NA ABDI SULEIMAN,PEMBA.
SHIRIKA la Umeme Zanzibar Tawi la Pemba, limepokea vifaa mbali mbali vilivyokua vilikosekana kwenye makabidhiano ya mradi wa umeme wa jua, katika Kisiwa cha Kokota na Njao kutoka kampuni ya Photons Energy LTD iliyoshinda tenda ya ujenzi wa mradi huo.
Vifaa hivyo vilivyokabidhiwa ni kwa ajili ya kwenda kufungwa kwenye nyumba za wateja wao, ili kulinda hitilafu zinazotokea na kupelekea mtambo wa uzalishaji wa umeme kuzimika.
Hafla ya makabidhiano hiyo yamefanyika katika ofisi za ZECO Tibirinzi Chake Chake Pemba, na kuhudhuriwa na viongozi wa shirika hilo, pamoja na mkurugenzi wa ufundi wa kampuni ya Photons.
Kaimu meneja ZECO Pemba Mohamed Ali Juma, ameipongeza kampuni ya Photons Energy LTD, kwa kutekeleza kwa vitendo ahadi yake licha ya mradi kuwa umeshakabidhiwa ZECO.
“Leo tupo hapa kwa madhumuni makubwa ya kukabidhi vifaa, ambavyo vilikosekana katika makabidhiano makubwa yaliyofanyika ya mradi huu kutoka kwa mkandarasi kuja kwetu ZECO,”alisema.
Nae Mkurugenzi Ufundi wa Kampuni ya Photons Energy LTD ya Arusha Roman Shayo, alisema wamelazimika kuja kukabidhi baadhi ya vifaa vilivyobakia katika utekelezaji wa mradi licha ya mradi huo kukabidhiwa ZECO kwa sasa.
“Mradi tulikua nao sisi na tukabakia nao mwaka mzima, sasa uko ZECO ila kuna vifaa vilikosekana wakati wa makabidhiano ya mradi ndio leo tumekuja kutekeleza, sisi na ZECO tuko pamoja kwa lolote lile,”alisema.
Aidha alisema bado wako tayari kusaidiza ZECO kitu chochote kitakachotokea kwenye mradi wa umeme wa jua Kisiwa cha Njao na Kokota nda ya kipindi cha miaka mitano na watasaidia wakihitajika.
Kwa upande wake Msimamizi wa umeme wa jua Kisiwa cha Kokota na Njao Wilaya ya Wete, Mhandisi Ali Faki Ali, alisema mradi ulianza mwishoni mwaka 2001 na kukamilika Mei 2022, baada ya kukamilika ulikua chini ya mkandarasi kwa mwaka mmoja, hivyo Julai 2023 wamekabidhiwa ZECO hadi sasa.
Alisema kipindi ambacho mradi upo chini ya mkandarasi, kuna vitu viligundulika ikiwemo wateja wengi wanatumia soket break, ambazo haziko na viwango zikawa zinaleta hitilafu kwa mtambo, baada ya kuwasili
Aidha alisema kampuni hiyo vifaa walivyokabidhi ni pamoja na sokot break za kisasa zaidi ya 200, zitakazokwenda kufungwa kwa wateja wote wa visiwa viliwi 176, ili kuzuwia tatizo lililokua likijitokeza la kuzima mtambo baada ya hitilafu kwa mteja inapotokea.
Nae afisa mawasiliano na huduma kwa wateja ZECO Pemba Haji Khatiub Haji, aliwataka wananchi wa visiwa hivyo kuwa wastahamilivu na moyo wa subra, ZECO itahakikisha wateja wote wanafungiwa vifaa hivyo vipya.
MWISHO