Monday, November 25

Waliokabidhiwa bajaji watakiwa kufuata sheria za barabarani.

NA ABDI SULEIMAN, PEMBA.

KAMANDA wa Polisi Mkoa wa Kusini Pemba, kamishna msaidizi wa Polisi Abdalla Hussein Mussa, amewataka vijana waliokabidhia bajaji na uongozi wa bank ya NMB kuhakikisha wanazitunza kwa hali ya juu, pamoja na kufuata sheria zote za usalama wa barabarani wakati watakapokua njiani.

Alisema NMB imetoa bajaji hizo kwa vijana, kwa nia na lengo zuri la kuwasaidia katika kujipatia ajira na kujikwamua na umaskini.

Kamanda Abdalla aliayeleza hayo, wakati wa hafla ya kukabidhi bajaji nne kwa vijana, ikiwa ni mkpo kutoka bank ya NMB kwa vijana hafla iliyofanyika mjini Chake Chake.

“Vijana sote ni mashahidi hapa, na tunapaswa tuishukuru bank ya NMB kwa kutoa mkopo wa bajaji kwenu, chamsingi ni kufuata taratibu na sheria zote za usalama wa barabarani, wakati wote mutakapokua barabarani,”alisema.

Aidha aliwataka vijana hao kuzitumia bajaji hizo kwa lengo lililokusudiwa, pamoja na kutii sheria za usalama wa barabarani, kwani vyombo hivyo ni vya moto wasipotii watakamatwa kwa uvunjaji wa sheria na hawatokua na muhali na mtu yoyote.

“Tuelewane na kufahamiana mapema mutakapotii sheria za usalama wa barabarani, hakutakua na ugomvi baina ya wamiliki wa bajaji na jeshi la polisi, sasa vizuri kufuata taratibu,”alisema.

Mapema afisa Mdhamini Ofisi ya Rais Ikulu, Shuwekha Abdalla Omar aliipongeza NMB kwa kuwasaidia vijana, katika kuwapatia vyombo vya moto ambavyo vitaweza kuinua kipato chao.

Aliwataka vijana hao kuhakikisha wanakua makini muda wote wanapokua barabarani, pamoja na kurudisha mkopo kwa wakati ili vijana wengine waweze kupatiwa.

“Nyinyi leo ndio mutakaoifanya bank hii iweze kuwasaidia vijana wengine, pia nyinyi ndio mutakaoifanya benk hii isiwasaidie vijana wengine pale mutakaposhindwa kuwasilisha mikopo yenu,”alisema.

Kwa upande wake meneja wa bank ya NMB Pemba Hamad Mussa Msafiri, aliwapongeza vijana hao wachache ambao wamewapatia mikopo nafuu ya bajaji, nakuwataka kutambua kuwa wao ndio mfano kwa Pemba nzima na kuhakikisha wanavitunza vyombo hivyo na kurudisha mkopo kwa muda.

“Hapa leo sisi ni mashahidi munapewa vyombo hivi vinne, nyinyi ndio vielelezo kuendelea kupata mikopo au kukosa mkopo, mutakaporudisha vizuri na kwa wakati muwafaka basi mutawafanya na vijana wengine kupatiwa,”alisema.

Nae katibu mkuu wa jumuiya ya waendesha bobaboda na bajaji mkoa wa kusini Pemba Nassor Kombo Khamis, aliipongeza benk ya NMB kwa kutoa mikopo nafuu kwa vijana, kwani imetoa mikopo kwa vijana Tanzania bara na imeona ipo fursa ya kutoa kwa vijana wa kisiwa cha Pemba.

Aidha katibu huyo aliwataka vijana wenzake kutambua kua wamepatiwa vyombo hivyo kwa ajili ya kujikomboa na umaskini, hivyo wanapaswa kuvitumia vizuri na kutii sheria za barabarani na kutoa huduma nzuri kwa upande wa jamii.

Hata hivyo aliwashauri kuhakikisha wanarudisha mikopo kwa wakati, wasije wakaharibu wakiharibu watawakosesha vijana wenzao mikopo baadae, kwani mkopo ukilipa kwa wakati utapata kuwasaidia wengine.

MWISHO