MARYAM SALUM ,PEMBA
Wafanyabiashara kisiwani Pemba wametakiwa kulitumia Baraza la ushindani halali la biashara la Zanzibar , kufikisha malalamiko yao ya rufaa baada ya kutolewa maamuzi na mamlaka za udhibiti.
Kauli hiyo ilitolewa na Ofisa kutoka Baraza hilo Fatma Gharib Haji wakati akizungumza na wajumbe wa kamati ya Baraza la biashara la Mkoa wa Kusini Pemba katika ghafla fupi ya kujitambulisha iliyofanyika ukumbi wa Tasaf Chake chake.
Alisema iwapo wafanya biashara watalitumia Baraza la ushindani halali la biashara wataweza kuondokana na migogoro inayojitokeza na kupata haki zao kama inavyotakiwa.
Alieleza miongoni mwa majukumu ya Baraza la ushindani halali la biashara ni kusikiliza rufaa na kutowa maamuzi kwa wafanyabiashara na wale wote ambao wana malalamiko dhidi ya mamlaka za udhibiti katika masuala ya uhalali wa biashara na kumlinda mtumiaji.
Alifahamisha ili mfanyabiashara aweze kulitumia Baraza hilo anatakiwa awe ameshapeleka malalamiko yake yanayohusiana na masuala ya ushindani pamoja na kumlinda mtumiaji katika mamlaka za udhibiti na tayari zikiwa zimeshatowa maamuzi dhidi ya malalamiko hayo.
“Iwapo mfanyabiashara hakuridhika na maamuzi yaliyotolewa na mamlaka ya udhibiti ndipo anaweza akakata rufaa Baraza la ushindani halali la biashara kwa ajili ya kupata haki yake anayostahiki”,alisema.
Alisema katika hatuwa nyengine mfanyabiashara anaweza kupeleka maombi ambapo yametolewa maamuzi na mamlaka ya udhibiti na hakuridhika nayo, hivyo anaweza kuliomba Baraza hilo kufanya maamuzi ambayo yeye anahisi yanaweza yakamletea haki yake.
Akiwasilisha mada kuhusu baraza halali la ushindani wa biashara, Fatma Ali Yahya alisema mamlaka za udhibiti sio msimamizi wa mwisho wa kuamuwa na wanavotakiwa iwapo mtu hakuridhika na yale maamuzi waliyotowa akate rufaa katika baraza hilo.
Alifahamisha kuwa baraza hilo lipo kwa ajili ya kutatuwa changamoto zinazowakumba wafanyabiashara,wajasiriamali na wawekezaji katika hatuwa ya rufaa .
“Wajumbe muliomo humu ni jukumu lenu sasa kuufikisha ujumbe huu kwa wafanyabiashara ili waweze kufikisha malalamiko yao katika baraza halali la ushindani wa biashara ili kuondokana na migogoro isiyo ya lazima”,alisema.
Mapema mwenyekiti wa kikao hicho Mkuu wa Mkoa Kusini Pemba Matar Zahor Massoud alisema zipo jitihada mbalimbali zinazofanywa na Serikali kuhakikisha wafanyabiashara wanapatiwa mazingira mazuri ya kufanya biashara zao.
Alieleza kuwa zaidi ya Bilioni nne zimetolewa katika mkoa wa kusini Pemba kwa wajasiriamali kwa ajili ya uzalishaji katika maeneo mbali mbali jambo ambalo ni faraja kwao.
Alisema atahakikisha anatumia nafasi aliyonayo kwa kubadilisha mkoa wa kusini Pemba ikiwemo kuujenga mji wa Chake chake na kupiga hatuwa kimaendeleo.
Wakichangia katika mkutano hupo wajumbe wa Baraza la wafanyabiashara mkoani humo Mohamed Abdalla Rashid na Abuubakar Mohamed Ali walisema kwa vile Baraza la biashara la mkoa wa kusini Pemba, lengo lake ni kuwawezesha wafanya biashara mbali mbali hivyo ipo haja kuwatembelea wafanyabiashara na wajasiriamali vijijini ili kuona yale wanayofanya kwa vitendo na kuweza kutowa maelekezo yatakayosaidia kupiga hatuwa kimaendeleo.
MWISHO.