Monday, December 23

“WEKENI MIKAKATI MAHUSUSI KUKITANGAZA CHUO CHA UJENZI ZANZIBAR” MHE. YAHYA RASHID ABDALLAH

Uongozi wa Chuo cha Ujenzi Morogoro umeshauriwa kuweka mkakati maalum wa kukitangaza chuo hicho Zanzibar ili kutoa fursa kwa vijana wanaotaka kujiendeleza kujiunga na chuo hicho.

Mwenyekiti wa Kamati ya Mawasiliano, Ardhi na Nishati Mhe. Rashid Yahya Abdallah ametoa ushauri huo wakati akizungumza na watendaji katika ukumbi wa mikutano wa chuo hicho.

Mhe. Rashid ameeleza kupitia wajumbe wa kamati ya Mawasiliano, Ardhi na Nishati watakua mabalozi wazuri kwa kukitangaza chuo hicho kwa wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.

Wakitoa michango yao katika kikao hicho wajumbe wa kamati ya Mawasiliano, Ardhi na Nishati wameishauri Serikali kutoa msukumo maalum wa kukiwezesha chuo hicho kujiendesha.

Wameeleza kwamba, Nchi kama China imepiga hatua kubwa ya kuwawezesha wananchi wake kwa kuanzisha vyuo vingi vinavyotoa elimu ya teknolojia.

Pia, waheshimiwa wajumbe wa Kamati hiyo wamependekeza kuekwa kwa mpango maalum wa kuwashirikisha wanawake katika mafunzo yanayotolewa na chuo hicho.

Akisoma taarifa Mkuu wa chuo cha Ujenzi Ndugu Mahamoud Mohamed amesema lengo la kuanzishwa kwa chuo hicho ni kuendeleza, kuratibu na kuimarisha mafunzo ya matumizi stahiki ya nguvu kazi Nchini.

Aidha, amesema chuo hicho kinatarajiwa kuwa ni kituo kikuu cha uenezaji wa teknolojia ujenzi kwa Nchi nzima.

Akigusia changamoto zinazokikabili chuo hicho Ndugu Mahamoud ameeleza kwamba uhaba wa wafanyakazi wakiwemo walimu wa kufundisha masomo pamoja na uhaba wa vifaa vya kujifunzia wanafunzi.

Wajumbe wa Kamati ya Mawasiliano, Ardhi na Nishati wamepata fursa ya kutembelea maeneo tofauti ya chuo ikiwemo kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la utawala.

Chuo cha Ujenzi kimeanzishwa mwaka 1975 na kina eneo lenye ukubwa wa zaidi ya hekta kumi na nne.

Imetolewa na Kitengo cha Habari (WUMU)