Sunday, November 24

Alhaj Dk. Mwinyi ameshiriki kwenye hitma na du’a maalum

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Al hajj Dk. Hussein Ali Mwinyi amejumuika na waumini wa Kiislamu kwenye Ibada ya Sala ya Ijumaa, huko Mkwajuni Kidombo, Wilaya ya Kaskazini A, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Mbali na ibada hiyo, Alhaj Dk. Mwinyi pia ameshiriki kwenye hitma na du’a maalum zilizosomwa baada ya ibada ya Sala ya Ijumaa kwa kuwaombea viongozi waliopo serikalini, wastaafu, masheikh na wazee walio hai na waliofariki dunia, ndani na nje ya Kijiji hicho.

Hafla hiyo pia ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa dini na Serikali akiwemo Makamu wa Kwanza na wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Mhe. Othman Masoud, Mhe. Hemed Suleiman Abdulla, Marais wastaafu, Alhaj Dk. Salmini Amour Juma na Alhaj Dk. Ali Muhamed Shein, Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh, Saleh Omar Kaab, Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Ayoub Mahmoud na viongozi wengine wa dini.

Alhaj Dk. Mwinyi pia alipata wasaa wa kusalimiana na wananchi wa Mkoa huo wa Kaskazini Unguja na kuwatakia kheir.

Akikhutubu kabla ya sala ya Ijumaa Khatib Sheikh, Abdulkarim Said Abdulla kutoka Ofisi ya Mufti wa Zanzibar, aliwasihi wananchi kuendelea kuwaombea du’a njema viongozi wa Serikali kwa kazi kubwa wanazozifanya za kuitumikia nchi na harakati zao za kuendelea kuiletea maendeleo.

Pia aliwaomba viongozi hao kuwaomba viongozi hao kuendelea kuwatumikia, kuwapenda na kuwahurumia raia.

Pia, Sheikh Abdulkarim aliikumbusha jamii ya Kiislam juu ya suala zima la kumpenda Mtume Muhammad (SAW) kwa kufuata mema yote na kuachana na mabaya aliyoyakataza.

Ibada hizo zilitekelezwa kufuaftia mwaliko kwa viongozi wa Kitaifa unaotolewa kila mwaka na Rais Mstaafu, Alhaj Dk. Salmin Amour Juma, ulioambatana na sherehe za usomwaji wa Maulid ya kumswalia Mtume Muhammad (SAW), kiijijini hapo.

IDARA YA MAWASILIANO, IKULU ZANZIBAR