Friday, December 27

Zanzibar imekuwa mfano bora utoaji huduma za msaada wa kisheria-LSF.

 NA ABDI SULEIMAN, PEMBA.

MWAKILISHI kutoka taasisi ya LSF Tanzania Wakili Alphonce Guru, amesema Zanzibar imejidhihirisha kuwa mfano bora, kwa utoaji wa huduma za msaada wa kisheria, sio ndani tu hata nje ya Tanzania na Afrika Mashariki.

Wakili huyo alisema, hilo lilijihidhirisha Agosti 8 Mwaka huu, katika mkutano mkubwa uliowashirikisha wadau kutoka Serikalini na watoa msaada wa kisheri kutoka Zanzibar na nje ya Tanzania, ulionesha wazi jinsi gani Zanzibar imepiga hatua katika utoaji wa huduma hiyo.

Aliyasema hayo wakati akitoa salamu za taasisi ya LSF, katika Jukwaa la Tatu la Mwaka la Msaada wa Kisheria Zanzibar 2023, lililoandaliwa na idara ya katiba na msaada wakisheria Zanzibar kwa Ufadhili wa LSF NA UNDP, nakufanyika katika chuo cha Utalii Maruhubi Unguja.

Alisema katika mkutano huo waliweza kufanya ushawishi kwa washiriki kutoka Uganda, Burundi, Kenya na Ruwanda, kuja kujifunza Zanzibar kwenye masuala ya utoaji wa huduma za msaada wa kisheria.

“Wenzetu kutoka mataifa hayo waliona jinsi gani, Zanzibar imekua mfano wa kuigwa na kupata vitu vya kwenda kufanyia kazi kwao, kutokana na umuhimu na dhamira za kweli kwa idara ya katiba na watoaji msaada wakisheria,”alisema.

Aidha alifahamisha kwamba, kufanyika kwa jukwaa hilo ni fursa adhimu kwa wadau wa msaada wa kisheria, tayari maendeleo mbali mbali yamepatikana kwa watoa msaada wa kisheria nchini.

Hata hivyo wakili Guru aliishukuru idara ya Katiba na Msaada wa Kisheria Zanzibar, kwa kauli Mbiu yake “kuimarisha huduma za Msaada wakisheria zenye ubora na zinazozingatia matokeo” kwani imekuja kwa wakati na LSF imekua ikiwekeza kwa miaka mingi, katika suala la utoaji wa huduma za msaada wakisheria.

“Maendeleo ya msaada wa kisheria yanongozwa kwa mfumo madhubuti na maamuzi yanafanywa kwa kuzingatia taarifa bora, zinazokusanywa kutoka kwa watoa huduma”alisema.

Mapema Mkurugenzi wa Idara ya Katiba na Msaada wa kisheria Zanzibar Hanifa Ramadhani Saidi, alisema watoaji wa msaada wa kisheria wamekua wakifanya kazi kubwa ya kutoa msaada wa kisheria, ambapo katika kuziboresha kazi hizo, lazima ziwe zinatoa matokea yake na yanaonekana.

Akiwasilisha malengo makuu ya Jukwaa la tatu, aliserma ni kuimarisha ufanisi na weledi wa utendeaji wa majukumu kwa watoaji msaada wa kisheria, kuwezesha upatikanaji wa sera na sheria mpya zinazokidhi mahitaji ya jamii, katika upatikanaji wa huduma za kisheria.

Aidha malengo mengine ni kurahisisha upatikanaji wa taarifa sahihi katika utoaji wa huduma za msaada wa kisheria, kukuza ubunifu na kuimarisha uwezo kwa watoaji wa msaada wa kisheria katika kuendeleza majukumu yao ya kazi ya kila siku, pamoja na kuwaunganisha watoaji msaada wa kisheria na taasisi nyengine ili kuwezesha kufanya kazi kwa pamoja.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Usajili wa shuduma za sheria, kutoka Wizara ya Katiba na Sheria ya Jamhuri ya Mkuu ngano wa Tanzania, Wakili wa Serikali Edith Shekidele, aliipongeza Ofisi ya Rais Katiba Sheria, Utumishi na Utawala Bora, kwa kuandaa jukwaa hilo kwani wataweza kupata uzoefu katika suala la utoaji wa huduma za msaada wakisheri.

Alisema kwa sasa wanaendelea na kampeni ya Mama Samia ya msaada wa kisheria na tayari wameshatoa katika mikoa mitano ya Tanzania Bara.

MWISHO