Thursday, January 16

Mhe.Hemed Suleiman Atembelea Ujenzi wa Mradi wa Mabanda ya Maonesho Nyamazi Wilaya ya Magharibi “B” Unguja

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe Hemed Suleiman Abdulla amewaagiza viongozi na watendaji wa wizara ya Biashara na Viwanda  kuhakikisha wanasimia vyema Mradi wa ujenzi wa Viwanja vya Maonesho ya Biashara eneo la Nyamanzi ili mradi huo uweze kukamilika kwa wakati na kiwango kilichikusudiwa.

Akitembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa mradi huo huko Nyamanzi Wilaya ya Magharibi “B” Mhe. Hemed ameutaka Uongozi wa Wizara ya Biashara na Maendeleo ya Viwanda kuhakikisha kuwa mradi huo unakamilika kwa wakati uliopangwa na kuwasisitiza kuwa  Maafisa watakaokwenda China kwa ajili ya ununuzi wa Vifaa vya ujenzi wa mradi huo wana utaalamu na utambuzi wa Vifaa vyenye  ubora na Viwango vya hali ya juu ambavyo  vitadumu kwa muda mrefu.

Aidha amewaelekeza Mkandarasi na Mshauri elekezi wa mradi huo kuhakikisha  shughuli za ujenzi zinaendelea katika kipindi ambacho wanasubiri baadhi ya Vifaa vikamilike na kumtaka mshauri elekezi kuwepo katika eneo la ujenzi kwa muda wote ambao harakati za ujenzi zinaendelea ili kutoa ushauri atakapohitajika.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amempongeza na kumshukuru Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussen Ali Mwinyi kwa maono na maamuzi yake ya kujenga Mabanda ya Maonesho ya Bishara katika Viwanja vya Nyamanzi ili kutoa fursa kwa Wafanyabiashara kufanya biashara zao katika mazingira mazuri yenye hadhi na mnasaba wa maonesho hayo.

Amesema Mabanda hayo yatakapomalizika yatotoa nafasi kwa wafanyabiashara kutangaza biashara zao kwa muda mrefu ikiwezekana  hata baada ya Sherehe za Mapinduzi maonesho hayo yaweze kuendelea.

Sambamba na hayo Mhe.Hemed amempongeza  Mkandarasi wa ujenzi wa mradi wa Viwanja vya Maonesho ya Biashara Nyamanzi ambae ni (JKU) kwa kufanya kazi kwa uzalendo na kujitolea licha ya changacmoto mbali mbali zinazojitokeza katika ujenzi huo bado Mkandarasi  anafanya kazi kwa uharaka na ufanisi wa hali ya juu .

Nae Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Mhe. Omar Said Shaaban amesema Serikali imeamua kujenga Mabanda ya maonesho Nyamanzi ili kuboresha mazingira ya maonesho, wafanyabiashara kuweza kujitangaza na kuyafikia masoko ndani na nje ya nchi.

HABARI OMPR