NA ABDI SULEIMAN, PEMBA.
MKUU wa Wilaya ya Micheweni Mgeni Khatib Yahya, amesema vijana 15 waliomo katika mradi wa dumisha amani kwa maendeleo, kutoka Wilaya hiyo wamefanya kazi kubwa katika kuelimisha na kuhamasisha jamii, juu ya suala zima utunzaji wa amani kwa wananchi na vijana wa Wilaya hiyo.
Alisema vijana hao awali walipatiwa elimu juu ya suala zima la utunzaji amani, ili elimu hiyo kwenda kuifukisha kwa vijana wenzao katika maeneo mbali mbali.
Mkuu huyo aliyaeleza hayo wakati alipokua akizungumza na waandishi wa habari, mara baada ya kumalizika kwa zoezi la utoaji wa elimu kwa wananchi kijiji cha Wingwi Michungani katika wilaya hiyo, ikiwa ni utekelezaji wa mradi wa Dumisha amani kwa maendeleo endelevu unaotekelezwa na CYD kwa ufadhili wa UNDP.
Alisema kwa sasa hali imebadilika katika suala la utunzaji wa amani, hivyo baadhi ya matukio yamepelekea kupungua na mengine kupotea kabisa.
“Sasa viongozi kutoka vyama vya upinzani wanahudumia wananchi wote, hivi sasa kwenye suala la maendeleo watu wote tuko pamoja na sio kama ilivyokua zamani,”alisema.
Aidha aliwataka vijana hao 15 na CYD, kuendelea kuelimisha zaidi jamii, katika suala zima la utunzaji wa amani kwani bado kunamataifa wanaitafuta amani iliyopo Tanzania.
Mapema Mkurugenzi wa Kituo cha Majadiliano kwa Vijana Zanzibar (CYD) Hashim Pondeza, alisema CYD imeamua kutekeleza mradi wa Dumisha Amani kwa maendeleo endelevu hasa kwa vijana, baada ya kuona vijana ndio wahusika wakubwa kwenye kutengeneza amani au kuharibu amani hiyo.
Alisema lengo ni kuwafahamisha umuhimu wakutunza amani, ili nchi iendelee kuwa na amani, kwani vijana wanakumbana na vishawishi vingi, ikiwemo kisiasa, kidini na kiuchumi hivyo vijana aliwaasa vijana wasikubali kushawishiwa na kupelekea kuharibu nchi yao.
“Serikali imetimiza wajibu wake kutengeneza skuli zilizo za kisasa zaidi, vijana wajibu wenu sasa ni kusoma kwa bidii na kutimiza ndoto za kila mmoja katika suala la elimu na sio kufanya mambo yasiokua na maana,”alisema.
Kwa upande wake afisa maendeleo ya vijana kutoka Wizara ya Habari Vijana Utamaduni na Michezo Pemba Zadida Abdalla Rashid, alisema CYD imewasaidia vijana 15 wa Wilaya ya Wete na kuwapatia Milioni 7.5 na Micheweni Milioni 7.5, ambapo tayari vijana washaanzisha miradi yao ya maendeleo.
“Vijana 15 wa micheweni wao wameingia katika uchumi wa buluu, kwa kutengeneza bwawa la kufugia samaki na kaa, hawa ni vijana waliopatiwa elimu na CYD ili kuelimisha vijana wenzao juu ya umuhimu wa amani,”alisema.
Aidha alisema mradi huo unatarajiwa ingizwa vifaranga elfu 20 wa samaki pamoja na kaa, ili kuwafanya vijana kuendelea kubaki pamoja ikizingatiwa vijana wameitikia wito wa serikali wa kutaka kujiajiri wenywe.
Aidha afisa huyo alisema watahakikisha wanashirikiana na Wilaya kufuatilia mradi, ili lengo la CYD na vijana liweze kufikiwa kwa kufuata miongozo na kanuni.
Nae Afisa Mdhamini Wizara ya Habari Vijana Utamaduni na Michezo Pemba Mfamau Lali Mfamau, aliwataka vijana kutambua kua hakuna mbadala wa amani, hivyo ipo haja vijana hao kuendelea kutoa elimu juu ya umuhimu wa amani.
MWISHO