NA ABDI SULEIMAN, PEMBA.
AFISA Mdhamini Wizara ya Nchi Ofisi ya Rais Katiba, Sheria Utumishi na Utawala Bora Pemba Halima Khamis Ali, amesema wasaidizi wa sheria bado wanakazi kubwa sana ya kuisaidia jamii, licha ya mafanikio kadhaa walioyapata.
Alisema bado katika jamii kuna watu hawafahamu chochote mpaka leo, juu ya masuala ya kisheria changamoto hiyo ni kubwa hali inayopelekea kukumbwa na mikasa mbali mbali.
Aidha aliyataja baadhi ya matukio yanayotokea ni Udhalilishaji, madawa ya kulevya, dhuluma na ukatili wa kijinsia, watoa msaada wakisheria ndio wakuisaidia jamii kwa kila mmoja kwa nafasi yake kuhakikisha haki inapatikana na kuonekana.
Mdhamini Halima aliyaeleza hayo wakati akifungua mkutano wa siku moja, wa Nusu Mwaka wa wahusika wa msaada wa Kisheria, ulioandaliwa na Idara ya katiba na msaada wa kisheria Zanzibar kwa ufadhili wa shirika la UNDP na kufanyika mjini Chake Chake.
Alisema bado wanakazi kubwa sana licha ya mafanikio makubwa walioyapata, vikao kama hivyo ndio vinavyoibua hisia mikakati pamoja na mambo yote yaliokusudiwa kufanywa ili kufikia malengo.
“Kila aliyepo hapa ni wahusika ambao wanahusika moja kwa moja katika utoaji wa msaada wa kisheria, anacho cha kuendeleza katika upatikanaji wa haki katika jamii,”alisema.
Aidha alisema kuna mambo mengi yamesaidia kutokana na juhudi za watoa msaada wa kisheria, kwa kushirikiana na idara ya katiba na msaada wa kisheria, kuhakikisha wanasimamia adhama ya serikali ya upatikanaji wa haki, kuondosha ujinga katika jamii pamoja na dhuluma.
Alisema ni jukumu la watoa msaada wa kisheria pamoja na wahusika wote, ambao wanashirikiana katika tasnia hiyo kuhakikisha wanazifikia jamii mguu kwa mguu licha ya changamoto zilizopo.
Alisema idara inafanya kazi kubwa sana kwa sababu wanahisi wanadeni katika taifa hili, changamoto zinazojitokeza zinapaswa kuchukuliwahatua na kufanywa kua ni fursa ya kufikia malengo.
Aliwataka kuzidishaa ari, mori na nguvu na kuweka akili katika kuhakikisha yanayoyapangwa yanafikiwa kwa kiwango kikubwa, muda sahihi na ushirikiano mkubwa kwani idara hiyo imefanikiwa.
Akizungumzia suala la Rushwa, alisema bado katika jamii rushwa imekua ikitesa sana jamii, rushwa muhali na rushwa ya ngono, rushwa ya fedha hizo lazima zipaziwe sauti kwa vitendo, kwani rushwa ni adui wa maendeleo na taifa litakosa wasomi kwa maendeleo.
Mapema Mkurugenzi wa Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria Zanzibar Hanifa Ramadhan Said, alilishukuru shirika la UNDP katika utekelezaji wa mradi wa upatikanaji wa haki Zanzibar.
Alisema lengo ni kuimarisha masuala ya msaada wa kisheria, pamoja na kujitathmini kwani wanafanya majukumu yao kwa kwenda sehemu mbali mbali, taasisi pia zinatekeleza majukumu yao kwenda kwenye jamii.
Aidha alisema wasaidizi wa Sheria waliosajiliwa katka mfumo ni 250, na waliosajiliwa tena ni 39 kati ya hao 33 Pemba na 6 Unguja.
Kwa upande wake Msaidizi wa sheria Said Rashid alisema hata kama wafadhili watasita kufadhili, basi huduma za msaada wa kisheria zinapaswa kuendelea kutolewa.
MWISHO