Thursday, January 16

DK. Mwinyi ajuulia hali  mwandishi wa habari Mwandamizi Haji Ramadhan Suweid Buda

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Al hajj Dk. Hussein Ali Mwinyi ameendeleza utaratibu wake wa kuwajuulia hali wazee na wananchi kwenye maeneo mbambali kwa kuwaombea dua na kuwatakia kheir na shufaa wagonjwa wapone haraka kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu.

Alhaj Dk. Mwinyi amewatembelea bw. Haji Ramadhan Suweid Buda, mwandishi wa habari Mwandamizi na Mstaafu kwenye utumishi wa umma na mama mzazi wa Sheikh Samir Zulfikar wa Mahad el Juneid ya Mkunazini ambao wanaendelea na matibabu hospitali kuu ya Mnazi Mmoja.

Pia, Alhaj Dk. Mwinyi aliwatembelea wazee wa Chama cha Mapinduzi ambao walitoa mchango mkubwa kwenye chama hicho, akiwemo bw. Kombo Mzee Kombo nyumbani kwake Miembeni Mkoa wa mjini Magharibi, bw. Bora Afya Silima Haji nyumbani aliekua Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mjini kichama nyumbani kwake Mwembelikunda na bi. Hiari Miraji Othman, Balozi wa nyumba 10 namba mbili huko nyumbani kwake Miembeni jitini.

Mapema, Alhaj Rais Dk. Mwinyi alijumuika na waumini wa dini ya Kiislam na wananchi wa Miembeni kwenye ibada ya sala ya Ijumaa kwenye msikiti wa Ijumaa, Miembeni, Wilaya ya Mjini.

Akizungumza kwenye ibada hiyo Katibu Mtendaji kutoka Ofisi ya Mufti Zanzibar, Sheikh Khalid Ali Mfaume aliwahimiza waumini wa Kiislam umuhimu wa tabia njema na kueleza tabia njema ni misingi ya mambo manne ikiwemo imani.

Sheikh Khalid alieleza, kwenye tabia njema imani hudumu kwa kutekelezwa amri za Allah (S.W) pamoja na kufuatwa makatazo yake.

Pia, alieleza kukosekana kwa tabia njema imani hupungua na kuongezeka kwa vitendo vya kuporomoka kwa maadili ikiwemo kupungua kwa heshima kwenye familia na jamii.

Alisema, siku hizi watoto hawawaheshimu wakubwa zao wakiwemo wazazi na walezi hata jamii zinazowazunguruka, aliiasa jamii ili kupunguza wimbi la ukosefu wa maadili na kuepusha athari kubwa za ndoa na takala zinazojitokeza kwenye jamii ni vyema kutafuta njia za busara ili kukinusuru kizazi cha sasa kilichogubigwa na wimbi la ukosefu wa heshima na maadili.

Pia, aliiasa jamii kuendelea kuwafundisha mema watoto ili kukuza jamii yenye heshima, maadili mema na tabia njema.

Kwa upande wake, Khatib wa ibada hiyo ya sala ya  Ijumaa aliiasa jamii kwamba uzuri wa waumini na waislam ni elimu, adabu na kuheshimu viongozi na jamii inayowazunguruka kwa kujiepusha kutoa maneno yasiyofaa kwa viongozi, wazazi na jamii ili kujenga jamii iliyonjema.

IDARA YA MAWASILIANO, IKULU ZANZIBAR