Sunday, November 24

WAZIRI DK. KHALID AIKABIDHI MAJUKUMU BODI MPYA YA SHIRIKA LA MAWASILIANO ZANZIBAR

Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeweka mkazo katika kuimarisha sekta ya mawasiliano ili kwenda sambamba na mabadiliko ya kiulimwengu.

Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Dk. Khalid Salum Mohamed ameeleza hayo katika hafla maalum ya uzinduzi wa bodi mpya ya shirika la Mawasiliano Zanzibar iliofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Wizara ya Ujenzi Kisauni.

Waziri Dk. Khalid amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imeweka kipaumbele maalum katika kuimarisha huduma sahihi za teknolojia ya habari na  mawasiliano kwa lengo la kuwajengea uwezo watu wake.

Mhe. Waziri ameeleza kwamba bodi hiyo iliochaguliwa itakua na jukumu kubwa la kusimamia sera za ICT, pamoja na kusimamia miundombinu, bajeti na matumizi ya Shirika katika kuhakikisha malengo ya Serikali yanafikiwa.

Pia, Mhe. Waziri amesema Serikali imeona ipo haja ya kuanzisha Shirika hilo ili kutoa nguvu zaidi liweze kujiendesha kibiashara na kuongeza faida.

Nae, Mwenyekiti mteule wa bodi ya Shirika la Mawasiliano Zanzibar Dk. Mahmoud Abdulwahab Alawi amemshkuru Mhe. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa kumuamini na ameahidi kuwa atahakikisha shirika hilo linafikia malengo na madhumuni ya kuanzishwa kwake katika ukuaji na kujiendesha kwa kujitegemea.

Aidha, Dk. Mahmoud amewaomba wajumbe wa bodi hiyo pamoja na wafanyakazi kutoa ushirikiano wao hasa katika utendaji wa kazi zao za kila siku ili kufikia lengo la kutoa huduma bora za mawasiliano.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Mawasiliano Zanzibar Ndugu Shukuru Awadhi Suleiman ametoa pongezi zake kwa Serikali na uongozi wa Wizara ya Ujenzi kwa kuwateua wajumbe wa bodi.

Amesema kuteuliwa kwa bodi hiyo kutasaidia kutoa msukumo katika utekelezaji wa miradi mbali mbali ya Shirika hilo ambayo kwa sasa ipo katika mchakato wa utekelezaji.

Wajumbe wa bodi hiyo wameteuliwa kwa mujibu wa sheria nambari nne  ya mwaka 2023 na inajumuisha:

Mahmoud Abdulwahab Alawi – Mwenyekiti
Said Seif Said – Mjumbe
Mohamed Khamis Mussa (Baucha) – Mjumbe
Abdulrahaman Ali Hassan (Bagash) – Mjumbe
John Mahundi – Mjumbe
Chai Ali Mohamed – Mjumbe na
Mhandisi Shukuru Awadhi Suleiman – Mjumbe

Imetolewa na Kitengo cha Habari (WUMU)