NA HANIFA SALIM, PEMBA
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi dk, Hussein Ali Mwinyi amesema, serikali kwa kushirikiana na mashirika yasio ya Kiserikali yanawajibu mkubwa wa kuwawezesha wakulima, kuendeleza juhudi za uzalishaji wa chakula na hatimae kuongeza tija kwa maendeleo yao binafsi na jamii kwa ujumla.
Alisema, jitihada hizo zinathibitishwa na utayari wa serikali kwa kushirikiana na wadau mbali mbali wa maendeleo ambapo bajeti ya sekta ya kilimo imeongezeka kwa asilimia 84% kutoka shilingi Bilioni 53.9 mwaka 2022-2023 hadi kufikia Bilioni 98.7 mwaka 2023-2024.
Akizungumza kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Othman Massoud Othman aliyasema hayo alipokua akifungua maonesho ya siku ya chakula Duniani yaliyofanyika katika viwanja vya Chamanangwe Wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Alisema, katika kutekeleza mustakbali mwema wa nchi serikali kupitia wizara ya kilimo, maliasili, umwagiliaji na mifugo iliweza kuwaingiza wakulima takribani asilimia 20% wa Unguja na Pemba katika teknolojia ya kilimo cha kumwagilia kwa njia ya matone kwa aina mbali mbali za kilimo ikiwemo cha mboga mboga.
“Kilimo cha umwagiliaji wa zao la mpunga teknolojia ya uvunaji wa maji ya mvua kwa mabwawa matatu yenye uwezo wa kukusanya zaidi ya lita Bilioni 1 imetumika, mabwawa hayo ni Mlemele kwa Pemba, Kinyasini na Chaani kwa Unguja, ambayo yatakuwa na uwezo wa kudumu kuvuna maji kwa zaidi ya miaka 50 endapo yatatunzwa vizuri”, alisema.
Alieleza lengo la teknolojia hiyo ya upatikanaji na matumizi bora ya maji ni kuhakikisha kuwa uzalishaji na utumiaji wa maji wenye tija kwa mazao ya chakula, kuondokana na kilimo cha mazoea na kuelekea katika kilimo cha biashara ili kuweza kujipatia chakula cha kutosha, kipato na mauzo ya ziada.
Aidha alisema, suala jengine muhimu ni kuhakikisha matumizi bora ya ardhi ndogo iliyopo inatumika kwa uzalishaji wenye tija huku ikizingatiwa vyema afya ya udongo, kwani sasa hivi, kuna vifaa vya kupima afya ya udongo katika Wilaya zote za Zanzibar, hivyo ni vyema kuvitumia kwa vitendo ili dhamira iliyokusudiwa iweze kufikiwa.
Hata hivyo alisema, lengo la maonesho hayo ni kuhimiza mapinduzi katika sekta ya kilimo kwa kuelimisha mbinu bora ya kilimo, ufugaji, uhifadhi wa misitu na mazao yake ambapo miongoni mwa mbinu hizo ni kuwa na matumizi ya teknolojia.
Waziri wa Kilimo, Umwagiliaji Maji ,Maliasili na Mifugo Zanzibar Shamata Shaame Khamis, alisema ni mara ya nne Kisiwani Pemba kufanyika maonesho hayo ya siku ya chakula Duniani ambayo yanawakutanisha wajasiriamali na wakulima kutoka taasisi mbali mbali zenye mnasaba na shughuli za kilimo.
“Siku ya chakula Duniani kote huadhimishwa kila ifikapo Oktoba 16 ya kila mwaka ambapo kwa umuhimu wake Zanzibar tumeona tuanze Oktoba 10 ili wananchi waweze kujifunza kama vile serikali yetu inavotaka”, alisema.
Alisema, wizara ya kilimo kupitia maonesho hayo imepiga hatua kubwa kupitia sekta ya kilimo, maliasili, umwagiliaji na mifugo, kwa kushirikiana wizara, taasisi na sekta binafsi ambapo kwa upande wa Pemba mashirikiano hayo ni makubwa ukilinganisha na Unguja.
Akitoa salamu za wananchi Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini ambae pia ni Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Salama Mbarouk Khatib alisema, maendeleo makubwa yamepatikana Kisiwani humo kupitia sekta ya kilimo ikiwemo kupatikana mabadiliko ya kilimo kwa wakulima.
Akisoma risala ya maadhimisho hayo Katibu Mkuu wizara ya kilimo, umwagiliaji, maliasili na mifugo Zanzibar Seif Shaban alisema, ni utaratibu wa wizara ya kilimo kufanya maonesho hayo kila ifikapo Oktoba 10 ya kila mwaka ambapo maonesho ya mwaka huu yamepangwa kugharimu zaidi ya shilingi milioni 200 na 80.
Siku ya chakula Duniani huadhimishwa kila ifikapo Oktoba 16 ya kila mwaka ambapo kwa mwaka huu kauli mbiu ya maadhimisho hayo ikiwa ni “MAJI NI UHAI MAJI NI CHAKULA ASIACHWE MTU NYUMA”.
MWISHO.