Saturday, December 21

MAKALA: Ramia, mwanamke aliepambania kujengwa barabara ya Sebuwatu, lengo lake ijegwe kwa kiwango cha lami

 

NA ZUHURA JUMA, PEMBA 

Kwa watu wa Sebuwatu, kati ya kijiji chao na mji wa Wete Pemba, ni mafupi sana… karibu kilomita tatu.

Lakini muda ulikuwa unachukua muda mrefu kwa aliyetaka kwenda huko au kurudi kijini kutoka mji wa Wete.

Kuifanya safari hio kwa miguu au gari la ng’ombe ni kazi pevu, yenye sulubu na huwa ngumu zaidi kwa mtu aliyebeba mzigo kichwani au mkononi.

Kwa aina wajawazito ndio hatari kabisa, hiyo inatokana na njia kuwa mbaya sana na zaidi wakati wa mvua.

Kila kukicha wanakijiji walikuwa wanajiuliza shida hii walioishuhudia tokea wakiwa wadogo itakwisha lini na wao kuwa na usafiri mzuri, wa haraka na salama kama wanavijiji wengine wa kisiwa cha Pemba?

Tunaambiwa baada ya dhiki faraja na sasa matatizo waliokuwa nayo wanakijiji cha Sebuwatu yameondoka na kuwa sehemu ya historia ya eneo lao.

Katika kila jambo, liwe zuri au baya, basi huwepo mkono wa mtu uliohusika zaidi na katika kuwaondolea hawa wanavijiji.

Na mtu aliyesaidia sana kufanikisha kuondoa tatizo hilo ni mwana mama kiongozi, sheha wa Bopwe, Ramia Said Rashid.

Mwana mama huyo, mara baada ya kushika hatamu ya uongozi wa shehia, aliweka nia ya kulimaliza tatizo hilo na juhudi zake za kupatikana njia nzuri zimethibitisha ule msemo wa penye nia pana njia.

Walikuwa wanatumia muda mwingi kwa usafiri hadi kufikia mjini wanapofanyia harakati zao za kila siku.

Barabara hiyo zamani ilikuwa ya dongo na sasa imesawazishwa vizuri na kuwekewa fusi, hatua iliyoweza kurahisisha usafiri kutoka kijijini kwenda Wete mjini.

Ambapo usumbufu wa usafiri kwa watu wa eneo hilo sasa umeanza kuondoka.

‘’Nashukuru kwa hapa tulipofika na hatua inayofuata ni kuhangaika kutaka itandikwe lami, ili iwe njia bora zaidi,’’ anasema.

Mafanikio haya ambayo kwa wanavijiji wa Sebuwatu ni hatua kubwa ya maendeleo yanatokana na uongozi mzuri wa sheha huyo.

Juhudi alizofanya ni pamoja na kumueleza mwakilishi wa jimbo la Gando Maryam Thani, kuwa katika shehia yake changamoto ilikuwa ni njia hiyo kuwa nyembemba, yenye mashimo na haipitiki siku za mvua.

Hata chombo cha maringi mawili ilikuwa shida kupita na labda unaweza kusema waliofurahia kupita wakati wa mvua ni bata.

Mbali ya kumshawishi mwakilishi kuhangaikia njia hio, pia aliwashirikisha wananchi katika mradi huo.

Matengenezo ya njia hio yaligharimu shilingi milioni 9,360,000, fedha ambazo zilitoka kwenye mfuko wa maendeleo wa jimbo.

Kadhia kubwa zaidi ya barabara hiyo ilikuwa inawakabili watoto wanaokwenda skuli na akinamama, hasa wajawazito na wafanyabiashara.

Wakati wa mvua ilihitaji ukakamvu na ustadi mkubwa kupita kwa miguu kwa kuchelea kuteleza na kuanguka.

Ilikuwa ni barabara yenye mtihani mkubwa kwa wakubwa na wadogo.

‘’Siku za mvua ilikuwa haipitiki kutokana na udongo wake wa kutengenezea vijungu na mikungu kuwa, ni wenye utelezi, watu walikuwa wanaanguka mara kwa mara,’’ anasema.

Ubaya wa barabara uliwapa shida wananchi ambao husafirisha bidhaa zao kati ya kijiji hicho na mji wa Wete kwa miguu na hii kuwaathiri sana kiuchumi.

Mwana mama huyo anasema, lengo lake kubwa baada ya kuteuliwa kuwa sheha, lilikuwa ni kuitumikia jamii kwa uadilifu bila kubagua rangi, wala jinsia na anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kumsaidia kuifanya kazi hiyo.

Uongozi wake mzuri umewavutia wananchi katika shehia yake na kuwa mfano wa uongozi bora katika jamii ambayo anashirikiana nayo katika masuala mbali mbali.

‘’Jambo lolote ikiwa utawashirikisha wanajamii, basi halikupi shida na ndio maana shehia yetu inapata mafanikio na maendeleo,’’ anaeleza.

Chini ya uongozi wake watu wa shehia hiyo wanashirikiana katika shughuli za usafi, kazi za kijamii, michezo na mambo mengine yanayowaletea maslahi yao na taifa kwa ujumla.

Mama huyo haonyeshi ajizi ya kukutana na wananchi kujua kero zinazowakabili na kusaidia kupata ufumbuzi, ambapo anafanya hivyo kila Jjumaa jioni.

Changamoto inayomkwaza ni kwa baadhi ya wananchi kutokuhudhuria mikutano, jambo ambalo linapunguza kasi ya maendeleo.

‘’Mara nyingi wananchi  wasiohudhuria vikao na mikutano ndio walalamikaji wakubwa, hivyo nawaomba nitakapowaita waje ili tuibue kwa pamoja changamoto zetu na kuzipatia ufumbuzi,’’anaeleza.

Ramia anasema, uongozi upo kwenye damu yake na ndio maana tangu zamani aliamua kujiingiza kwenye siasa.

‘’Kama nisingeteuliwa hii nafasi ya usheha basi naamini kuna siku ningegombea nafasi za uongozi majimboni, kwa sababu tangu zamani natamani niwe kiongozi ili nisaidie wananchi,’’ anahadithia.

Sheha huyu alizaliwa Juni 8, 1972 katika kijiji cha Kikunguni Shumba Vyamboni Wilaya ya Micheweni na amepata elimu mpaka kidato cha nne.

Alisoma skuli ya msingi Jadida na kumalizia skuli ya Sekondari Utaani mwaka 1989, aliolewa 1992 na kubahatika kupata watoto watatu, wanaume wawili na mwanamke mmoja.

SERIKALI YA WILAYA  

Dk. Hamad Omar Bakari ambae ni Mkuu wa Wilaya ya Wete anamuezea Ramia kuwa ni kiongozi jasiri, mwenye uthubutu na uwezo katika kuongoza sehemu yeyote atakayowekwa.

Anasema, huyu mama ni mmoja kati ya masheha wanawake anayefanya kazi vizuri ya kuitumikia jamii, kusikiliza kero zao na kuzifikisha sehemu husika ili kutatuliwa.

“Inapoibuliwa changamoto kwenye shehia ni lazima zifike kwenye Wilaya na hapo ndio tunatafuta njia ya kuzitatua kulingana na uwezo wetu na ikiwa ni kubwa tunalifikisha sehemu husika,” anafafanua.

WIZARA YA MAWASILIANO

Afisa Mdhamini wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Pemba, Ibrahim Saleh Juma anasema, barabara hiyo imejengwa na wananchi wenyewe bila ya Wizara kupewa taarifa yeyote.

‘’Bado barabara hiyo hawajaiweka kwenye mpango wao wa ujenzi na wala hatujapata maombi ya ujenzi, lakini kwa sasa zipo barabara nyingi kwenye mpango wa ujenzi,’’ anafahamisha.

Anasema, watafaya ukaguzi wa barabara katika Mkoa wa Kaskazini Pemba, ili atakapotokea mfadhili apewe, ingawa hilo litafanyika kwa kuangalia umuhimu wa hio barabara.

WANANCHI

Mkaazi wa shehia hiyo Bahati Ame Said, anamueleza kiongozi huyo kuwa ni mzuri kwa sababu anajiamini na anapenda kushirikiana na wanavijiji wa shehia yake bila ya ubaguzi.

Anasema, uongozi wake ni tofauti kidogo na masheha waliopita kutokana na yeye kuikusanya jamii nzima na kuiweka pamoja, kuondoa fitna, majungu na kushirikiana.

Mkaazi mwengine wa kijiji cha Sebuwatu, Amina Ali anasema, wamepata faraja kuona barabara hiyo imetengenezwa angalau kwa kifusi, kwani walikuwa wanapata shida.

Anawataka wanavijiji wenzake kuzidi kumpa mashirikiano sheha wao, ili aweze kutekeleza majukumu yake ipasavyo kwa maslahi yao.

Kijana mmoja aliyekataa kutaja jina lake anasema, sheha huyo anashirikiana na wananchi katika majukumu yake ya kila siku na ndio maana kwa kiasi fulani anatatua changamoto zilizopo.

‘’Unapomwendea na tatizo au kesi anakuhudumia vizuri mpaka kufikia hatua ya mwisho na kama tatizo ni kubwa analifikisha kwenye vyombo vya sheria,’’ anaongeza.

ASASI ZA KIRAIA

Mratibu wa TAMWA Pemba, Fat-hiya Mussa Said anasema, wanao mpango mkubwa wa kuwajengea uwezo wanawake na jamii, ili wawe na muelekeo chanya wa kushiriki kwenye vyombo vya maamuzi.

‘’Tumewaona wanawake wengi walioingia kwenye uchaguzi wa mwaka 2020, ingawa wengine hawakushinda, lakini wameonesha moyo wa kushiriki tena kugombea mwaka 2025,’’ anaongeza.

Anasema, kwa sasa TAMWA inawanawajengea uwezo zaidi ili wajielewe, wajiamini na wajue namna ya kutengeneza timu ya kampeni katika kufanikisha azma yao.

Hiyo ni pamoja na namna ya kuzungumza katika hadhara za watu, kuzielewa sheria na kanuni za chaguzi na kutengeneza mtandao kwa ajili ya kushikana mikono katika uongozi.

‘’Tunawajenga kujua haki zao za kisheria na kikatiba, masuala ya siasa na demokrasia,’’ anafafanua.

Kwa Pemba, TAMWA imeshawapatia mafunzo wanawake 70 na wamewaunganisha na wanawake mashujaa ambao tayari wameshagombea nafasi mbali mbali.

Akimzungumzia Ramia, Mratibu huyo alisema… ‘’Mimi nipo kwenye shehia hiyo ya Bopwe na nauona utendaji wa kazi zake ni mzuri na anafaa kuendelea kuitumikia jamii,’’ Mratibu.

Hafidh Abdi Said ambae ni Mkurugenzi wa Jumuiya ya Mazingira na Utetezi wa kijinsia Pemba (PEGAO) anasema, wanawake wachache wanaokaa katika nafasi za uongozi wanaonyesha juhudi kubwa katika kutekeleza majukumu yao.

‘’Tulipofanya utafiti kwenye vyama walituambia, wanapochaguliwa viongozi wanawake hata chama kinaimarika zaidi kwani wanachangia kwa kiasi kikubwa,’’ anasema.

Anaeleza, kwa sasa wanawahamasisha wanawake kujiingiza katika masuala ya kiuchumi kwa sababu uongozi na chaguzi ni gharama, hivyo wakipata fedha zitawasaidia katika shughuli zao.

Anavitaka vyama vya siasa kuwapa wanawake fursa ya kushiriki katika uongozi, ili maendeleo ya haraka yapatikane, kwani wao hawapendi rushwa.

Shehia ya Bopwe ina wananchi 4,303 wanawake 2,292 na wanaume 2,011.

MWISHO.