Tuesday, November 12

DC chake chake CYD inachochea maendeleo ya nchi

 

NA ABDI SULEIMAN, PEMBA.

MKUU wa Wilaya ya Chake Chake Abdalla Rashid Ali, amesema taasisi ya CYD inachochea maendeleo ya Nchi kupitia Mradi wa Wanawake na Amani, kwani bila ya kuwapatia elimu juu ya umuhimu na utunzaji wa amani mambo mengi yanaweza kukosena.

Alisema wanawake ndio walezi wakubwa wa familia majumbani, hivyo mradi huo umekuja wakati muwafaka kwani unawagusa moja kwa moja wanawake.

Ameyaeleza hayo wakati akizungumza na wadau wa masuala hayo kutoka makundi mbali mbali, ikiwemo watu wa ustawi wa jamii, viongozi wa dini zote mbili, maimamu, Polisi, watu mashuri, hafla iliyoandaliwa na CYD, kufadhiliwa na shirika la WIIS-Kenya kwa kushirikiana na USIP na kufanyika mjini Chake Chake.

Alisema amani inapoharibika watoto na wanawake ndio waathirika wakubwa, hivyo vinapotokea viashiria vya uvunjifu wa amani kila mtu anapaswa kuvikemea kwa nguvu zote.

Aidha aliwataka viongozi wa dini kutumia nafasi yao ili amani iendelea kuwepo, kwani kumekua na migogoro mingi ya ardhi inajitokeza, ikiwemo suala la mirathi, hata kuuziana vizuri kufuata taratibu husika.

“Lazima tuwe kitu kimoja katika suala zima la ulinzi wa maeneo yetu, vijana wetu kutokuruhusu migogoro ya ardhi kutokutokea, nayo pia inasababisha uvunjifu wa amani,”alisema.

 

Naye Afisa Mdhamini Wizara ya Habari Vijana Utamaduni na Michezo Pemba Mfamau Lali Mfamau, alisema kila mtu kwa nafasi yake anapaswa kupigania suala zima la amani, kwani ndio tunu pelekea iliopo kwa wazanzibari.

Mapema mkurugenzi wa CYD Zanzibar Hashim Pondeza, alisema mikakati ya mradi huo ni kuzuwia uhalifu usitokee, ikizingatiwa wanawake ni walinzi wakubwa majumbani.

Alisema lengo la mradi huo ni kutaka kuwashirikisha wanawake juu ya masuala ya amani, ili waweze kufahamu zaidi amani na usalama katika maeneo yao, ili kusaidia kwenye kampeni za kitaifa za kupambana na kupinga matendo yanayoweza kupelekea uvunjifu wa amani ikiwemo udhalilishaji.

“Wanawake wanamchango mkubwa katika kuhakikisha amani inadumu, na wakitaka kuipoteza basi ni mara moja, kwa vile muda mwingi wanakua majumbani hata wageni basi wanawajua wao wanapoingia,”alisema.

Kwa upande wake Mkufunzi wa masuala ya Wanawake na Amani, Mhadhiri kutoka SUZA Dkt.Said Mohd Khamis, alisema amani ni tunu ikitokea kutoweka kuirudisha kwake ni shida, hivyo kila mmoja anapaswa kuwa mzinzi wa amani hiyo kwenye maeneo yake.

Nae afisa vijana Wilaya ya Chake Chake Stara Khamis Juma, alisema suala la kujitoa kwa vijana ni tatizo, vijana waliowengi wanataka urahisi kwa kila kitu, wakati serikali inahimiza vijana kujiajiri wenyewe.

Kwa upande wake Abdullatif Abdalla, alisema wakati umefika kwa kuwapatia fursa za uongozi wanawake, kuingia katika siasa katika chaguzi zinazokuja.

MWISHO