Sunday, November 24

SMZ imeamua kujenga Skuli  za ghorofa ili kuondoa changamoto ya uhaba wa Madarasa-Mh Hemed

Kukamilika kwa Mradi wa ujenzi wa Skuli za ghorofa zinazoendelea kujengwa Unguja na Pemba kutatatua changamoto ya uhaba wa Madarasa

Kukamilika kwa Mradi wa ujenzi wa Skuli za ghorofa zinazoendelea kujengwa Unguja na Pemba kutatatua changamoto ya uhaba wa Madarasa na wingi wa Wanafunzi katika Skuli mbali mbali.

Akikagua Miradi hiyo katika Mkoa wa Kusini na Mkoa wa Kaskazini Pemba Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdulla amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeamua kujenga Skuli hizo za ghorofa ili kuhakikisha changamoto ya uhaba wa Madarasa inamalizika pamoja na kuborosha mazingira ya kujifunzia na kufundishia.

Amewataka wakandarasi na washauri elekezi wa miradi hiyo kuongeza kasi katika ujenzi ili kuhakikisha wanamaliza kwa wakati uliopangwa na kwa ubora wa hali ya juu na Skuli hizo zifunguliwe mwanzoni mwa Mwezi Januari mwaka 2024 ili wanafunzi waweze kusomea .

Mhe. Hemed amewaeleza wakandarasi wa Skuli hizi kuwa Serikali ya mapinduzi ya Zanzibar imetenga fedha zote za miradi hiyo na kusema kuwa chamgamoto yoyote itakayojitokeza Serikali itaitatua kwa haraka sana.

Amewataka Wakandarasi na Mshauri elekezi wa miradi hiyo kuhakikksha Wananchi wa maeneo yanayojengwa Skuli hizo wanapewa kipao mbele katika suala la ajira ambazo wanaweza kuzifanya ili nao waweze kufaidika na kupunguza ukali wa maisha.

Amewaomba Wananchi wanaoishi katika maeneo yanayojengwa Miradi hiyo ya Skuli za ghorofa kutoa ushirikiano mkubwa katika kufanikisha kukamilika kwa miradi hiyo ambayo itawanufaisha vizazi vilivyopo na vijavyo huku akisisitiza kuwa changamoto ya barabara za ndani zitafanyiwa kazi kwa kujengwa barabara zenye kiwango cha lami.

Sambamba na hayo Mhe. Hemed ameeleza kuwa kukamilika kwa Skuli hizo Serikali itaweka vifaa vya kisasa na kuwawezesha walimu kwa kuwapatia ujuzi ili wanafunzi waweze kukuza ufaulu wao.

Nae Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar Mhe. Lela Mohamed Mussa amesema hatua iliyofikia katika miradi hiyo ni ya kuridhisha inayotokana na maamuzi ya Wizara kukabidhi wakandarasi wazawa ambao watakuwa na uzalendo kwa nchi yao.

Imetolewa na Kitengo cha Habari (OMPR)