Thursday, November 14

WHVUM inapaswa kusimamia uchezaji wangoma za uchi katika maeneo ya hoteli za kitalii.

 

NA ABDI SULEIMAN, PEMBA

WAJUMBE wa Kamati ya Ustawi wa Jamii ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar, wamesema kuwa Wizara ya Habari Vijana Utamaduni na Michezo Zanzibar, inapaswa kusimamia uchezaji wangoma za uchi katika maeneo ya hoteli za kitalii, ili kunusuru kupotea kwa maadili ya kizanzibari.

Wamesema nchi ina uwekezaji wa hoteli mbali mbali na ngoma nyingi zimekua zikichezwa usiku uchi, jambo ambalo linaleta athari kubwa kwa jamii iliyozungukwa na hoteli hizo na taifa kwa ujumla.

 

Hayo yameelezwa na wajumbe wa kamati hiyo, wakati wakichangia taarifa ya utekelezaji wa bajeti ya baraza la Sanaa, sensa ya filam na utamaduni, kipindi Cha robo ya kwanza kuanzia Julai hadi Septemba 2023, Kwa wajumbe wa kamati hiyo huko katika ukumbi wa wizara ya habari Gombani.

 

Mjumbe wa kamati hiyo Sulubu Kidongo Amour, alisema Zanzibar ni nchi inayoongozwa kwa misingi ya uislamu, lazima kuzingatiwa maadili na silka za kizanzibari katika utekelezaji wa majukumu ya kazi.

 

“Kama tunataka kulifanyia kazi hili lazima wizara tujipange kikweli, kuna baadhi ya matukio hutokea usiku usiku kama lile la kanga moko, hata baadhi ya nyimbo nyengine zinachezwa na zimekatazwa,”alisema.

 

Nae Bihindi Hamad Khamis ambae ni mjumbe wa kamati hizo, alisema vijana wamekua wa hakihadalika na utumiaji wa mitandao ya kijamii, hali inayopelekea kusahau Mila, tamaduni na silka zao .

 

Kwa upande Abdalla Hussein Kombo mjumbe wa kamati hiyo, ameitaka wizara ya habari kupitia baraza la Sanaa sensa na filamu, kuhakikisha wanazichukulia hatua filamu chafu zisizoendana na maadili, silka na tamaduni za kizanzibari.

 

Alisema filamu ambazo hazifai kuoneshwa Zanzibar zinapaswa kukatazwa kabisa, ili kunusuru vizazi vya vijana wakizanzibari,”alisema.

 

Mapema Katibu Mkuu wizara ya habari Vijana utamaduni na Michezo Zanzibar Fatma Hamad Rajab, alisema baraza la Sanaa limefanikiwa kukagua kazi za filam 91 kwa lengo la kulinda Mila, silka na utamaduni wa kizanzibari, huku filamu Tano (5) hazikuruhisiwa kuoneshwa ndhani kutona na kukiuka Mila, silka na utamaduni wa Mzanzibari.

 

Aidha alisema baraza limefanikiwa kuibua vipaji vya Sanaa ya sarakasi, maigizo na ngoma za asili, Sanaa ya sarakasi ilishirikisha skuli nane (8) za msingi Unguja na Pemba, Sanaa ya maigizo skuli mbili na sanaa ya ngoma za asili ni kikundi kimoja kutoka mchangamdogo Pemba.

 

Nae katibu mtendaji baraza la Sanaa sensa na filamu Zanzibar Dr.Omar Abdalla Adamu, alisema zipo filamu ambazo tayari wamezizuia kuonyeshwa Zanzibar, kutokana na kwenda kinyume na maadili ya Kizanzibari pamoja na ngoma zao.

 

“Wapo wasanii pia tuliwazuwia na kuwakataza kurikodi video zao, kutokana na upigaji wa picha zao na nguo zao walizokua wamevaa katika kipindi Cha Ramadhani,”alisema.

 

Katika hatua nyengine Menyekiti wa kamati hiyo Sabiha Filfil Thani, aliwataka watoto walioko kwenye sana kuhakikisha wanaelekeza nguvu zao pia katika suala la elimu, kwani ndio jambo la msingi na muokozi wa maisha yao.

 

MWISHO