NA AMINA AHMED -PEMBA.
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar Kupitia Wizara ya Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi imewalipa fidia wananchi 607 ambao waliharibiwa Majengo pamoja na vipando vyao vilivyo takiwa kupisha ujenzi wa barabara kuu ya Wete Chake inayoendelea ujenzi wake Kupitia Kampuni ya Engineering Company Limited (MECCO) yenye urefu wa kilo mita 22. 2 huku wananchi 16 waliobaki wakiendelea na mchakato wa kumaliziwa fidia hizo.
Ameyasema hayo waziri wa Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar Dk Khalid Salum Mohamed alipokuwa akitoa taarifa ya utekelezaji wa programu ya uimarishaji wa usafiri wa barabara kwa kipindi cha Julai hadi September 2023, pamoja na taarifa ya maendeleo ya mradi wa ujenzi wa Bandari ya Shumba Mjini sambamba na utendaji wa Bandari ya Wesha katika kikao maalumu cha kamati ya Mawasiliano Ardhi na nishati ya baraza la wawakilishi Zanzibar kilichofanyika katika ukumbi wa wawakilishi Wete Mkoa wa Kaskazini Pemba.
Amesema jumla ya shilingi 8,645,938,670 zimetumika kwa ajili ya fidia hizo kuanzia Meli 5 hadi Limbani Wilaya ya Wete ambapo wananchi hao 16 waliocheleweshewa ni kutokana na kulazimika kufanyiwa mapitio ya tathimini ya nyumba zao baada ya kubadilika kwa mchoro wa ujenzi wa barabara hiyo katika baadhi ya maeneo na kulazimika kuingia nyumba za wananchi hao 16.
“Mchakato wa tathmini umeshakamilika tayari na maombi kwajili ya malipo yameshafikishwa katika ofisi ya Rais Fedha na mipango tunaamini muda sio mrefu wananchi hao 16 kati yao 10 ni wenye Nyumba, wananchi wawili 2 wamiliki wa Faundation, pamoja na wanne waliosalia ni wamiliki wa vibanda vya biashara wataanza na mchakato wa kulipwa .”
Akitoa taarifa kuhusu mradi wa maendeleo bandari ya Shumba mjini waziri Khalid ameieleza kamati hiyo kuwa wizara inatekeleza ujenzi huo kufuatia agizo la rais wa Zanzibar Dk Hussein Ali Mwinyi alilolitoa mwaka 2021 ambapo kwa sasa hatua mbali mbali za ujenzi wa gati zinaendelea Ambapo jumla ya shilingi 64,790, 000 zimelipwa fidia kwa wananchi wenye mazao pamoja na mimea katika eneo hilo huku tathmini ya ulipwaji wa fidia kwa wananchi wawili 2 ambao ni wamiliki wa vibanda zikiwa katika hatua za mwisho za ulipwaji.
Alieleza kuwa Ujenzi wa gati ya bandari hiyo yenye urefu mita 45 na upana mita 20 ambapo itakapokamilika inatarajiwa kuhudumia meli zenye uzito wa mizigo tani 2,000 itasaidia kuzipatia ufumbuzi changamoto za wafanya biashara wanaoagiza mizigo yao nje ya kisiwa cha Pemba.
Akizungumza mara baada ya taarifa hiyo mweyekiti wa kamati hiyo Yahya Rashid Abdalla ameitaka wizara ya Mawasiliano kuendelea kutoa fursa za ajira zinazopatikana hususan ni kwa wananchi wazawa katika ujenzi wa barabara hizo zinazoendelea kujengwa Unguja na Pemba na kuweza kujipatia kipato.
Aidha akiwa katika eneo la mradi wa maendeleo ya ujenzi wa Bandari ya Shumba Mjini Wilaya ya Micheweni Mwenyekiti wa kamati hiyo ameitaka wizara ya Mawasiliano Pemba kutafuta barabara rasmi itakayotumika kufika katika eneo hilo ili kuepeusha athari zitakazojitokeza baadae katika majumba ya wananchi wa karibu na eneo la bandari hiyo itakapokamlika .
“Wakati tunakuja huku tumepita njia ambayo ni ya asili inayotumika kikawaida na wananchi wa maeneo haya ya Shumba niiase Wizara kutafuta njia rasmi itakayotumika kufika katika eneo hili bila kuwasababishia usmbufu wananchi hapo baadae”.
Kwa upande wake mshauri elekezi wa mradi wa bandari hiyo kutoka kampuni ya Anova Consult Limited Ramadhan Khamis amewaomba wasimamizi wa mradi huo ambao ni wizara ya ya mawasiliano kupitia shirika la bandari ZPC kutohofia kuongezeka kwa gharama za mradi huo kutokana na kupanda kwa dola ulimwenguni .
Ziara ya siku mbili kwa Kamati hiyo ya Mawasiliano, Ardhi na nishati ya baraza la wawakilishi licha ya kusomewa taarifa ya utekelezaji wa programu ya barabara na ujenzi wa mradi wa bandari ya Shumba Mjini na uimarishaji wa bandari ya wesha pia ilitembelea barabara kuu ya Birikau, Kipapo Mgelema, Sambamba na Chake wete.
Mwisho.