlaka ya Maji (ZAWA) Pemba Suleiman Anass Massoud, alikiri kuwepo kwa tatizo hilo kituoni hapo, ambapo wamebaini kuwa chanzo kikubwa kinachopelekea kukosa maji katika maeneo hayo.
Alieleza kuwa shida hiyo imesababishwa na baadhi ya wananchi kujiungia maji kinyume na utaratibu, na kupeleke kupasuka kwa njia kuu ‘lain’ za kusambazia huduma hiyo.
“Lakini mafundi wako kwenye mchakato wa kufanya matengenezo, ili kuona huduma hiyo inapatikana kwa haraka ili huduma kituoni hapo ziimarike”, alisema.
Nae Mratibu wa mradi wa kuendeleza utetezi wa vyombo vya habari juu ya haki ya Afya ya Uzazi kwa wanawake na wasichana kutoka TAMWA Zanzibar Zaina Abdalla Mzee, alisema lengo ni kutathmini hali ya utolewaji wa huduma, changamoto zinazo wakabili.
Afisa Mdhamini wizara ya Afya Pemba Khamis Bilali Ali alisema ni kweli kuna tatizo la maji katika baadhi ya vituo vya afya, na kwa sasa wizara ina mpango wa kuchimba Visima katika kila kituo kinachotoa huduma ya kuzalisha ili kuona maji yanapatikana kwa wingi.
Kwa mujibu wa Taarifa ya wizara ya Afya Zanzibar, inaeleza kuwa, kipindi cha mwezi mwezi Julai 2020 hadi Machi, 2021, vifo vya mama 44 na watoto wachanga 1,201 viliripotiwa katika hospitali zinazotoa huduma za uzazi.
Moja ya sababu ya vifo hivyo, ilitajwa ni kifafa cha mimba, upungufu wa damu wakati wa ujauzito, kupoteza damu wakati wa ujauzito pamoja na kisukari na maradhi mengine sugu wakati wa ujauzito.
Imefahamika kua, wajawazito 46,050 walihudhuria kliniki ya upimaji mimba angalau mara moja katika kipindi cha ujauzito, ambapo idadi hii ni kubwa ukilinganisha na wajawazito 40,177 kwa mwaka wa fedha 2019 na mwaka 2020.
Imeripotiwa kuwa, katika kipindi hicho, wajawazito 33,057 sawa asilimia 61.3, walijifungua katika hospitali.
SERA NA SHERIA.
Sera ya wizara ya Afya ya Zanzibar ya mwaka 1990 ni kuhakikisha inaimarisha huduma za afya ya uzazi ya mama na mtoto, ili kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi pamoja na vya watoto wachanga.
Ziara hiyo iliandaliwa na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania Zanzibar ( TAMWA-ZNZ) kwa kushirikiana na Maafisa kutoka Tume ya UKIMWI, Kitengo Shirikishi Afya ya Mama na Mtoto na Wandishi kutoka vyombo vya habari tofauti kwa ufadhili wa shirika la WELLSPRING PHILANTHROPIC FUND ambapo walitembelea Vituo vya afya mama na mtoto ikiwemo kituo cha Afya Wesha, Mgelema,Pujini na Vikunguni katika wilaya ya Chake chake Pemba.
MWISHO.