Wednesday, January 29

Kodi ya majengo haitolipwa kwa wananchi wote, Kamishna Mwenda

NA ABDI SULEIMAN, PEMBA

KAMISHNA Mkuu wa Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRA) Yussuph Juma Mwenda, amewahakikishia wananchi wa Zanzibar kuwa, Kodi ya majengo haitolipwa kwa wananchi wote bali ni kwa wale wenye uwezo tu.

Alisema wanaopaswa kulipa kodi hiyo ni wale wamiliki wa majengo ya biashara yenye gorofa, majengo ya gorofa ya makaazi, majengo mengine ya biashara na majengo ya Hoteli.

Mwenda aliyasema hayo huko katika Ukumbi wa baraza la Wawakilishi Wete, wakati alipokuwa akizungumza na viongozi mbali mbali wa Mkoa wa Kaskazini Pemba, pamoja na masheha wakati wa kutoa ufafanuzi juu ya kodi ya majengo Zanzibar.

Alisema kuwa Kodi ya majengo haimuhusu mwananchi wa kipato Cha chini, na badalayake wanaopaswa kulipa kodi hiyo ni wale tu wenye uwezo wao.

“Kodi hii sio ya watu wote bali ni wale wenye majengo ya gorofa, majengo ya biashara hawa uwezo wao ni mkubwa na wanachjangia tu, wale waliojenga na nhyumba zao kupangisha au ameweka duka atachangia kodi ya jengo,”alisema.

Alisema kodi hiyo inapaswa kulipwa na mmiliki wa jengo husika na sio mpangaji wa nyumba, aliwataka Masheha kuwa Kodi hiyo haitohusu sehemu zote za majengo ya Serikali au nyumba za ibada isipokuwa zile ambazo zitakuwa na sehemu za biashara yu.

Aidha kamishna huyo aliwataka Masheha hao kila wanapofanya manunuzi au kuuza kitu, ni vyema kudai risiti za kieletroniki ili kumuunga mkono Rais wa Zanzibar Dkt.Hussein Ali Hassan Mwinyi katika kuleta maendeleo.

Mapema akifungua kikao hicho, Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Pemba Salama Mbarouk Khatib, aliwataka Masheha kushirikiana na ZRA katika kuhakikisha inatekeleza vizuri majukumu katika maeneo yao.

Aidha Mkuu huyo alimuhakikishia, Kamishna Mwenda kuwa Ofisi yake itakuwa bega kwa bega, kuhakikisha wananchi wa Mkoa huo wanalipa kodi zao bila ya tatizo lolote.

Mkuu huyo wa Mkoa aliwataka masheha hao kutambua kuwa kodi ya nyumba, ipo zamani lakini Serikali ilikuwa haijaweka msisitizo juu ya kodi hiyo.

“Hapa lazima tuwe makini kodi hii ya nyumba, isiwe ni sababu ya kuingiza katika mambo ya kisiasa, nchi mbali mbali duniani zimekuwa zikiendeshwa na kodi za wananchi, hivyo kodi ya nyumba kwa nchi za wenzetu ni jambo la kawaida tu,”alisema.

Hata hivyo aliutaka uongozi wa ZRA kuchukuwa hatua za makusudi kutoa elimu kwa wananchi, ili waweze kufahamu kodi hiyo kwani hivi sasa kodi hiyo imeshaleta sitofahamu kwa wananchi, huku baadhi yao wakiuhusisha na mambo ya kisiasa

Nao Wakuu wa Wilaya za Wete na Micheweni, waliahidi kuhakikisha kuwa elimu waliyoipata wataweza kuwafikishia wananchi wao, ili waweze kuelewa ni nani ambae anapaswa kulipa kodi hiyo.

Nae Mkurugenzi wa Bodi ya Mapato Zanzibar ZRA Pemba Jamal Hassan Juma, alisema kodi hiyo haitokuwa na athari yeyote kwa wananchi wa chini, hivyo ni vyema kwa Masheha kuchukuwa juhudi za makusudi kuwaelimisha wananchi wao

Alisema kodi ya majengo ilianzishwa tokea mwaka 2008, lakini hivi Sasa ndio Sheria hiyo itakapoanza kutumika na kodi hiyo itahusu nyumba za ghorofa na zile za biashara tu.

 

MWISHO.