NA ABDI SULEIMAN, PEMBA.
MKUU wa Wilaya ya Chake Chake Abdalla Rashid Ali, amesema uwepo wa Amani katika jamii ni kichecheo kikubwa cha maendeleo katika taifa, hivyo ni jukumu la kila mmoja kuhakikisha suala hilo analipa nafasi kubwa katika maisha yake ya kila siku.
Mkuu huyo aliyaeleza hayo wakati wahafla ya uzinduzi wa Mradi wa Wanawake na Amali katika Wilaya hiyo, unaotekelezwa na kituo cha majadiliano kwa vijana Zanzibar (CYD) umefadhiliwa na shirika la WIIS-Kenya kwa kushirikiana na USIP na kufanyika mjini Chake Chake.
Alisema yapo mataifa mbali mbali yalikuwa na uwezo mkubwa wa kimaendeleo, kutokana na kutoweka kwa amani kwenye mataifa hayo, maendeleo yalitoweka kama umweso na sasa wamekuwa wakiitamani irudi, lakini walishachelewa na kuingia katika mizozo isikwisha.
Alisema mradi huo katika Wilaya ya Chake Chake na Taifa zima ni muhimu, ikizingatiwa viongozi wakuu wa nchi Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan wa Tanzania na Rais Dkt. Hussein Ali Mwinyi wamekuwa wakipambana kwa kila hali kuona amani inaendelea kudumu nchini.
Alisema miongoni mwa hatua zinazochukuliwa na serikali ni pamoja na kuwezesha upatikanaji wa huduma mbali mbali ikiwemo chakula, ili kila mwananchi aweze kufanya shughuli zake kwa utulivu.
“Sisi Viongozitunawapongeza wenzetu wa wa CYD kwa kubuni mradi huu, kwa kina mama kwani wanawake wanao mchango mkubwa katika kuendeleza amani ya taifa la Tanzania,”alisema.
Aidha aliitaka jamii kuendelea kuitunza amani na kuepukana na migogoro mbali mbali ikiwemo ya ndoa, ardhi na udhalilishaji yote hiyo ni kichocheo cha uvunjifu wa amani, lakini jamii imekua mstari wambele kukimbilia suluhu pale wanapokutwa na migogoro.
Naye Mkurugenzi wa CYD Hashim Pondeza, aliwataka wanawake katika maeneo mbali mbali kujikita katika kutunza amani, kuanzia majumbani mwao ikizingatiwa kuwa wao ndio wanaoyajua masuala mengi, yaliyopo katika jamii yakiwa katika hatua za awali.
Alisema lengo la mradi huo ni kutaka kuwashirikisha wanawake juu ya masuala ya amani, ili waweze kufahamu zaidi amani na usalama katika maeneo yao, ili kusaidia kwenye kampeni za kitaifa za kupambana na kupinga matendo yanayoweza kupelekea uvunjifu wa amani ikiwemo udhalilishaji.
“Wanawake wanamchango mkubwa katika kuhakikisha amani inadumu, na wakitaka kuipoteza basin i mara moja, kwa vile muda mwingi wanakua majumbani hata wageni basi wanawajua wao wanapoingia,”alisema.
Mapema Mratibu wa Ofis wa Mrajisi wa Asasi za Kiraia Pemba Ashrak Hamad Ali, alisema kuwafundisha wanawake masuala ya amani ni jambo kubwa sana, kwani wanawake wanajua mambo mengi na makubwa yaliyo katika jamii.
Alisema yapo matendo katika jamii kama vile vitendo vya udhalilishaji, rushwa, uhujumu wa uchumi kunachangia kuwepo kwa viashiria vya uvunjifu wa amani na kukosekana utulivu kwenye jamii.
Akichangia katika uzinduzi wamradi huo, Samira Omar alisema kuwepo kwa umaskini wa kipato kwa wananchi na uduni wa maisha, kunapelekea kuwepo kwa mkanganyiko wa jamii katika kujikimu kimaisha.
Naya Salma Khamis Haji, alisema jamii endapo itazitumia ipasavyo fursa mbali mbali zinazotolewa na serikali, kama vile ruzuku na mikopo itawawezesha kujikita kwenye masuala ya uzaalishaji mali, na kuondokana na kujiweka kwenye vijiwe visivyo na tija.
Kwa upande wake Mwalimu katika skuli ya msingi ya Michakaini A Fatma Haji, alisema baadhi ya wanaume kutowajibika vyema katika kuhudumikia watoto na kumuachia mama pekee, kunapelekea ndoa kuvunjika na wanawake kushindwa kuwapatia huduma stahiki watoto wao, hali inayopelekea kujiingiza kwenye shughuli zisizo saizi yao.
Akiwasilisha mada Dr. Moh`d Said, aliwataka wazazi/walezi kuwa macho kuona watoto wao hawatumbukii kwenye mrengo mbaya, kwani wanaweza kupelekea kuwapoteza watoto wao, pamoja na kutambua mabadiliko yao mapema.
MWISHO