Saturday, December 28

Wamiliki wa vyombo vya utangazaji wametakiwa kufuata sheria zilizowekwa na Tume.

KATIBU Mtendaji wa Tume ya Utangazaji, Suleiman Abdulla Salim, amesema wakati umefika kwa wamiliki wa vyombo vya utangazaji kufuata sheria zilizowekwa na Tume sambamba na kuhakikisha wanajisajili ili kufanya kazi zao kwa uadilifu na umakini zaidi ili kuepuka kuchukuliwa hatua za kisheria.

Akizungumza na waandishi wa habari Ofsini kwake Kilimani, Katibu Suleiman alisema ukaguzi wa hivi karibuni uliofanywa na Tume umebaini wapo baadhi ya wamiliki wa vyombo vya habari vya utangazaji wanafanya kazi zao bila ya kufuata sheria na miongozo jambo hilo ni kinyume na matakwa ya serikali.

“Katika tathimini yetu fupi iliyofanywa hivi karibuni tumebaini kuwepo kwa baadhi ya vituo vya utangazaji hasa vya maudhui ya mtandaoni (online tv) zimeanzishwa bila ya kufuata utaratibu hivyo Tume inatoa muda wa wiki mbili kwa wale wenye hizo online waje kuzirasimisha ili wawe salama katika kazi zao”.

Alisema katibu huyo kwa mujibu wa sheria ya tume ya utangazaji. 7 ya mwaka 1997nam Kifungu cha 11 kinapiga marufuku kwa mtu yeyote kurusha au kwa namna yoyote kuendesha huduma za Utangazaji pasi na kua na Leseni inayotambulika.

Katibu Mtendaji alifahamisha kwa kuwa Tume imepewa mamlaka ya kuhakikisha wanasajili watoa huduma za utangazaji Zanzibar ikiwemo Online, Televisheni na
Radio hivyo haitakuwa na muhali kwa kituo chocte cha utaungazaji kitakachobainika kuwa na kosa hilo.

Aidha alisisistiza kuwa tume ya utangazaji Zanzibar inaendelea kufuatalia pia matangazo ya vituo vya utangazaji kwa kutumia mitambo ya kitaalamu kwa ajili ya kuhakikisha habari zinazotolewa zinakuwa ni za ukweli na kulinda maslahi ya taifa na hazimuumizi mwengine endapo zitakapotoka sambamba na kuhakikisha usalama wa nchi unabaki ulivyo na utamaduni wa nchi unalindwa.

Nae, Mrajisi wa Tume hiyo, Mohamed Said Mohamed, alisema Tume itahakikisha wanaendelea kushirkiana na wadau wa sekta ya utangazaji ili kuona wanafanya kazi kwa mujibu wa maombi yao wanayoyafikisha katika Tume kwa mujibu wa sheria na kanuni na miongozo inayoruhusu shughuli za utangazaji Zanzibar.