Sunday, January 5

MAKALA: MTAALA WA ELIMU NA MCHANGO WA VIONGOZI WA KIKE WA BAADAE.

NA AMINA AHMED MOH’D, PEMBA. 
WAHENGA  wa jamii ya Waswahili wametoa elimu, mafunzo na kutanabahisha jamii juu ya masuala mbali mbali kwa kutumia vitendawili, mafumbo na methali.
Haya yamo pia katika malezi au kujitayarisha kwa kitu au jambo ambalo matokeo yake huwa na uhusiano mkubwa na kinachotokea hapo baadae .
Miongoni mwa maneno ya hekima yaliokuwa yamesukwa kwa njia ya mafumbo  ni ule msemo wa “Samaki Mkunje angali mbichi’’.
Methali nyengine yenye lengo la kuelimisha juu ya suala hilo hilo ni ileisemayo ‘Udongo upate ulimaji’’.
Misemo hii inakusudia kuitahadharisha jamii juu ya umuhimu wa maadalizi ya mapema katika kumuandaa mtoto na hata mtu mzima kwa jambo liliopo mbele ili aweze kuhimili changamoto na mikiki yake na asije kujikuta amezongwa na vitendawili ambavyo utatuzi wake haujui uanzie wapi na kumalizikia wapi.
Kwa muda mrefu  sasa mtaala wa masomo  Zanzibar,  kuanzia  masomo ya skuli za msingi  hadi sekondari umekuwa na msururu wa changamoto ambazo zinaelezwa kuwa chanzo cha kutoshajiisha   uwezo  wa watoto wakike na wakiume kwa maisha ya baadae.
Hii ikiwa pamoja  na kuwaandaa kushiriki  katika kupanga na kutoa maamuzi juu ya mambo mbali mbali yaliomo katika jamii.
Kwa maana nyengine mambo ya kushika hatamu ya uongozi yalikuwa yanaonekana kama vile hayawahusu na wao siku zote kuwa wanaongozwa, hata na watu wasiokuwa na haki  sifa pamoja na uwezo wa kuifanya kazi hio.
Serikali, kwa kushirikiana na wadau wa elimu, baada ya kubaini kuwepo hali hii ambayo inadumaza maendeleo ya nchi iliamua  kukaa kutafuta  dawa mujarab (muarubaini) wa kupata ufumbuzi wa  tatizo hili.
Miongoni mwa njia zilionekana ndio sahihi kupita ni  kubadilisha baadhi ya mitaala iliyoonekana  inamdumaza mwanafunzi ili kupata mtaala mpya wa kufundishia wanafunzi kwa baadhi ya madarasa .
 Mtaala  huo uliolenga kubadilisha  maisha ya wanafunzi wa kike na kiume  kutoka kusoma kwa nadharia  kama ilivyokuwa  katika mtaala wa awali wa maandalizi,  kuja katika ushirikishwaji wa masomo  kwa vitendo kwa kutumia mtaala mpya ulioanza kutumiwa mwaka huu.
Hapa najaribu kuangazia huu mtaala mpya wa elimu ya maandalizi katika  darasa la awali  ulioanza kutumika  Januari 1 mwaka 2023  kwa lengo la kumuandaa mapema mtoto wa kike kuweza kukabiliana na changamoto atakazokumbana nazo baadae katika jamii ikiwemo   uongozi.
Fursa na  uhuru ulipo   katika mtaala huu unahitaji kutiliwa mkazo katika kumuendeleza  vyema mtoto ili kuepuka kuwa  tegemezi hapo baadae .
 Watoto wa kike wengi wamekuwa wakikosa uthubutu wa kutaka uongozi kutokana  na kutopatiwa mapema maandalizi ya kufikia huko licha ya wao kuonekana kwa idadi kubwa madarasani ukilinganisha na wanaume.
Hadi kufikia mwaka 2022  Zanzibar ilikuwa na skuli za maandalizi  508 ukilinganisha na  498  zilizokuwepo  2021  za serikali na binafsi ambapo jumla ya wanafunzi   74, 950  waliojiunga na skuli hizo  mwaka 2022.
 Katika mwaka 2021 walikuwemo wanafunzi 91,074 Unguja na Pemba.
Mitaala mingi ya    kufundishia wanafunzi  ilijenga  nadharia ya kumuonesha mtoto wa kike kuwa ni mtu ambae anaandaliwa kuwa mtu wa mwisho katika kutoa maamuzi na sio kushiriki kwa usawa ambapo hali imebadilika kupitia mtaala huu mpya.
 Mtaala huo wa elimu ya maandalizi darasa la awali  unaotambulika kwa jina la MUHTASARI WA ELIMU YA MAANDALIZI  unatoa muongozo  wa kumsaidia mwanafunzi kujiandaa mapema na kumtoa katika fikra hizo.
Katika  mtaala huo  mwanafunzi anatarajiwa kujifunza kwa vitendo mambo mbali mbali, kama kusema   kusikiliza na kuzungumza, kusoma na kuandika sambamba na   kufanya vitendo.
 WAALIMU WANASEMAJE 
 Baadhi ya waalimu wa madarasa ya maandalizi  wamesema laiti mtaala huu  ungelitumika kabla mabadiliko makubwa  ya maendeleo katika nyanja na sekta mbali mbali  yangepatikana
 “Hivi sasa mtoto anafundishwa sio aweze kuhifadhi peke yake, bali anachofundishwa  aweze kukitumia na kumsaidia katika maisha. Kwa mfano atafundishwa  kufanya kazi za vitendo  ambavyo akitoka darasani anajaribu akiwa katika jamii”  Salma Moh’d khatib
 ” Tungelikuwa tuko mbali  kwa sababu nchi za  wenzetu waliotumia mtaala kama huu ambao kwetu Zanzibar ni mpya  wapo mbali”.
Alisema huu ni mtaala unaowataka  waalimu kuwapa nafasi wanafunzi kuweza kujitayarisha mapema na kuweza  kujitambua , aliendelea    Salma Mohd khatib ambae ni mwalimu wa skuli ya maandalizi Madungu Chake Chake Kusini Pemba.
MTAZAMO WA TAASISI YA ELIMU ZANZIBAR. 
Soud Abdalla Tumu, Afisa Mkuza mitaala  kutoka taasisi ya elimu Pemba alisema lengo la serikali na wadau katika kuboresha mitaala ya kufundishia ni kuleta mageuzi ya elimu yatayowasaidia wanafunzi kukabiliana na mazingira katika Jamii.
“Lengo la kutumika  mtaala mpya  unaoendana na jamii ni kuona mtoto anayakabili mazingira katika na kuweza kukifanyia kazi kile kinachofundishwa na sio abaki na kuhifadhi alichofundishwa ubaoni hili halikuwepo katika mtaala wa awali ” , alieleza.
” Mtoto anafundishwa  kuanzia darasa la awali kujua yeye ni nani na anatakiwa afanye nini, ijapokuwa atahitaji usaidizi,lakini ile akili yake inaandaliwa kuendana na mazingira ya kujitambua na kujiamini juu ya kila kitu”, aliongeza.
Alisema hapo awali  mtaala uliwahifadhisha tu watoto kwa mwalimu kuandika ubaoni, au kuwapa   maelekezo kwa njia ya maandishi anazungumza yeye na watoto  kuhifadhi kilichoandikwa. hali ambayo ilikuwa  haiwachangamshi  wala kuwaandaa watoto.
Hivi sasa muongozo unawataka waalimu wamsikilize mwanafunzi  kwa vitendo na  kuwaongoza  wafanaye kazi gani .
Muhamed Nassor Salum, Afisa Mdhamini wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Pemba amewataka waalimu wakuu kusimamia mitaala  mipya iliyorekebishwa kuanzia madarasa ya awali na msingi ili kusaidia   kuzidisha maarifa  yatakayowasaidia  kujikomboa na changamoto ziliopo katika jamii wanapomaliza masomo yao .
WAONAVYO WAZAZI.
Ishaka Muhamed Khamis alisema anaona bado  watoto wengi Pemba  hawana  uthubutu na ni nadra  kumuona mtoto mdogo anatumia vifaa vya  kujifundishia  kwa vitendo   au kusimama mbele za watu kueleza yeye ni nani kutokana na kukosa maandalizi ya kuwa na uthubutu wa kuzungumza mapema “.
  ” Wanajitambua ila mara chache  utamuona mtoto anajieleza yeye ni nani, anaishi wapi, mama yake anaitwa nani,   anataka kufanya kazi kwa vitendo yapo mabadiliko na zaidi katika skuli za binafsi, alisema Mariam Kombo Hamad.
Aliona kuwepo tofauti kidogo kwa vitendo  kati ya mwanawe mdogo na mwenzake aliyepita  skuli ya maandalizi.
Tafauti aliyoina ni pamoja na kufahamu mambo vyema kuliko mwenzake.
WADAU WANAVYOUONA MTAALA MPYA. 
Halima Juma khamis alisema kuboreshwa  mitaala  ya kufundishia kutasaidia kuodokana na fikra mgando kwa wanafunzi ambao kwa asilimia kubwa wanalazimika kusoma kwa kuhifadhi maandishi, lakini kubwa zaidi ni kutokana na kutotambua kinachowasubiri baadae.
“Mfumo ulikuwa unawalea vibaya watoto mtoto mpka anatoka maandalizi  hajui yeye ni nani kivitendo  kwa mabadiliko haya katika mitaala huenda tukapata mabadiliko  yanayostahiki”.
Sifuni Ali Juma  kutoka mwamvuli wa asasi za kiraia,  Pemba Pacso, amesema  mabadiliko ya mitaala yaliofanywa kwa baadhi ya madarasa yanahitaji usimamizi mkubwa ili kuleta mabadiliko yatayozalisha tija  kwa wanafunzi.
 “Tija inayohitajika ni mabadiliko ya kimaendeleo’’,aliongeza
Alisema ni matumaini yake endapo mtaala mpya utatumika ipasavyo hakuna ambacho kitarudisha nyuma kumuandaa mapema mwanamke katika kujikomboa juu ya nyanja tofauti za kijamii na siasa na kuweza kushika hatamu za uongozi.
CHANGAMOTO ZA  WAALIMU  
 Miongoni mwa chngamto walionazo walimu katika utekelezaji wa huu mtaala mpya ni vitendea kazi ambavyo vitakidhi mahitaji ya wanafunzi wanafunzi ni wengi vifaa ni kidogo.
Jengine  ni kutumia nguvu nyingi kulinganisha na ilivyokuwa kwa mtaala wa awali. Alisema Bimkubwa Khatibu Said Mwalimu Darasa la maandalizi.
Alisema ili kuendana na kasi ya maendeleo katika elimu kupitia mitaala liyorekebishwa  wazazi wanapaswa kuwasaidia kuwakuza watoto kuyakabili mazingira yaliopo katika jamii.
“Wazazi wengi bado wanahisi jukumu la kusimamia maendeleo ya elimu kwa mtoto ni ya waalimu peke yao jambo. Hali hii inarudisha nyuma jitihada zetu na mfano ni pale tunapotoa kazi za majumbani utaona  wanafunzi hawasimamiwi au kusaidiwa na wazazi wao kuzifanya kazi hizo’’, alisema Shadida  Tahir Nyange.
Aliitaka serikali kuhakikisha utekelezaji wa mitala mipya unaendana na kuwepo vifaa vya kusomesha maskulini.
 Licha ya kuwepo changamoto, mtaala huu wa muhtasari umeonesha dhamira ya kusaidia kumuandaa mtoto wa kike kwa maisha ya baadae , ikiwa pamoja nakushiriki katika shughuli za uongozi.
Kama serikali itasimamia vizuri mtaala huu na kuboresha mitaala ya elimu katika ngazi nyengine za elimu Zanzibar inaweza kupata  viongozi na wasimamizi wazuri wa taifa, ni  muhimu ni kutambua kuwa samaki mchanga hukunjwa angali  mbichi.