Sunday, November 24

MAKALA: Sheha aliyebadili tabia za vijana na watoto katika shehia yake.

NA, AMINA AHMED MOHD, PEMBA 
ULEZI sio kazi ya wazazi peke yao, bali ni ya wazee wote na hasa wanaoshika nafasi moja au nyengine ya uongozi katika jamii.
Kupewa dhamana ya uongozi ni jambo moja na kuonyesha njia nzuri ya kuongoza na kusaidia jamii ni jambo nyengine.
Wapo watu wanaofanya kila juhudi kupata nafasi ya uongozi, lakini wakishachaguliwa huzipa kisogo ahadi walizotoa walipogombea uongozi na kutojali maisha na masalahi ya wana jamii.
Miongoni mwa mifano ya uongozi ulio bora na unaofaa kupigiwa mfano ni wa sheha wa shehia ya  Madungu, Chake Chake Pemba, Mafunda Hamad Rubea.
Mwana mama huyu sio tu ametimiza wajibu wake kama kingozi, bali amethibitisha ukweli wa usemi maarufu wa ‘ Uchungu wa mwana aujuwae  mzazi kutokana na jitihada alizochukua katika kupambana na vitendo viovu  ikiwemo mmonyoko wa maadili kwa vijana na watoto.
Shehia ya Madungu ambayo katika sensa ya mwezi Agosti, mwaka  2022 ilionekana kuwa na  wakaazi  5869  (wanaume   2,788 na wanawake 3,081)   kaya  1,0 78  huku ikiwa ni miongoni mwa shehia yenye idadi kubwa ya watu katika Jimbo la Chake chake.
Licha ya idadi hiyo  kuwepo kwa kingozi imara na mwenye kujituma katika shehia hiyo   basi maendeleo hupatikana na mambo ambayo yalikuwa yakihatarisha maisha ya vijana na watoto na kuwa kero kwa jamii yamepungua
Akizungumzia hali iliyokuwepo kabla ya kuchaguliwa sheha, Mafunda alisema Wanafunzi walikuwa wanavutishana  sigara nyakati za Skuli kwa kukaa kwa  vikundi  kwenye vivuli vya miti na hawaingii madarasani na wengine walikuwa hawaendi kabisa na kuzura mitaani  na kukaa katika maskani za vijana ambao hawasomi
 “Uchungu wa mwana anaujuwa mzazi na ni mama nimeuonja uchungu huo na sipo tayari kuona wimbi  la  vijana linapotea  hivi hivi’’ amesema.
Hali aliyoikuta ilimlazimisha  kuwafuatilia karibu mwendo wa vijana na watoto katika shehia yake kwa kushirikiana na wasaidizi wake.
Miongoni mwa njia walizotumia ni kuzungumza nao kama marafiki na kuwashauri hasara ya mwenendo wao mbaya na faida za kuachana nao na kujihusisha na masomo au kazi zenye manufaa kwao na familia zao.
“Tabia nyengine hatarishi ni kwa watoto wadogo wa kiume, zaidi katika mitaa ya Mtoni na Fueni ambapo  watoto wengi walipiga kambi mchana na usiku na hapo  hapasomwi wala hapaandikwi “, alieleza kwa masikitiko makubwa.
“Watoto wengine waliiba pesa majumbani ili kwenda kushiriki michezo ya video na masikini walihadaiwa kufanyiwa mambo mabaya ili mradi wapate pesa za kucheza kwenye vibanda vya hio michezo. Walikuwa wanatoka makwao mapema asubuhi na kubakia huko hadi saa tano za usiku.

 MIKAKATI  ILIYOTUMIKA
Kwanza alifanya mikutano kuzungumza na viongozi katika shehia, maimamu, wazee, askari polisi  na  wazazi ili kushauriana njia zipi zitumike kurekebisha mwenendo wa hao vijana waliokuwa wanashiriki katika mambo ambayo yanawaharibia maisha.
‘’Kwa pamoja tuliafikiana kuvifunga kwa muda  vibanda vya michezo ya video  huku masharti maalum yakiandaliwa  dhidi ya uendeshwaji wa biashara hiyo ya video  pamoja  na kufanya doria nyakati za usiku na kumuwajibisha mzee ambaye mwananawe ataonekana anazurura mtaani nyakati za usiku mkubwa’’, alieleza.
Vile vile pia aliunda kamati ya  maalum ya kusimamia mwenendo wa vijana na watoto katika shehia.
WANANCHI WAPONGEZA
Abrahman Abubakar Mohamed na  Jamila Muhammed waliupongeza uongozi wa sheha wao katika kushughulikia mwenendo mbaya wa vijana na watoto na mchango anaoendelea kuutoa kwa kushirikiana na  viongozi wa misikiti, madrasa pamoja na viongozi wengine wa dini.
Katika mapambano haya palifanyika zoezi maalum za kuwatafuta wanafunzi, hasa wa Skuli ya Madungu, ambao waliweka mbele michezo ya video badala ya masomo kwa fedha za matumizi walizopewa na wazazi walipokwenda skuli walizitumia kwa michezo ya video.
Vile vile walimu wa vyuoni (madrasa) waliwahimiza wanafunzi wasishiriki michezo ya video kwa vile haina faida kwao.
Mtoto mmoja , Amran Sharif Amran, alisema siku hizi haendi katika vibanda vya michezo ya video kwa vile wamekatazwa kufanya hivyo na walimu wao chuoni.
“Mama kasema nisome kwa bidi, nisiende katika michezo ya video kwa sababu nitakuwa sifahamu masomo .
 Siku hizi siendi kwa sababu tumeambiwa skuli  atakaekwenda atapelekwa Polisi’’  alisema Ahmad Khamis Hamad, mwanafunzi wa skuli iitwayo Bright Academy ya Madungu.
 MCHANGO WA POLISI. 
Kwa kushirikiana na viongozi wa shehia tumefanikiwa kuanzisha  kamati maalum   , ulinzi shirikishi ambazo tunazisimamia sisi jeshi la Polisi na hii  imekwenda sambamba na  kuanzisha mashindano ya michezo mbali mbali, ikiwemo ligi maalumu za  mpira wa miguu ambayo  inashirikisha vijana kutoka shehia zote za Kusini Pemba.
Hii imesaidia vijana kuwa hawana muda wa kujiunga na vikundi viovu na hii imesaidia vijana wengi kubadilika kwa kuupa mgongo mwenendo usiokuwa na manufaa kwa maisha yao, kama kuvuta sigara na kujiunga na vikundi vya vijana wenye mwendo  mizuri na kujiweka katika maskani kujadili mambo ya hovyo.
Vijana  wapatao 100, Madungu walikuwa wanaishi katika mazingira hatarishi,  ndani ya  shehia ya Madungu  walijiunga na michuano ya kombe la RPC Kusini.
Katika mashindano haya shehia ya Madungu ni moja kati ya shehia ambayo  iliingiza timu nyingi kuliko sheha nyengine zote, alisema kaimu kamanda  wa Polisi  kusini Pemba Siprian Alaice Mushi.
Mashirikiano ya  viongozi  imesaidia kuwaepusha  vijana wengi na vitendo viovu, kama wizi uporaji, na uvutaji bangi pamoja na kuendelea kudumisha amani ni wachache sana  kwa sasa wenye tabia zisizoridhisha na Tunaendelea na mashirikiano   kumaliza kabisa changamoto hizo kwa vijana.
  MADUNGU KWA SASA YADAIWA KUWA NA MABADILIKO HAYA . 
Baadhi ya vijana  hao wamesema kwaheri maisha hatarishi ya maskani ambapo  shughuli mbali ikiwemo michezo yenye tija, kuendesha boda boda  kutoka maskani ambazo katika shehia hiyo zilikuwa zikitajika kwa viashiria vya kuporomoka kwa maadili ikiwemo maskani iliyobeba jina maarufu la  shamash, pamoja na maskani ya  mazombi zinaendelea .
Walimu katika skuli hizo  akiwemo Nunuu Muhamed Hassan na Arkam Zahor  Ali   walieleza kwamba hapo awali tatizo la wanafunzi  kukosa usimamizi  ndani ya jamii lilikuwa changamoto jambo ambalo lilipelekea kutoonekana madarasani kwa muda mrefu na wengine kutohudhuria bila taarifa kutoka kwa wazazi, lakini sasa limepungua.
Walimu hawa walieleza kwamba wanafunzi zaidi ya 40 walikuwa hawaonekeni  katika skuli  wiki mbili wiki tatu wengine siku mbili tatu na utoro wa kukata kata ndani ya wiki  bila taarifa kutoka kwa wazazi wao, lakini sasa hali imebadilika.
’’    Sababu kubwa ilikiwa ni michezo tu mitaani bila uangalizi wala kufuata maadili vishawishi pia alisema Arkam, mwalim wa nidhamu na maadili  wa Skuli ya The Bright Academy.
Mwalimu Nunuu alisema uongozi  wa shehia umetoa mchango mkubwa Kusaidia kurejesha maadili, kama awali baadhi ya  vijana walikuwa wanavaa  suruali  nusu uchi, nywele kubwa  kichwani ila  tunashukuru kuona hali imebadilika.
Halima Juma Diwani ambaye ni mratibu wa shehia hiyo alisema  vitendo vya udhalilishaji  kwa watoto   vinavyojitokeza mara nyingi katika shehia hiyo vinatokana na wazazi kukosa uangalizi  na ufuatiliaji ambapo hatua mbali mbali zinaendelea kuchukuliwa kwa kushirikiana na uongozi wa shehia.
  WAMILIKI WA BIASHARA KUENDESHA MCHEZO WA VIDEO WANASEMAJE.
  Wananchi  ndio wanaona  hii michezo haifai, lakini michezo hii ipo kwa wenzetu ipo na wahusika ni watoto zaidi na ni biashara halali kabisa .
 “Tunaendelea kufuatilia vibali vyetu kuendesha biashara hii ambayo inatuingizia kipato kuendesha shughuli zetu” Alisema Nasibu  Muhamed (Chibu) moja kati ya wamiliki wa video game Madungu .
Suala la  kujiuliza ni namna gani vibanda  hivo vya michezo vitaendeshwa na jee havitakuwa kimbilio la watoto, badala ya kwenda kusoma  au kutakuw ana mpango maalum wakuhakikisha hali iliokuwepo kabla haijirudii?.
Juu ya hilo sheha  Mafunda aliwataka wazazi na walezi kuzidisha mashirikano ya malezi ya watoto na vijana, hususan wakiume  kuwafuatilia kwa karibu mienendo na tabia zao.
Alisitiza kwamba mpango wa kuondosha michezo ya video, kutoa elimu na kudumisha michezo yenye tiba  ndani ya shehia hiyo itaendelea.
Aidha alitaka Serikali   kuliangalia suala la vibali vya kuendeshea biashara  ya video na kama ni kuendelea basi pawekwe masharti yatayozuia uharibifu wa vijana ili kuwanusuru wanafunzi  na watoto kupoteza haki yao yakupata elimu na ulinzi dhidi ya vitendo vya udhalilishaji.
Sheha wa Madungu ameonesha mfano wa uongozi bora ambao unafaa kuigwa na wenzake wa shehia nyengine za Unguja na Pemba. Penya uongozi mzuri, hasa wa mwanamke mambo huwa mazuri.
Nimalizie makala hii kwa ule msemo maarufu unaolenga mashirikiano katika kufanya jambo usemao kuwa
“KIDOLE KIMOJA HAKIVUNJI CHAWA” endapo  wanajamii wa Madungu Serikali pamoja na wadau wa maendeleo ya vijana na watoto wataendelea kuunga mkono jitihada hizo zilizooneshwa na kiongozi huyo mafanikio ya kudhibiti maadili yataongezeka na kupata taifa  bora zaidi sasa na baadae.
Mwisho.