Thursday, November 14

ZAIDI YA MIFUGO 340 NA TREKA MOJA YAKAMATWA NDANI YA HIFADHI YA TAIFA RUAHA

Na. Jacob Kasiri – Ruaha.
Mifugo ipatayo 345 na Trekta moja imekamatwa ndani ya Hifadhi ya Taifa Ruaha na askari wa hifadhi hiyo waliokuwa doria  wakitekeleza majukumu yao kwa mujibu wa Sheria ya Hifadhi za Taifa  Tanzania Sura ya 282 marejeo ya mwaka 2002.
Swala la uingizwaji wa mifugo na kilimo ndani ya Hifadhi ya Taifa Ruaha limekuwa ni tatizo sugu licha ya wananchi wanaozunguka hifadhi hiyo kupewa elimu inayohusiana na madhara na kadhia inayoweza kulikumba Taifa kutoka na uharibifu wa ardhi Oevu ya Ihefu ambayo ni chanzo cha maji yanakwenda kuzalisha umeme katika mabwawa ya kimkakati nchini.
Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Uhifadhi Godwell Meng’ataki Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Ruaha alisema, mifugo hiyo 345 imekamatwa na askari wakiwa doria tarehe 13 na 14 Novemba, 2023 zaidi ya kilometa 100 ndani ya ardhi Oevu. Wafugaji hao wamebuni mbinu ya kuingiza mifugo usiku wa manane na kuiondoa alfajiri”.
Aidha, “Mnamo tarehe 14.11.2023 askari wetu wa Uhifadhi wakiwa doria pia, walifanikiwa kuwakurupua majangili kadhaa waliokuwa wakilima ndani ya Hifadhi ya Taifa Ruaha kwa kutumia Trekta aina ya Solanika lenye namba za Usajili T.377 EBA kinyume cha Sheria zilizoanzisha Hifadhi za Taifa Tanzania”.
Kamishna Meing’ataki aliongeza kuwa baadhi ya majangili hao walikimbia kusikojulika lakini dereva wa Trekta amekamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria. Pia mifugo hiyo 345 iliyokamatwa na askari hao imefikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Maafisa na askari wa Hifadhi ya Taifa Ruaha wameendelea kukabiliana na vitendo vya ujangili ndani ya bonde la Ihefu ili kuhifadhi vyanzo vya maji kwa ajili ya “The Great Ruaha” na bioanuai zilizomo katika hifadhi hiyo ya pili kwa ukubwa Tanzania kwa ajili ya maendeleo ya utalii na kuongeza pato kwa Taifa.
MWISHO.