Thursday, January 16

Wahamasishaji jamii wawasilisha changamoto na mafanikio

NA ABDI SULEIMAN, PEMBA   

MASHEHA na viongozi wengine katika maeneo tofauti, wameombwa kutoa mashirikiano ya dhati kwa wahamasishaji jamii waliopo kila Wilaya Kisiwani Pemba, ili kuweza kuibua changamoto zilizopo ndani ya jamii na kuweza kuchukuliwa hatua na mamlaka husika.

Wito huo umetolewa na Mkurugenzi wa Mradi SWILL Hafidh Abdi Said, wakati akizungumza katika kikao maalum kilichowakutanisha wahamasishaji jamii, Masheha wa wilaya nne na baadhi ya watendaji wa serikali huko katika ukumbi wa KHUHAWA mjini Chake Chake

Alisema kupitia wahamasishaji jamii hao, wanaendelea kuibua changamoto mbali mbali kama vile ukosefu wa huduma ya maji safi na salama, upatikaji wa vyeti vya kuzaliwa, utoro wa wanafunzi, uhaba wa walimu, madaktari na uchakavu wa miundombinu ya barabara, zilizoweza kuibuliwa katika jamii na nyengine kupatiwa ufumbuzi.

Aidha alisema mafanikio hayo yametokana na mashirikiano ya dhati baina ya wahamasishaji jamii, masheha na wadau waliofikiwa na jamii kupata kueleza changamoto zilizopo kwenye maeneo yao.

Alisema Mradi SWILL unatekelezwa kwa pamoja kati ya TAMWA  Zanzibar, ZAFELA na PEGAO kwa ufadhili wa Ubalozi wa Norway Tanzania, unalengo la kufungua fursa zaidi za ushiriki wanawake katika nafasi ya uongozi, kwenye vyama vya kutoa maamuzi katika uchaguzi mkuu ujao, ili kuona wanawake wengi wanajitokeza kuwania nafasi majimboni, kwenye wadi na hatimae wachaguliwe kwa idadi kubwa.

“Bado nafasi za ushiriki wa wanawake kwenye kwenye vyombo vya kutoa maamuzi haijakizi mahitaji ya kikatiba, huu ndio wakati wa kuwanda wanawake wengi zaidi watakaohamasika kushiriki kwenye chaguzi mbali mbali, watakapoingia kwenye vyembo hivyo kuwakilisha majimbo au wadi zao, watakuwa na sauti nzuri kuwatetea wanawake wenzao kupitia changamoto walizonazo,”alisema.

 

Akiwasilisha Changamoto na mafanikio waliyopata katika ufuatiliaji wao, Muhamasishaji Jamii Wilaya ya Micheweni Semeni Ali Khamis, alisema miongoni mwa changamoto ni ukosefu wa huduma za maji safi na salama katika shehia za Shumba Viamboni, Kipangani, Mihogoni, Makangale, Kinoe na Kipangani Shehia ya Mlindo.

Alisema changamoto nyengine ni Uchakavu wa miundombinu ya barabara, baadhi ya vijiji kutofikiwa na huduma ya umeme, utoro wa wanafunzi, mashamba ya wakulima kuingiliwa na maji katika Shehia ya Kinoe, umbali wa upatikanaji wa huduma za kijamii ikiwemo shule na vituo vya afya huku akitolea mfano eneo la Bandari Kuu Mlindo.

Kwa upande wa mafanikio alisema ni pamoja na baadhi ya maeneo kusogezwa huduma za kijamii, kama vile kuajiriwa kwa walimu, kuanzishwa kwa madarasa ya kisomo shehia ya Kinoe.

Kwa upande wa ripoti ya Wahamasishaji kutoka Wilaya ya Wete, iliyowasilishwa na Husna Ali Said, alisema moja ya changamoto ni ukosefu wa vyoo kwa jamii, katika kisiwa kidogo cha Kojani, kukosekana kifuta jasho kwa walimu wanaofundisha katika madara ya kisomo cha watu waliyoyaadhisha.

Hata hivyo alisema tayari, baadhi ya changamoto hizo zimeanza kupatiwa ufumbuzi ikiwemo kujengwa vyoo vya jamii katika kisiwa cha kojani, kufanyiwa ukarabati kwa baadhi ya skuli ambazo zilikuwa hali mbaya ikiwemo ya maandalizi ya Machengwe.

Akiwasilisha changamoto za wilaya ya Chake Chake Hasina Omar Salum, ni kukosekana kwa darasa la kisomo shehia ya Kibokoni, usambazaji umeme kijiji cha Kwamburi na ukosefu wa huduma ya maji kwa maeneo mengi ya Chake Chake.

Alisema changamoto nyengine ni uwepo wa vijana wengi katika shehia ya wara, kujiingiza kwenye vitendo vya biashara ya kuuza na utumiaji wa madawa ya kulevya, kutoendelezwa kwa barabara ya ndani kutoka Mkanjuni hadi Muharitani.

 

 

Kwa upande wa wilaya ya Mkoani, wamesema utoro wa wanafunzi katika skuli ya msingi Wambaa, Dodo na Jambangome, uchakavu wa barabara ya Mzingani–Wmbaa, Jambangome-Kichunjuu inayowapatia usambufu mkubwa wa kusafiri wananchi wa maeneo hayo.

Akizungumzia changamoto ya ukosefu wa maji katika maeneo mbali mbali ya kisiwani Pemba Ali Haji Mbwana kutoa ZAWA, alisema changamoto hiyo inasababishwa na umeme kuwa mdogo katika visima vingi na uchakavu wa miundombinu hata, hivyo alisema juhudi kubwa zimechukuliwa kubadilisha miundombinu hasa ya mabomba, kazi ambayo inaendelea kwenye maeneo tofauti.

Naye Abeida Abdi kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, alisema wizara hiyo kupitia idara yake ya elimu mbadala na watu wazima, imekuwa ikichukua juhudi kubwa kuwarejesha watoto walitoroka maskulini na kupitia mradi maalum uliopo  na watoto wengi wamesharejeshwa.

 

MWISHO