Saturday, December 28

Skuli ya Nyerere sekondari yatoa Msanii bora Tamthilia.

NA ABDI SULEIMAN,PEMBA.

MSANII bora katika sanaa ya Tamthilia Haitham Hafidh kutoka skuli ya Nyerere Sekondari, amesema siri ya mafanikio iliopelekea mpaka akibuka mshindi wa kwanza ni kujiamini wakati alipokua akiigiza.

Haitham alibeba uhalisia wa mtu mwenye ugonjwa wa akili (chizi), wakati wa mashindano ya tamthilia kwa skuli za sekondari, kwenye shamrashamra za kuelekea tamasha la 59 la elimu bila malipo linaloendelea katika viwanja vya skuli ya Fidel Castro, hali iliyowafanya watazamaji kubakia vyinywa wazi.

Akizungumza na mwandishi wa habari hizi, mara baada ya kutangazwa kuwa mshindi kwa upande wa ektazi, alisema kujiamini na kubeba uhalisia wa sehemu unayopangiwa ndio moja ya mafanikio yaliofanya kuibuka mshindi.

“Tokea siku tulipoambiwa kila mtu achague sehemu yake anayotaka kuigiza, mimi nilichagua kipande hiki cha uchizi, nilikua nakifanyia mazoezi mara kwa mara, na mwisho wa siku nimeibuka mshindi,”alisema.

Alisema unapotaka kuigiza lazima ukubali kubeba uhalisia wa kitu moja kwa moja na sio kuona haya, jambo ambalo linaweza kumto mtu katika mchezo.

Hata hivyo aliwataka wanafunzi wenzake wanapoingiza katika sanaa, kujiamini, kutoa hofu kwani hakuna mtu anaefundishwa na kushindwa katika eneo la muigizaji.

Kwa upande wake mkufunzi wa sanaa kutoka skuli ya Nyerere Ruwaida Ramadhani, alisema mafanikio ya mwanafunzi huyo ni kutokana na juhudi na jitihada alizokua akizifanya kila muda wa mazoezi unapofika, kutokana na kipengele cha sehemu yake kuwa kigumu.

“Unajua kupata mtu kuekti kama chizi anaekaa majaani kinataka umahiri wa hali ya juu, lazima ujiamini na uwe mbunifu na Haitham ametimiza vigezo,”alisema.

Nae Mwalimu msimamizi wa sanaa upande wa waamuzi Salim Kassim Hamad, alisema kwenye suala la tamthilia hakuna suala la mada kwani mada ziko kwenye mdahalo, ispokua tamthilia zinatakiwa kwenda kwa kutumia karent ishu tu.

Kwa upande wa Matokeo ya Tamthilia skuli za Sekondari, skuli ya Chasasa imeibuka mshindi wa kwanza ikiwa na alama 346, nafasi ya pili ikaziangukia skuli za Nyerere na fujoni zilizofungamana kwa alama 345, skuli ya maendeleo ikikamata nafasi ya nne kwa alama 325.

Kwa upande wa skuli za msingi, skuli ya msingi Kajificheni imepata alama 356 na kushika nafasi ya kwanza, nafasi ya pili ikaangukia kwa skuli ya Simai msingi iliopata alama 334, nafasi ya tatu ikaenda kwa skuli ya Kusini msingi baada ya kupata alama 332, nafasi ya nne ikachukuliwa na skuli ya Chanjamjawiri iliopata alama 296.

MWISHO