Friday, November 15

Waalimu kisiwani Pemba wametakiwa kuzitumia fursa   za kujiunga na  Mifuko ya bima

NA AMINA AHMED-PEMBA.

Waalimu Kisiwani Pemba wametakiwa kuzitumia fursa   za kujiunga na  Mifuko ya bima   ili kuweza kuzipatia  ufumbuzi changamoto mbali mbali zinazowakabili katika maisha  ikiwemo, Afya mali, Ajali pamoja na majanga mengine mbali mbali.

Ushauri huo umetolewa na  mkuu wa Wilaya ya Chake chake  Abdalla Rashid Ali alipokuwa akizungumza na waalimu  katika ufunguzi  wa mafunzo maalumu ya utowaji wa elimu ya bima  yalioandaliwa na mamlaka  ya Usimamizi wa Bima Tanzania TIRA kwa  wanachama wa  Saccos ya walimu  Pemba yaliofanyika katika ukumbi wa  Tibirinzi Chake Chake Pemba .
Amesema  kujiunga na Bima mbali mbali ni moja kati ya hakiba zitakazosaidia  kukabiliana na majanga yasioepukika  kwa mtu mmoja mmoja au kikundi na kuweza kupata usaidizi wa kujikimu  pindi yanapotokea.
  Aidha Rashid Ameitaka mamlaka hiyo  kuendelea kuzipatia ufumbuzi changamoto zinazoendelea kulalamikiwa na wanachama wanaojiunga na bima mbali mbali ikiwemo  kucheleweshewa  fidia wanapopatwa na majanga pamoja na kuchelewa kupatiwa bima mpya kwa baadhi ya bima ambazo zimemaliza muda wake.
Naibu kamishna wa Mamlaka hiyo Zanzibar  Khadija Issa Said amewataka   walimu hao  kisiwani Pemba kuanzisha uwakala wa bima katika Taasisi zao Ili kurahisisha kuzipatia ufumbuzi  changamoto hizo kwa urahisi.
Amesema mamlaka hiyo inayotambulika kisheria  itaendelea kuratibu na kusimamia shughuli za bima  bara na visiwani Zanzbar kwa lengo la   kusajili na kusimamia huduma za bima nchini, kutoka kwa kampuni, mashirika na taasisi ili kuona malengo ya kuanzishwa  kwa sekta hizo yanaendelea kufikiwa na kuwanufaisha wanachama wake.
 Akitoa  neno la shukuran kwa niaba ya Walimu kutoka Saccos ya  walimu Pemba Said Suleiman  ameishukuru taasisi hiyo kwa kuwapa elimu  juu ya bima mbali ambazo zitasaidia  kutatua changamoto zinazojitokeza kila siku katika maisha.
Utolewaji wa elimu ya bima kwa Saccos ya walimu Pemba  yameandaliwa na mamlaka hiyo kwa kushirikiana na Taasisi ya Bima ya Jubilee Life Insurance imewashirikisha zaidi ya waalimu 150 ambapo jumla ya mada 3 zimewasilishwa   ikiwemo Bima ya maisha kwa na vikundi, bima ya elimu,  pamoja na bima ya afya.
mwisho .