Zanzibar :Unaweza kuona mafanikio na kusikia kesi kadhaa za vitendo vya udhalilishaji vikichukuliwa hatua na wahusika kufikishwa katika vyombo vya dola ila bado jamii inawazunguka wahanga wa vitendo vya udhalilishaji wanaliona suala la ushahidi kama kaa la moto hususan linapohusu suala la kifamilia.
Chama cha Waandishi wa Habari wanawake Zanzibar – TAMWA iliadhimisha siku ya mtoto wa kike duniani Oktoba 28, 2023 kwa kuwasilisha Ripoti maalum juu ya ufanisi wa mahakama maalum ya udhalilishaji Kisiwani hapa.
Maadhimisho hayo yaliyofanyika katika Ukumbi Mansoor uliopo,Fuoni Nyumba Moja uliwakutanisha wadau mbalimbali walihudhuria wakiwemo walimu, mahakimu,viongozi wa dini,wadau wa kupinga udhalilishaji pamoja na waandishi wa habari.
Akifungua kikao hicho Asha Abdi ambaye ni Mwenyekiti wa bodi ya Chama cha Waandishi wa Habari wanawake Zanzibar Tamwa ,amesema Umoja wa Mataifa walitangaza kuwepo kwa siku ya mtoto wa kike Disemba 19,2011 siku hiyo ambayo husherehekewa kila ifikapo Oktoba 11 kila mwaka ila dunia hutambua mwezi Oktoba kama mwezi wa kusherehekea na kutambua pamoja na kusaidia changamoto zinawakuta watoto wa kike duniani.
Amesema jamii inawajibu wa kutambua kuwa kuna haja wa kuwasaidia watoto wa kike kujitambua na kuwasaidia kufikia malengo yao “Watoto wakike wajitambue na kila mmoja kwa nafasi yake ajitambue na kuweka malengo ya baadae ili kuweza kukamilisha ndoto zake hio itasaidia kuwa na wanawake wengi wenye maisha yao na wasiotegemezi kwa jamii yenye msaada kwa kizazi kijacho” Amemalizia Asha Abdi.
Kwa mujibu wa sensa ya watu na maakazi ya mwaka 2022, Zanzibar ina ina jumla ya watu 1.8 milioni huku idadi ya watoto wakike ikiwa 447,326 na kati ya hao wanaokaa vijijini ni 239,652 na wale wanaokaa mjini ni 207,674.
Afisa mradi wa kupinga vitendo vya udhalilishaji kutoka Tamwa – Zaina Salum Abdallah amesema kuwa mtoto wa kike ni miongoni wa watoto ambao wanakutana an changamoto nyingi ndio maana taasisi nyingi zinaendelea kuweka juhudi juu ya kutekeleza miradi kadhaa kwenye kumlinda na kumsaidia mtoto wa kike na mwanamke kufikia malengo yao pia kujua suala lao la kupata haki zao na kufikia ndoto zao.
“Kufikia hatua hio ni jambo ambalo tunafanya kutoa elimu juu ya masuala ya udhalilishaji kwenye radio na kuwafundisha masuala ya kuripoti na kuandika habari zinaohusu udhalilishaji waandishi wa habari ili kuweza kuifikisha ujumbe kwa jamii kupitia vyombo vya habari” Amesema Zaina,
Maryam Ame Chum ni Afisa mradi wa wanawake na uongozi kutoka TAMWA – Zanzibar amesema suala la watoto wa kike kuwa viongozi sio jambo ambalo linakuja tu bali ni suala ambalo linaaanzia katika kuaminishwa uwezo wake akiwa nyumbani na kujua haki zake za msingi “Upatikanaji wa haki za kidemokrasia na kumuwezesha mtoto wa kike mapema hutoa nafasi ya kujitambua na kupata nguvu anapokuwa mkubwa kupata nafasi ya kugombea na kushiriki masuala ya uongozi “ Ameendelea kusema kuwa “ Watoto waanze kushirikishwa katika masuala ya maamuzi na kuwapa nafasi ya kuwasikiliza kwenye ngazi ya familia hii pia itatoa nafasi ya watoto kutoa taarifa pale wanapopitia vitendo vya udhalilishaji kwa wazazi wao” Amemaliza Maryma kuzungumza pale alipopewa nafasi hio.
Ripoti hio maalum juu ya ufanisi wa Mahakama maalum ya udhalilishaji inaonesha kwamba June, 2021, Zanzibar ilianzisha Mahakama Maalum zinashughulikia kesi za udhalilishaji na hadi sasa kuna Mahakama 5 zenye Mahakimu 8 wanaoshughulikia kesi za Udhalilishaji na hizo Mahakama 5 ,3 zipo Unguja na 2 zipo Pemba.
Kwa upande wa Unguja Mahakama zinazoshughulika na kesi za udhalilishajiji ni pamoja na Mahakama ya Vuga ambayo ina mahakimu 3,Mahakama ya Mahonda nayo ina hakimu 1,Mahakama ya Mwera ambayo ina mahakimu 2 na huku Kisiwani Pemba ni Mahakama ya ChakeChake ina hakimu 1 na Mahakama ya Wete yenye hakimu 1 pia.
Ripoti hio iliyofanyika kwa mwezi mmoja kuanzia Juni 16,hadi Julai 16,2023 ilizifikia Wilaya 8 na shehia 57 za Unguja na Pemba na kuwahoji jumla ya wazazi wa wahanga 71 pamoja na maofisa 4 wa mahakama maalum na Ofisi mbili za Mwendesha Mashatka za Unguja na Pemba. Jumla madodoso 77 yalijazwa.
Akiwasilisha Ripoti hio Haura Shamte ambaye ni Mwanachama wa Tamwa amesema “Waliohojiwa wengi walisema kuwa walipata ushirikiano mzuri kutoka kwa wasimamizi wa sheria, Polisi, Ofisi ya mwedesha mashtaka DPP na mahakama na hiyo inaonesha kwamba 65% ya wahojiwa walisema kuna ushirikiano mzuri huku 35% walisema hakuna ushirikiano” Alisema Haura.
Haura pia ambaye ni mwanahabari mkongwe visiwani hapa amesema Ofisi kuu ya Mwendesha Mashataka (DPP) Unguja ilijibu dodoso na kusema kuwa kwa kawaida wanapokea wastani wa kesi 70 hadi 100 kutoka ofisi zote za wilaya za Unguja na Pemba kwa mwezi za kesi za udhalilishaji.
Wakichangia juu ya Ripoti hio yenye kurasa 24 wadau wa kupinga vitendo vya udhalilishaji akiwemo Fatma Hamis Ali ambaye ni Msaidizi wa kisheria ni mwanaharakati wa kupinga vitendo vya udhalilishaji amesema kuwa kutokana na ripoti hio inaonesha kwamba bado kuna shida katika jamii ya kushirikiana “Sisi kama wanaharakati tunaenda kwenye jamii kuona kwamba kama vitendo vimetokea familia itoe ushahidi ila baada ya hukumu kutoka mfano baba amefungwa basi hio familia haina tena msaada wa kupata chakula na mahitaji mengineyo hivyo nashauri kwa serikali kuwa na mfuko wa kusaidia hizi familia” Amesema Fatma.
Mwandawa Suleiman Juma ni Mwalimu wa Shule ya Msingi Chukwani akichingua ripoti hio ametoa wito kwa wanawake kuondoka na watoto wao pale wanapoamua kuachika “ Usimuachie jirani ukiachwa ondoka na watoto wako wawe kwenye mikono yako,wawe salama huo ndio wito wangu” Amemalizia Mwandawa .
Mwaka 2022, matukio 1,360 ya udhalilishaji yaliripotiwa, kati ya hayo 534 yapo chini ya upelelezi wa polisi, matukio 2 yapo ofisi ya Mwendesha Mashtaka DPP, matukio 421 Mahakamani, matukio 181 yalihukumiwa, matukio 139 yaliachiwa huru, matukio 19 hayakuwa na mtuhumiwa/hakuna mtuhumiwa aliyepatikana na 64 hakuna hatua iliyochukuliwa.
Sarah Omar Hafidh ni Hakimu wa Mahakama ya Vunga anayeshughulikia masuala ya udhalilishaji amesema “ Jamii ijue na itambue kuwa suala la kutoa hukumu ni suala linalonaendana na sheria na ikiwa kuna hukumu imetolewa basi hiyo inazingatia sheria za nchi.”
Ripoti hio pia imetoa mapendekezo kwa Jamii kuwa inapaswa kuwa karibu na watoto chini ya umri wa miaka 18 ili kuweza kuelewa mapema iwapo kuna jambo lolote baya likiwa limetokea.
Imezishauri pia Azaki kusaidia kuendelea kutoa mafunzo kwa wasimamizi wa sheria na wananchi kwa ujumla huku wakishauri Serikali kuanzisha na kuwezesha matumizi ya ushahidi wa kielektroniki hasa kwa kesi zinazohusu watoto na kusimamia na kupinga masuala ya rushwa kwenye kesi za udhalilishaji.