Sunday, January 5

MAKALA: KWA PAMOJA TUPINGE UKATILI WA KIJINSIA KULIOKOA TAIFA.

NA THUREYA GHALIB PEMBA.

Unaposikia neno Ukatili wa kijinsia ,mawazo yako moja moja yatakupeleka kwenye maana ya mateso yanayofanywa kwenye jinsia iwe ya kiume au yakike ,pia unaweza kuwaza ni mateso yanayoumiza mwili na Akili .

Maana halisi ya Ukatili wa kijinsia ni kitendo chochote ambacho kinaweza kusababisha madhara ya kimwili ,kingono na kisaikolojia au mateso kwa jamii ikiwa nikutisha maisha au kunyimwa uhuru iwe hadharani au kificho .

Asilimia kubwa ya watu wamekua wakipitia katika hali hizo za ukatili ambazo nimezielezea hapo Juu ,lakini wengi wao wakiwa wanaficha kujionesha kuwa na wao ni miongoni mwa waathirika wa ukatili huo .

Jambo la kusikitisha wengi wa wafanyaji Ukatili ni watu wa karibu katika Familia ,kitu ambacho kinapelekea sababu kubwa ya kuvifichwa  kwa vitendo hivi.

Kwa muktadha huo mwandishi wa Makala haya hakulenga kuelezea maana tu ya Ukatili wa kijinsia ,lengo lake nikufahamisha sababu zinazopelekea kuongezeka kwa maswala ya Liwati (kulawiti).

Liwati ni kitendo kibaya ambacho kimelaaniwa na kupingwa vikali katika jamii zetu za kiafrika na hata katika Vitabu vyote vya  dini .

 Hadithi katika vitabu hivyo takatifu vinasema Mungu aliwashushia mvua ya moto kwa kuendekeza liwati watu wa Nabii luti (watu woavu wa sodoma na gomora)walipotaka kuwabaka malaika wa Mungu walilaaniwa na kuadhibiwa na mungu.

Katika kitabu cha mwanzo kilichopo katika biblia agano la kale na hata katika kitabu takatifu cha Quran na vilevile agano jipya vitabu vyote hivi vinaelezea watu hao waovu maarufu Kaumu Luti.

Watu hao ndio kizazi cha kwanza kuanza kuifanya dhambi hio ya liwati ,vizazi vilivyopita havikuwahi kuifanya dhambi hio,kabla ya mungu kuwangamiza watu hao aliwapelekea mtume  Luti  allaisallamu kwa mujibu wa historia ya vitabu hivyo vinavosema .

Lakini watu hao hawakumsikiliza na walimwambia Mtume Luti mlete huyo Mungu wako tutapambana nae ,watu hao walikua wananguvu na wajasiri .

Kwenye vitabu vya dini vinasema Mungu alileta malaika watatu ,Malaika Jibril , Malaika Mikail na Malaika Israfil na walikuja kwa umbile la binadamu na walikuja kwa jinsia ya kiume.

Mke wake luti nae alikuwa muovu  ndie alietoa tarifa kwa watu wa mji huo kuwa wamepata wageni wazuri ,na ndipo walipokuja vijana na wazee kuizunguka nyumba ya  Mtume Luti na kutaka kuvunja mlango ili wawalawiti wageni hao.

Mungu aliwagiza Malaika wake kuwa wasiwangamize watu hao mpaka Nabii Luti atakapo tamka mara tatu kama watu wake ni waovu sana.

Nabii Luti aliwageukia wageni wale huku akiwa hajui kuwa ni malaika na kuwambia hakika ya watu wa kizazi hiki  ni wabaya sana ,Malaika Jibril akanoti kauli ya Nabii luti kwa mara ya kwanza ,pia luti akaendelea kusema naomba mnivumilie nimetumwa kwa watu waovu sana na akasema mara ya tatu kwa kulalamika hakika watu wake ni wachafu.

Hapo sasa MALAIKA hawakuwa na mswalia mtume tena zaidi ya kutimiza agizo la mungu la kuwangamiza kizazi kile kikorofi kilicholaniwa na mungu .

Malaika wakamwambia Nabii luti usiogope na wakajitambulisha wao ni nani na wamekuja hapo kwa ajili gani , ilikua ni majira ya saa 4 za usiku na Malaika Jibril  alitakiwa na Mungu awangamize watu hao mpama ifikapo majira ya Alfajiri.

Basi ndipo Malaika Jibril aliinuka na kufata mlango na akakutana na watu wale waovu nje ya nyumba na akawawapasa kwa ubawa wake na watu hao walipofuka macho hapohapo .

Nabii Luti alitakiwa aondoke katika mji huo wa laana kabla ya mangamizi ,na kutakiwa wataponza safari basi wasigeuke nyuma kuangalia kinachoendelea.

Mungu aliungamiza mji wa watu hao kwa kuwaletea mvua ya mawe na moto ,mvua hio iliteketeza kila kilichohai katika mji huo,na ardhi yao ilipinduliwa juu chini ,chini juuu kwa mujibu maandiko yanayosema.

Mke wa Nabii Luti (a.s)alishindwa kutii amri ya kutogeuka nyuma ,alipogeuka nyuma  alipata adhabu yake nayeye aligeuzwa jiwe la chunvi ,jiwe ambalo mpa leo lipo.

Hii ni hadithi inayosimuliwa na Vitabu vya dini zote mbili waislamu na wakiristo ,hadithi inayochefua kwa vitendo vya liwati na nihadithi inayonesha utukufu wa Mungu.

Katika hadithii hii inasema dhambi la ulawiti itarudi tena katika dunia ,na sote ni  mashahidi tunajionea dhambi hii imerudi tena ikifanywa wazi wazi bila kificho.

Kwenye kitabu kitukufu cha  Qur_an Surat Israa Aya ya32 Juzuu y 15 Sura ya 17 inasema Wala msiikaribie zinaa kwa hakika ni uchafu na ni njia mbaya kabisa.

Vile vile Kitabu hicho  kitukufu Surah Al-Aʿrāf aya ya  80 Na tulimtuma Luti alipo waambia watu wake Je, mnafanya uchafu ambao hajakutangulieni yeyote kwa uchafu huo katika viumbe vyote.

Kwa Upande wa Kitabu cha Biblia takatifu  mwanzo Sūra ya 18-19 ,sura ya 18 imezungumzia Bwana na malaika wawili kuja kuzungumza na Ibrahim.

Bwana alimwambia Abraham kwamba “Kilio dhidi ya Sodoma na Gomora ni kikubwa sana na dhambi yao ni mbaya “

Mwanzo 18:20 mstari wa 22 – 33 inarekodi Abraham akimsihi Bwana awahurumie Sodoma na Gomora kwa sababu mpwa wake Luti anaishi Sodoma .

Hivyo Ushahidi wa Vitabu vyote Viwili vinaonesha kuwa Liwati haikubakili katika maisha ya Bwanadamu na pia nijambo linalomkasirisha Mungu.

Vijana kwa sasa wamesahau makatazo hayo yenye Ushahidi wa wazi wazi ,Wanalichukulia ni jambo la kawaida na kuamua kufuata matamanio na utashi wao binafsi   na kuishi  watakavo wao.

Aidha, imefikia hatua wameanzisha bendera yao inayokitambulisha chama chao (LGBT) Bendera yenye rangi 5 za Ukole.

LGBT ni kifupisho cha Kiingereza kinachojumlisha watu wanaojiona au kujitambulisha kuwa wasagaji (Lesbians), mashoga(guys), wenye kubadilisha jinsia kutoka ya kike kwenda ya kiume au ya kiume kuwa wanawake (Transgender), wanaume wanawake(queer), intersex na wasio na jinsia.

Kwa sasa jamii hiyo imekuwa ni mtandao mkubwa sana duniani na kujaribu kutapakanya utamaduni huo usiokubalika katika vitabu vitakatifu, mila na desturi za waafrika  kwa  mwamvuli wa haki za binadamu.

Katika mambo haya ya liwati kuna wanaoamua kuishi hivyo kwa matakwa yao wenyewe na kuna waliongia kwa sababu ya kuwa wahanga wa vitendo vya udhalilishaji kwa njia ya unajisi na ulawiti tokea wakiwa wadogo.

Takwimu za ukatili na udhalilishaji  wa kijinsia Zanzibar mwezi Agosti mwaka 2023 makossa ya ulawiti zinasema jumla matukio 26 yameripitiwa na waathirika wa matendo hayo wakiwa ni wavulana 23.

Kwa upande wa kosa la kuingiliwa kinyume na kimaumbile jumla ya kesi 6 zimeripotiwa waathirika wa mtendo hayo wakiwa ni wasichana 5

Kwa kuliona hili nikamua nirudi kwa Jamii nakuwauliza ni sababu gani hasa inayopelekea kuongezeka kwa matendo haya ya Liwati ndipo nilipoweza kupata majibu tofauti tofauti .

 Amina Mahmoud Ali ni mwanafunzi wa chuo kikuu cha Zanzibar Universityb (ZU)alisema Kwa mtazamo wake sababu  inayopeleka kuongezeka kwa liwati ni malezi ya mzazi mmoja .

“Ukipiga tathmini watoto wengi wanaofanyiwa udhalilishaji wazazi wao wamefariki wanalelewa na bibi au wazazi wao wametangana wanalelewa na mazazi mmoja tu’’alifafanua.

Aidha alisema Mdhalilishaji inakuwa rahisi  sana kupata mwanya wakumdhalilisha mtoto yule sababu mtoto yule anakuwa hapatiwi uwangalizi mzuri.

Aliendelea kuiomba Serikali kuchukua hatua kwa kueka sheria itaikayomdhibiti mdhalilishaji akishahukumiwa kubaki vyuo vya mafunzo.

‘’kila siku tunaona na kusikia hukumu zinatoka miaka 30,miaka 15 baada ya mwezi mmoja unamuona mtuhumiwa yule yupo nje  na anaendelea kudhalilisha wengine’’alifafanua

Pamoja na hayo Amina alieleza kuwa kuwachiwa huru watuhumiwa wa makosa hayo ndio kitu kinachopelekea kuongezeka kwa matendo hayo siku hadi siku ,tutapiga kelele kila siku lakini tutaona matendo yanazidi kukua.

Kwa upande wake Mwalimu wa Skuli ya Uwandani Chake chake Pemba Zainab Abdalla Aley alimfahamisha mwandishi wa makala haya sababu inayopelekea kuongezeka kwa matendo hayo ya ulawiti ni tukokuridhika nafsi kwa vijana wetu na kupenda kujaribu vitu.

Alifahamisha kuwa vijana wengi wanatamaa sana ya vitu vya gharama huku wakiwa hawana pesa ya kununulia viti hivyo,ndipo wanapapata watu wakawalaghai na kufanywa matendo hayo.

‘’Ni jambo la kushangaza kwa sasa utawaona watoto wa kiume wanaazimana nguo  jambo ambalo ni ishara ya tama kuwa haridhiki na nguo alizonunuliwa na wazazi wake. Ingawa tabia hiyo inafanya zaidi na watoto wa kike  ’’alifafanua.

Aidha alisema kuwa utandawazi pia unachangia kuongezeka kwa matendo hayo ,simu hizi zinatumika vibaya kwa kuangalia picha za ngono na kuipelekea na wao kujaribu vitendo vile.

Abdalla Hamad ni mwalim wa Madrasa alisema kuwa inatokana watu kuacha kufuata maamrisho ya Allah sw na kufuata mambo ya kidunia pekee ,

Alisema jambo jengine linalopelekea kuongezeka kwa liwati ni wasimamizi wa familia kuacha kuwa wafuatiliaji wazuri wa mienendo na mafunzo sahihi watoto juu ya jambo hili au mfano wa hili.

Ustadh pia alisema sababu nyengine ni wazazi  kuwapa watoto  uhuru mkubwa  wa kwenda watakapo  na kulala wakatapo kwa kisingizio cha twishan.

‘’kwa sasa wazazi wanatakiwa wawe macho wahakikishe wanajua na kufuatilia  watoto wao wanalala kambi wapi na nani anaelala nao, je! hali za usalama za watoto hao zikoje huko ‘’alisisitiza.

Kwa upande wake Mzazi na mlezi Zamzam Mohd alisema kwa kweli jambo hili sasa limekuwa tishio na linamkosesha amani kila Mzazi hapa nchini.

Wafanyaji wa matendo haya sasa wamekuwa wakijitangaza waziwazi kupitia mitandao ya kijamii,huku wakiwahamasisha wengine raha wanazozipata kupitia Liwati.

Katika Kumbukumbu zangu kuna kisa kimoja kilitokea katika mtaa wetu,nilikua mdogo kipindi hicho na sikuwa na uelewa wa madhara ya liwati.

Mtoto wa jirani yetu alikuwa anafanyiwa matendo hayo kila siku anapokua anakwenda chuoni ,kuna kijana alikua anamchukua kwa nguvu na kumlawiti.

Kutokana na hofu aliyokua hayo alishindwa kumueleza mamake ,mamake alikuwa mkali sana ,hadi siku moja alipojinyea na mamake akaingia wasiwasi na kumchunguza  na kugundua alikua anafanywa hivyo.

Cha kusikitisha Mamake alimpiga sana na kumfungia ndani hakuchukua hatua yoyote nyengine ili kuweza kukomesha yule mfanyaji asiendelee.

Makusudio yangu ya kukielezea kisa hiki ,wazazi tunatakiwa tuwe karibu na watoto ,kusiwe wakali mpaka watoto  wakashindwa kutuambia wanayokutana nayo.

Kaimu Kamanda wa Polisi  Mkoa wa Kusini Pemba Kamishna msaidizi wa polisi Cyprian Aloyc Mushi alisema kunakesi nyingi za udhalilishaji ambazo zimefanyika madrasa,maskulini na majumbani .

Alisema kwa sasa mwamko wa kuripoti makosa ya udhalilishaji  umeongezeka ,pia jamii inatakiwa kuamka hususan katika liwati,kwani athari yake kubwa zaidi.

“Wazazi wakae na watoto wao pia kufatilia matendo yao ,ujue yupo chuoni anafanya nini,kila hatua ambayo mtoto wako yupo uijuwe  ”alifafanua.

Alishauri wazazi kuwapa maadili watoto wao ili kuweza kijiepusha na masuala ya liwati,kwani maadili yetu hayaruhusu masula hayo kimila na kidini.

 Mkaguzi msaidizi wa Polisi  A/INSP Habiba Ali Saidi kutoka Dawati la kijinsia la Mkoa wa Kusini alisema changamoto kubwa aliona Kuwa sheria inasema mtoto ni miaka chini ya miaka 18 ,lakini unapopata kesi ya mtoto wa umri huo unapofanya nae mazungumzo unamuona kabisa bado mtoto .

“Mtoto wa miaka 18 kiuhalisia kabisa unamuona bado anakili za kitoto lakini kutokana na maumbile yake aliyonayo anajiona mtu mzima “Alisema

Akitoa wito wake nae pia ameshauri wazazi kuwa walinzi na watoto wao ,masula ya liwati yanathari kubwa sana ,tusipokua makini tutakosa taifa lililo na nguvu kazi ya vijana Shababi.

Kwa mujibu wa takwimu kutoka Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali matukio ya ujdhalilishaji wa kijinsia yameongezeka, ambapo mwaka 2022  jumla ya matukio 1360 ya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia  yaliripotiwa.

Jumla ya   watoto  1173 sawa na  Asilimia 86.2 walidhalilishwa  watoto wa kike 889 na watoto wa kiume 284  ulimnganisha na watoto waliofanyiwa udhalilishaji waka 2021 wakike 846 na wakiume 222 mwaka 2021.

Kwa Mwezi July 2023 takwimu zinasema Jumla ya matukio 168 ya ukatili wa kijinsia yameripotiwa ambapo waathirika walikua 168, Wilaya ya Magharib A imeripotiwa kuwa na matukio mengi kulinganisha na Wilaya Nyengine.

Idadi ya matukio kwa mwezi imeongezeka kwa asilimia 32.3 kutoka matukio 127 kwa mwezi June 2023 hadi 168 mwezi wa Julai 2023.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Hussein Ali Mwinyi alizindua kamati maalum ya kupambana na makosa ya udhalilishaji .

Mh Rais mnamo tarehe 1 Juni Alizindua kamati hio katika ukumbi wa  Sheikh Idrisa Abdul Wakil na kusema Serikali yake inaunga mkono jitihada za kuanzishwa kamati hio.

Aidha Mh Rais alisema ameziagiza tasisi zote zenye wajumbe wanaounda kamati hio kutoa ushirikiano  na kufanya kazi kwa ukaribu na afisi ya mkurugenzi wa Mashtaka ili kufanikisha Malengo yaliyokusudiwa.

Yote kwa yote Jamii inatakiwa iamke na iwe macho,kila mmoja awe mlinzi wa mtoto wa mwenziwe ,inapotokea kesi za udhalilishaji muathirika asinyanyaswe au kutengwa.