Friday, December 27

SMZ yathamini jitihada zinazochukulia na mashirika ya maendeleo UNDP, LSF

NA ABDI SULEIMAN, PEMBA.

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) imesema inathamini jitihada zinazochukuliwa na mashirika mbali mbali ikiwemo LSF na UNDP katika kuunga mkono utoaji wa msaada wa kisheria.

Hayo yameelezwa na Mwanasheria mkuu Zanzibar Dkt.Miwnyi Talib Haji, wakati akifungua jukwaa la tatu la mwaka la msaada wa kisheria 2023, huko katika ukumbi wa chuo cha Utalii Maruhubi.

Alisema jitihada zinazotolewa zimesaidia kuwasogezea wananchi huduma ya msaada wa kisheria, katika maeneo wanayoishi na kuondokana na changamoto zilizokua zikiwakabili.

Akizungumza kwa niamba ya mwanasheria Mkuu, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, Shaaban Ramadhan Abdallah alisema Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, itaendelea kufuata nyayo hizo za kuyathamini mashirika hayo na kuendelea kufungua milango ya kufanya kazi kwa pamoja.

“Mbali na hayo lakini pia nimefarajika kuelezwa kuwa rasimu ya sera ya msaada wa kisheria tayari imepita katika baadhi ya ngazi ikiwemo ya kukusanya maoni ya wahusika Unguja na Pemba,”alisema.

Alifahamisha kwamba matarajio yake baada ya kukamilika kwa sera, hiyo mafanikio mengi yatapatikana ikiwemo kuanzishwa kwa mfuko wa msaada wa kisheria, kupima ubora wa viwango vya utoaji wa msaada wa kisheria na njia madhubuti za ufuatiliaji na tathmini.

Aidha Naibu huyo alieleza kwamba, matarajio mara baada ya kumalizika kwa jukwaa hili, washiriki wataondoka na maazimio yatakayoimarisha masuala ya msaada wa kisheria, hasa katika mwelekeo wa mapito ya sera ya mwaka 2017 na hatimae kupelekea mabadiliko ya sheria ya msada nambari 13 ya mwaka 2018.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Katiba, Sheria,Utumishi na Utawala Bora Mansura Mossi Kassim, alisema kuwepo kwa jukwaa la msaada wa huduma za kisheria kumesaidia kupatikana maendeleo makubwa katika kuwasaidia wananchi.

Alisema kazi inayofanywa na watoa msaada wa kisheria inatambulika na ndio sababu ya kuanzishwa kwa kampeni maalum ya Mama Samia.

“Nawashukuru sana kwa kazi mnayoifanya ya wito na kujitolea katika utekelezaji kwa watu wanyonge na wale ambao hawana elimu ya sheria,”alisema.

Naye Mkurugenzi Idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria Hanifa Ramadhan Said, alisema miongoni jukwaa la pili la msaada wa kisheria limefanikiwa kutekeleza mambo mbali mbali, ikiwemo mahakama kushirikiana na watoa msaada wa kisheria kwa kutoa elimu katika maeneo mbalimbali,kuajiriwa kwa watu wenye mahitaji maalum na kupatikana kwa elimu ya lugha za alama kwa askari polisi

Aidha Mkurugenzi aliyataja malengo ya jukwaa la tatu ni pamoja na kurahishisha upatikanaji wa taarifa sahihi kwenye utoaji wa huduma za msaada wa kisheria,kukuza ubunifu na kuimarisha uwezo wa watoa msaada wa kisheria na kuendeleza majukumu yao ya kazi ya kila siku.

Malengo mengine ni kurahisisha upatikanaji wa taarifa sahihi za huduma wa msaada wa kisheria pamoja na kuwaunganisha watoaji msaada wa kisheria na taasisi nyengine ili kuwezesha kufanya kazi kwa pamoja.

Kauli mbiu ya mwaka huu ni “kuimarisha huduma za msaada wa kisheria zenye ubora na zinazozingatia matokeo”

MWISHO