NA AMINA AHMED-PEMBA.
Taasisi ya utafiti wa kilimo Zanzibar (ZARI) kwa kushirikiana na shirika la World Vegetable Center chini ya ufadhili wa USAID limetoa mafunzo ya uzalishaji mbegu bora kwa wakulima wa mboga mboga na matunda kutoka maeneo mbali mbali kisiwani Pemba kwa lengo la kusaidia kupunguza gharama za ununuaji wa mbegu sambamba na kuondoa usumbufu unaowakabili juu ya mbegu zisizo na tija .
Akizungumza katika mafunzo hayo msimamizi wa mradi wa kilimo cha mboga mboga kutoka taasisi hiyo Khadija Ali Juma amewataka wakulima hao kujikita katika kilimo cha mbegu ili kuweza kupata faida mbali mbali .
Alisema licha ya kupata mboga kwa ajili ya kuendeleza kilimo chao wenyewe lakini pia ni moja kati ya fursa za kibiashara kwa wakulima ambacho kitawasaidia kuongeza Kipato.
Kwa upande wake Abdul rahim Ramadhan Hassan kutoka taasisi hiyo alisema kuwa muitikio mzuri uliooneshwa na wakulima juu ya uchakataji mbegu za mazao, mboga mboga na matunda Zanzibar utasaidia kufikia malengo yaliowekwa na taasisi hiyo ya wakulima kuweza kuzalisha mbegu bora wao wenyewe bila kuagiza kutoka nje.
Awali akitoa mafunzo ya nadharia na vitendo juu ya mkufuzi kutoka shirika la World vegetable center Omar Mbwambo alisema kuwa upatikanaji wa mbegu bora za kilimo cha mboga na matunda mkulima anashauriwa kuvuna mazao mara baada ya kukomaa sambamba na kuweka mazingira mazuri yatakayosaidia kuhifadhi mbegu zisiharibike.
kwa Upande wake mshauri wa mradi juu ya mazao ya kilimo kutoka Shirika la World vegetable center Hassan Mndiga amesema kuwa mradi huo umejikita katika kushauri wakulima juu ya Afya na rutuba ya udongo, mifumo ya kuzalisha mbegu bora zenye rutuba, kutizama thamani ya mazao kuanzia shamabani hadi sokoni, Usalama wa chakula, sambamba na kukuza kipando cha bustani za mboga na mazao ya nyumbani na mashuleni.
Wakuzungumza baadhi ya wakulima walioshiriki katika mafunzo hayo ya uchakataji wa mbegu akiwemo Aziza Saidi Ali mkulima wa mboga mboga na matunda kutoka Ole, alisema kuwa licha ya kulima mazao hayo mda mrefu lakini alishindwa kuzalisha mbegu kupitia elimu hiyo kutasaidia kupata mabadiliko yatakayokuza kilimo chake.
Nae Sleiman Said Muhammed Mkulima kutoka Mtakata Wawi amesema mafunzo hayo yataongeza uwezo wa kulima kilimo cha biashara na kuzalisha mbegu.
Mafunzo hayo ni muendelezo wa utolewaji elimu juu ya kilimo cha mboga mboga na matunda ambapo awali wakkulima hao walupatiwa elimu juu ya utambuzi wa udongo, pamoja na namna bora ya kulima shamba.
Mwisho.