NA AMINA AHMED-PEMBA.
UHABA wa wafanya kazi ni miongoni mwa changamoto kubwa inayovikabili vituo vya mkono kwa mkono kisiwani Pemba jambo ambalo hupelekea kupungua kwa ufanisi wa vituo hivyo ambavyo kazi yake kubwa ni kusaidia kwa kiasi kikubwa mapambano dhidi ya vitendo vya udhalilishaji kwa watoto na wanawake katika kusaidia kupatikana kwa ushahidi wa moja kwa moja.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti baadhi ya wadau wa kupambana na vitendo vya udhalilishaji kisiwani Pemba wamesema miongoni mwa changamoto walizozibaini ni kutokuwepo kwa idadi kubwa ya watendaji katika vituo hivyo jambo ambalo hupelekea kurudisha nyuma mapambano dhidi vitendo hivyo.
Fat hiya Mussa Said Mratibu wa Tamwa Zanzibar kwa upande wa kisiwani Pemba alisema kuwa huenda hakuna usimamizi wa vituo vya mkono kwa mkono jambo ambalo hupelekea kupungua kasi ya ufanisi katika vituo hivyo.
“Tulio wengi katika taasisi tumezoea kusimamiwa ndio tutende kazi ipasavyo inapotokea hatukusimamiwa hatutowajibika tutaendelea kufanya kazi tu kwa mazoea bila kujua kwamba tunapunguza ufanisi uliokusudiwa” Amesema Fat-hiya.
amesema kama watendaji tunatakiwa tubadilike na sio kusubiri kiongozi atusimamie ndio tutende jambo kama lilivyo bila kulipindisha .
Hata hivyo amesema tufanye kazi kilillahi taala kwa sababu majanga haya ya udhalilishaji leo yanamtokea mwezako kesho linaweza kumtokea mtu ndani ya familia yako kama likienda lisivyoeleweka kwa uzembe tu wa watendaji kama halitoleta madhara zaidi.
” Ili serikali ipate sifa nzuri katika kupambana na vitendo vya udhalilishaji ni kuongezeka kwa utendaji kazi kwa vituo hivi katika kusaidia mapambano hayo “. amesema
Aidha Tatu Abdalla Msellem Mkurugenzi mtendaji wa taasisi ya Tumaini Jipya Pemba ni miongoni mwa wadau waliozungumza na habari hizi kuhusu ufanisi wa vituo vya mkono kwa mkono katika kupambana na vitendo vya udhalilishaji.
Alisema kuwa lengo la serikali kuanzisha kwa vituo hivyo vya mkono kwa mkono kulitokana na malalamiko ya wananchi baada ya kubaini kuwepo kwa urasimu katika kesi za udhalilishaji .
“Urasimu ulikuwa ni mkubwa zinapotokea kesi za udhalilishaji, mtu ilikuwa mara aende kwa sheha, mara Polisi, mara kwa dakatari kwa hiyo ikaamulika na kuonekana ni vyema kuanzishwa ka vituo hivyo vya Mkono kwa Mkono ili kuweza kutolewa huduma zote kwa wakati mmoja, lakini bado mpaka sasa wapo baadhi ya watu wanapopata kadhia hii ya udhalilishaji ema mtoto kubakwa au kulawitiwa huanzia polisi na wengine kwa sheha “
“Nikiwa kama mdau wa kupinga udhalilishaji bado naona Kuna asilimia 50 kwa 50 katika ufanisi wa vituo hivi na sababu ya kusema hivyo kwanza vituo hivi havifanyi kazi masaa 24 kama ambavyo vinatakiwa iyo nadharia ya kufanya kazi kasaa 24 ni ya maneno tu”.
“Ukienda wanasema wanafanya kazi masaa 24 lakini uhalisia haipo ivo ukweli ni kwamba kuna watu sio wawili watatu wala wanne wameshaleta malalamiko wakienda katika vituo usiku kesi zinpotokea hawapo watendaji mpka wapigiwe simu ndio watoke majumbani waje suali jee ikitokea mtendaji hapatikani!
Alisema Tatu Abdalla Msellem.
“Serikali inaanzisha vitu kwa malengo mazuri lakini changamoto ni kuviendeleza kuna tatizo kubwa katika kuendeleza mambo mbali yanayoanzishwa vinaishia kuwepo jina tu lakini malengo yote yaliokusudiwa hayatekelezwi ipasavyo” .
SHIRIKA LA MSAADA WA KISHERIA .
Ili mahkama iweze kuthibitisha na kutoa hukumu ni lazima muhanga awe amepita kituo cha mkono kwa mkono na aweze kuthibitika kama amefnyiwa tukio la udhalilishaji, kwa sababu hapo ndipo itakapopelekwa PF3 kwajili ya kufanyiwa vipimo mtoto, na hapo ndipo inapojazwa na kuonekana kweli kama limefanyiwa tukio la ubakaji au kadhia yeyote, lakini ufanisi wa vituo hivi haswa kwa hapa kisiwani Pemba naweza kusema bado ni mdogo kwa asilimia 30 naweza kusema “.
Sababu hivi vituo vinatakiwa viweze kufanya kazi kwa masaa 24 na wakati wa kufanya hiyo kazi watendaji wote wanatakiwa wawepo yaani wawepo Madaktari, Mtu wa Usatawi au mshauri nasihi, Afisa Polisi pia lakini mtoto anafikwa na kadhia usiku wa saa 2 au 3 tunakwenda kituo kimefungwa”.
“Mara nyengine madakatari wanapigiwa wanatoa sababu hawana usafiri mara niko mbali, simu mara haipatikani inakuwa ni usumbufu kufika inabidi huduma zisite mpka asubuhi kwahiyo zile Particula ambazo zinatakiwa zipatikane red hended yaani kwa muda ule ule ambao tukio lile lilipotokezea zinakosekana, Daktari hayupo, au anakuja asubuhi kwa muda ule tukio limeshatokezea labda limetokea mchana wake ushahidi hautopatikana kutokana na kuondoka kwa mazingira kama hayo ambayo yanatokana na kutokufanya kazi masaa 24 kwa hivi vituo vya mkono kwa mkono. “
“Ufanisi huo mdogo unapelekea hata baadhi ya kesi kukosa mashiko, na ule uthibiti zaidi ambao utaweza kumuonesha kwamba huyu mtoto ameathirika, au amefanyiwa tendo la kubaka ama hakufanyiwa tendo la kubaka na kukosekana kwa haki”
” Inavyotakiwa haswa kitengo cha mkono kwa mkono kwanza kiwe na madaktari maalum ambao watakuwa ni mahsusi kupokea wahanga wa vitendo vya udhalilishaji na kuwapatia huduma zinazotakikana pale, lakini uhalisia Daktari anaenda kuchukuliwa Odini, au OPD kule akija muhanga ndio anaenda kuchukuliwa kumuhudumia mtoto au muhanga wa udhalilishaji”.
“Utamkuta daktari huyo huyo aliesaini kwa kazi hii maalum lakini pia anafanya shughuli nyengine katika wodi kwahiyo ule ubora wao unaweza ukashuka kwa sababu huu uchunguzi wa masuala haya yanahitaji kufanyika kwa hali ya uangalifu zaidi “. Ni Maneno ya Siti Habib Muhammed wakili wa kujitegemea kesi za udhalilishaji ambae pia ni mratibu wa Shirika la msaada wa kisheria Pemba.
WIZARA YA MAENDELEO YA JAMII JINSIA WAZEE NA WATOTO
Omar Muhammed Ali ni mkuu wa idara ya wazee na ustawi wa jamii Pemba amesema kuwa mara nyingi waathirika wa vitendo vya udhalilishaji wanapotokewa na vitendo hivyo pamoja na mambo mengine wanahitaji wataalamu wa kuweza kusimamia ili kujua hatua gani wanaweza kuzipita ili kuweza kupata haki katika vyombo vya sheria.
” Siwezi nikavisemea sana hivi vituo vya mkono kwa mkono kwa sababu kwa sasa havisimamiwi tena na wizara yetu kama ilivyokuwa awali vipo wizara ya afya, lakini kiukweli kumekuwa na changamoto ambazo wananchi wanakuja kuziripoti hapa wizarani kwetu kuhusu hivi Vituo kwanza vituo vinafanya kazi kwa masaa 9 tu ule mda wa kuondoka kazini tu”.
“Afadhali mkono kwa mkono Chake chake baadhi ya siku wanajivuta unaweza ukaenda saa 2 za usik ijapo mtoa huduma mmoja yupo lakini humo katika wilaya nyengine hamna utaratibu huo kabisa ” .
Haileti picha nzuri kutokukamilika kwa ule msururu labda daktari yupo mtu wa ushairi hayupo au polisi mpaka atafutwe kutokana na kutokuwepo kwa sehemu yake sehemu rasmi ya kutoa huduma kwa wahanga ikiwa ni ushauri nasaha au kufuatilia kwa waathirika wa hivi vitendo.
Kwa wakati kama ule tunaona watu wengi akili zinakuwa hazipo sawa jee wakipata mawazo mabaya wakahisi labda ni usumbufu wakaamua kujitenga kujinyonga na kujidhuru nani alaumiwe kwa sababu pale akili kila mtu anajua inakuwa haipo sawa. .
WANAJAMII WASEMAJE!
Usumbufu unaweza ukaenda usimkute daktari, au usimkute mshauri na kituo kinafanya kazi mara unaambiwa uje asubuhi, ukiritimba kama huo lazima mtu atasita kuenda pale, kama kurudi nyumbani atarudi aendelee na shughuli nyengine kujisafisha na nyenginezo” Safia Muhammed Ali wanajamii.
Ushahidi unapotea kwa sababu mbali mbali kwanza mimi naona baadhi ya hao watendaji wa mkono kwa mkono naona hawana mashirikiano yaani ile mkono kwa mkono iliyokusudiwa asa haipo ni umbali kwa umbali sikuizi ni majengo tu” Abdalla Said Hamad.
Sijui lakini hii mkono kwa mkono asa mimi naona bado jamii haijui dhamira na malengo yake katika kupambana na vitendo hivi wengine wanauelewa wengine hawana asa na ndio mana wengine wanafika siku 3 au nne hawajaenda hata kutoa taarifa ipo haja kutoa elimu kwa jamii juu ya hivi vituo kazi yake.
OFISI YA MKURUGENZI WA MASHTAKA
Seif Muhammed Khamis ni kaimu mwanasheria dhamana ofisi ya mkurugenzi wa mashtaka Pemba anasema kuwa athari kubwa endapo ufanisi wa vituo vya mkono kwa mkono hautokuwa madhubuti juu ya kusimamia kesi hizi za udhalilishaji hupelekea kuachiliwa huru kwa washtakiwa baada ya kuachiwa kuongezeka kwa vitendo hivyo .
Ili ushahidi juu ya kesi hizi uweze kuwa na mashiko kwanza ni kuaminika kwa shahidi, tunaangalia kuanzia mwanzo huku kesi ilivyoanza jee imepita mkono kwa mkono , taarifa za muathiriwa yaani kibali kutoka kwa daktari PF3 jee imejazwa kitaalamu na mengine ambayo yote hayo huwezi kuyapata kama hujaenda mkono kwa mkono.
“Mifumo ya utoaji haki inahitaji uthibitisho makini katika kutoa maamuzi uthibitisho lege lege tu mara nyingi unakuwa na mashaka na wakati mwengine hupelekea hata kuondoshwa mahakamani, iwapo msururu wa ushahidi hautokuwa na mashaka basi haki itaweza kutolewa kama ilivyo na kesi hizi zinahitaji zaidi ushahidi wa kitaalamu kwa madaktari na wengine”.
“Matukio ya ubakaji unaweza ukamkuta mtu pengine amebakwa, amepata athari ya kimajeraha, vidonda, wengine wanapata maradhi yakuambukiza, hata kisaikologia pia mtu anaweza kupata athari kwaio hayo yote vipi yataweza kuthibiti kama ushahidi mahakamani ni lazima muathirika awe amepita mkono kwa mkono kwa wakati “
VITUO VYA MKONO KWA MKONO WANASEMAJE.
Tunakuwepo masaa 24 , tunakuwepo siku za mapumziko pia ila kutokana na kuwa tuna upungufu wa watendaji kidogo tunalazimika kutofikisha hayo masaa 24, na ikitokea kesi usiku basi tunapigiwa simu tunakuja lakini hapa kituoni tunaweza tukakaa mpka saa 11 au saa 12 “.
” Ufanisi upo vizuri kwa sababu kesi zinakuja, mwanzoni zilikuwa hazifiki kwa wakati lakini kwa sasa watu wanafika ndani ya wakati, na hii imetokana na faida ambazo tunawaelezea , dawa matibabu, ushahidi unaweza kuchukuliwa kwa hiyo huo ni miongoni mwa ufanisi wa hivi vituo”.
“Changamoto kubwa ni kwamba lazima tufanye kazi na watu wa ustawi wa jamii, lakini kiukweli hao watu wapo mbali, inakuwa usumbufu kwa wahanga wanapokuja kuwapeleka katika kitengo chao” .
“Huduma zinapatikana endapo mteja kafika Polisi mtu wa ushauri na daktari ni lazima anakuwepo, isipokuwa kuna upungufu wa wafanya kazi ndio tunakuwa tunaondoka lakini linapotokea tunapata simu tunarudi”.
” Ni lazima tunafika tukipigiwa tu simu hatujali kama ni usiku wala nini tunakuja tunamuhudumia ipasavyo, tunakuja kuchukuliwa na usafiri.
Aidha anasema kuwa kuchelewa kwa kesi kuripotiwa katika kituo hicho ni kutokana na baadhi ya wanajamii kukosa uelewa juu ya kazi za kituo hicho, wanapopata majanga yeyote ya udhalilishaji wapi anatakiwa kufika kwa hatua za awali wapo wanaokwenda kwa sheha, suluhu na sababu nyengine mbali mbali.
Kwa mujibu wa Afisa huyo Kituo cha mkono kwa mkono kinaweza kupokea Jumla ya wahanga 4 kwa siku sawa na wahanga 120 kwa mwezi ambapo idadi hiyo hupungua kutokana na baadhi ya siku kutopokea wahanga au kutokufikia watu wanne kamili. .
WADAU WANA WITO GANI
Kwanza naiomba serikali iendelee kuwaajiri hawa watabibu wakiwemo madaktari ambao watakuwa ni maalum watakaosimamia katika hichi kitengo cha mkono kwa mkono” Tatu Abdalla Msellem anaiomba Serikali
“Serikali kulitilia mkazo hili suala la watendaji hawa wa kitengo cha mkono kwa mkono kuwepo katika vituo vya kazi masaa yote 24 ili muhanga atakapofika kazini aweze kupata huduma kwa wakati” ni ushauri kutoka kwa Siti Habibu Muhamed
“Wizara yetu ya maendeleo ya jamii tuijaribu kukaa na wenzetu wa wizara ya afya kuzungumza nalo suala hilo la kutokufanya kazi kwa masaa yote wamelipokea na wameahidi kubadilika kwaio tunasubiri mrejesho kutoka kwa wananchi, sote tunajenga nyumba moja tunaahidi kuwasaidia juu ya hili” Aliongeza mkuu kutoka wizara ya Ustawi.
Tunaiomba serikali kutuongezea pia watu wa ustawi wa jamii katika hivi vituo pia yaani wasiwepo mbali na sisi ili tupate mashirikiano ya karibu hii itasaidia kuondoa ule usumbufu wa kuwa mtu ashapata matatizo, ashahangaika kuja halafu tunamuongeza nenda rudi kuwafuata maafisa ustawi.
Pia watendaji waongezeke serikali ione kuwa hili ni tatizo ili kuondoa ule usumbufu na kuongeza ufanisi zaidi.Alisema Asha Masoud Salim Mshauri nasaha kutoka kituo cha mkono kwa mkono Chake Chake Hospital.
Mwisho.