NA, AMINA AHMED MOH’D- PEMBA.
Kila aneyepanda mbegu hutarajia mavuno mazuri na pale ambapo mti ukiwa haujashuhulikiwa vizuri basi mazao yake huwa madogo na pengine yasiwe na ubora wa kuridhisha wala kuvutia.
Hivyo hivyo huwa kwa kikundi cha watu kinapoamua kuunda jumuiya au taasisi kwa vile baada ya uzazi huitajika malezi na hio pia sio kazi rahisi.
Kazi ya malezi imekuwa na changamoto zisizo hesabika kidoleni kwa taasisi na jumuiya nyingi Zanzibar na unaweza kusema nyengine zipo kwa jina tu.
Hali hii ndio inayopelekea baadhi ya wakati kusikika Msajili wa Asasi za kiraia akitaka kuzifuta baadhi ya asasi kwa vile shughuli zake hazionekani.
Moja ya taasisi ambayo kuwepo kwake kulitetereka na jamii ikawa haioni kwa vitendo shughuli ziliopelekea kuundwa kwake ni ya mwamvuli wa asasi za kiraia Pemba Association for civil Society PACSO iliyoanzishwa mwaka 2005.
Kwa zaidi ya miaka 10 PACSO ilikabiliwa na changamoto ya wanachama kwa vile shughuli zake zilitiliwa mashaka na kutoweza kufanya vizuri kuzileta pamoja taasisi zisizo za kiserikali zilizopo Pemba ili kutimiza lengo la kuundwa kwake.
Tabaan, kuanzisha taasisi mpya sio kazi rahisi na hasa ikiwa inahusisha jamii pana na yenye watu wenye malengo na mitazamo tafauti ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.
Hata hivyo, PACSO ilihimili dhoruba kali lakini mwenendo wake ulikuwa wa kuchechemea na safari yake kuwa ngumu na malengo yake mengi kushindwa kuyafikia.
Lakini hatimaye akatokea mwana mama aliyeitafuta na kuipata njia ya kuifufua na kuiimarisha PACSO na sasa kuwa taasisi imara ambayo kazi zake zinafahamika na kutambulika kisiwani Pemba na nje.
Mwanamke huyu aliyeleta mageuzi katika PASCO na kuthibitisha uwezo wa mwanamke wa kuwajumuisha wana jamii na kuwaongoza kwenye safari ya maendeleo ni Sifuni Ali Haji ambaye hivi sasa ni katibu mkuu wa huu mtandao wa asasi za kiraia Pemba.
Kutokana na juhudi zake mwamvuli huu uliweza kuvutia wananchama 20 tu kwa zaidi ya miaka 10 wakati lengo lilikuwa kuwaweka pamoja wanachama wasiopungua 100 kati ya 264 waliopo kisiwani Pemba.
Hawakukosea wale waliosema “Nyuma ya kila mafanikio yeyote kuna juhudi za mwanamke “.
Miongoni mwa sababu zilizopelekea kutokuaminika ipasavyo kwa taasisi hiyo hapa kisiwani Pemba ni pamoja na usimamizi wa awali uliokuwa ukisua sua na kupelekea kupoteza utendaji kazi mzuri wa kuaminika.
Kazi haikuwa rahisi na iliendelea hivyo hivyo kuwa na wanachama wake 20 ambao ni taasisi za kiraia bila mafanikio yeyote.
Chini ya uongozi wake migogoro ya wenyewe kwa wenyewe iliyokuwepo kwa muda mrefu ndani ya asasi ilipata ufumbuzi na kwa sasa unaweza kusema mafanikio na malengo ya uanzishwaji wa taasisi hiyo yamefikiwa kwa asilimia 50.
Chini ya uongozi wake tasasi ilianzisha miradi mbali mbali ambayo faida zake zinaonekana na hazihitaji kumurikwa tochi.
” Kabla ya mimi kushika nafasi ya ukatibu kulikuwa na katibu mwanamme ambae aliiwacha nafasi hii mwaka 2015 baada ya kuona malengo hayatimii mambo hayaendi sawa mwaka 2015 na akaamua kuondoka ndani ya taasisi”.
Alisema mara baada ya kushika nafasi ya katibu alifanya utafiti wa kujua mapungufu yako wapi ili asizidi kuikwamisha taasisi na bada ya hapo ndio akapanga kazi za kufanya, hatua kwa hatua.
“Taasisi haikuwa na miradi na tokea kuwa katibu tumefanikiwa kuwa na miradi mitatu ambayo inasaidia wananchama , wasio kuwa wanachama pamoja na wana jamii, Ninafurahia mafanikio tulioyapata’, Bi Sifuni alisema.
Alisema taasisi hiyo imeweza kusaidia na kuzijengea uwezo jumuiya wanachama kutokana na kuwapatia elimu nahii ndio ilioshajihisha kupata wanachama zaidi’’, aliongeza.
‘’Kitu muhimu katika uongozi ni wa taasisi kuweka mbele maslahi na malengo ya taasisi “, alieleza.
Alisema kati ya asasi 110 zilizojiunga na mwamvuli huo 30 zimefanikiwa kuandika miradi ya maendeleo kutokana na kupata elimu ya uwandishi wa miradi.
WITO WAKE KWA WANAWAKE
Bi Sifuni aliwataka wanawake waliopo Pemba kuzichangamkia fursa zinazotokana na asasi za kiraia katika kujikomboa na kuonesha uwezo wao wa kiutendaji kama yeye alivyothubutu kuleta mageuzi.
Asasi za kiraia, zikiendeshwa vizuri na kwa uwazi, haziwekewi vizingiti na serikali.
Lilio muhimu ni kufanya kazi kama ilivyobainishwa katika Sheria ya Jumuiya namba 6 ya 1995 ambayo inatumika kuzitambua, kuzisajili, kuongoza, kuweka masharti, utaratibu, muongozo wa uendeshaji na usimamizi.
Kupitia sheria hii asasi za kiraia zimegawika katika makundi ikiwemo ya asasi katika maeneo ya kazi maalumu, eneo maalumu, nchi maalumu, sambamba na mataifa maalum.
Ashrak Hamad Ali, ambaye ni Mratibu Ofisi ya Msajili wa Asasi za Kiraia upande wa Pemba alisema ofisi hiyo inatambua mchango mkubwa unaofanywa na taasisi za kiraia Pemba, ikiwemo PASCO.
“Hivi sasa taasisi nyingi za kiraia (NGO’s) kupitia Pacso zimekuwa na utayari waa kutoa mashirikiano kwa serikali kwa kutambua wao ni kama daraja la kazi za kuitumikia jamii” .
Alisema baadhi ya taasisi Pemba zilikuwa katika hali ngumu, lakini hivi sasa kwa msaada mwamvuli wa PASCO zinaendeshwa kisheria kama taasisi nyengine.
KAULI ZA WANACHAMA WA PACSO
Tatu Abdalla Msellem wa jumuia ya Tumaini Jipya (TUJIPE) alisema mwamvuli umewasaidia kutambulika uwepo wa taasisi zao kisheria na unaendelea kuwasaidia kupata misaada ya kuendeleza shughuli zao.
Alisema anafurahia kuiona PASCO inaendesha shughuli zake kwa uweledi na ina inazisaidia asasi kupata misamaha katika kodi.
kwa upande wake Alawi Bakar Hamad, Mkurugenzi wa taasisi ya Popular Inspiring and Relief Organization ( PIRO ) Pemba ambayo ni miongoni mwa wanachama waliojiunga na mwamvuli huo wa PACSO ameishukuru PASCO, kwani wamekuwa na uhusiano mzuri baina yao na serikali na taasisi nyengine katika kutekeleza shughuli mbali mbali
Mwisho.