Monday, November 25

Wananchi watakiwa kuchukua thadhari kwa kusafisha maeneo ya makaazi

NA ABDI SULEIMAN,PEMBA

WANANCHI Kisiwani Pemba wameshauriwa kuendelea kuchukua tahadhari juu ya maradhi ya mripuko, katika kipindi hiki cha mvua zinazoendelea kunyesha nchini.

Ushauri huo umetolewa na viongozi wa Serikali Pemba, wakati walipokua wakizungumza na mwandishi wa habari hizi kwa nyakati tafuti, juu ya hali ya mvua zinazoendelea na suala la maradhi ya mripuko.

Viongozi hao wamesema ili kusitokea maradhi hayo, wananchi wanapaswa kusafisha maeneo yao yaliowazunguruka, kuacha kutupa takataka ovyo katika vyanzo vya maji, pamoja na kusafisha mitaro ya maji taka ili isiweke uchafu.

Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Mattar Zahor Massoud, alisema mpaka sasa ndani ya Mkoa huo, hakuna kesi ya kipindupindu iliyoripotiwa au kutoka kwa maradhi yoyote katika kipindi hiki cha mvua.

Ndugu zanguni suala la kusafisha mitaro ni muhimu, wakati wote inatakiwa kuwa safi kwa sababu inatiririsha maji, tuendelee kuhamaisha wananchi kutokuweka mataka,”alisema.

Alisema ni wakati sasa kwa wananchi kuchukua tahadhari kikamilifu, kwa kuchemsha maji ya kunywa, kunawa mikono kwa sabuni kila wakati, pamoja na kuweka usafi mazingira ya majumbani mwao.

Akizungumzia suala la Vyoo, Mkuu huyo aliwataka wananchi safisha vyoo vilivyojaa, ili kudhibiti uchafu kuenea katika mitaro ya maji, ikizingatiwa watoto ndio wamaocheza muda mwingi.

Hata hivyo aliwataka wananchi kuhakikisha wanatumia vyoo wakati wa kwenda haja zao, ili kuimarisha usalama wa wananchi katika maeneo yao.

Mkuu wa Wilaya ya Michweni Mgeni Khatib Yahya, aliwataka wananchi kuendelea kuchukua tahadhali kwa kuweka safi maeneo yao, ili kuepukana na maradhi ya mripuko hususana kipindupindu katika kipindi hiki cha mvua zinazoendelea kunyesha.

Alisema tayari wilaya imeshaanza kutoa elimu katika maeneo mbali mbali ambayo wanahisi uwepo wa viashiria vya kutokea maradhi hayo, kwa kuwashauri wananchi kuchemsha maji ya kunywa, pamoja na kutumia sabuni wakati wanapotoka chooni.

“Kama Wilaya tumeanza mkakati wakupita nyumba kwa nyumba kutoa elimu, pamoja na kuwashajihisha wananchi kuweka mazingira safi katika nyumba zao, zaidi katika yale maeneo ambayo huwa yanatokea maradhi hayo mara kwa mara,”alisema.

Alisema maafisa Afiya wa Wilaya na Radio jamii Michweni katika kutoa elimu kwa wananchi, zaidi kipindi hiki cha mvua kwa kuchukua thadhari ya kukabiliana na maradhi ya mripuko.

Nae Mratib wa kamisheni ya kukabiliana na maafa Pemba Khamis Arazak, alisema kamisheni tayari imeshajipanga kikamilifu katika kukabiliana na athari zozote zitazotokea, ikiwemo maradhi ya mripuko.

Alisema kwa kushirikiana na kamati za maafa za wilaya, tayari wameshatenga mapka sehemu za dharura kwa kuwaweka weagonjwa watakaotokea, huku akisisitiza suala zima la usafi kwa wananchi katika nyumba zao.

“Sisi tupo tayari kwa kushirikisha na wadau wenzetu wakiwemo watu wa Wizara ya Afya, lengo ni kuhakikisha wananchi wanakua salama katika kipindi chote cha mvua.

Kwa upande wake Mkuu wa Idara ya Kinga na Elimu ya Afya Pemba Msanif Othaman, alisema wizara imejiandaa katika suala zima la kinga na tahadhari, kwa kutoa elimu elimu ya afya katika maeneo mbali mbali juu ya hali ya mvua na watu kuweza kujikinga nayo.

Hata hivyo aliwataka wananchi kuendelea kuchukua tadhari zote katika kipindi cha mvua, ikiwemo wafanya biashara wa vyakula pamoja na vinywaji.

MWISHO