Friday, December 27

RC Mattar ashiriki matembezi maalumu ya Wiki ya Shukurani kwa walipakodi Pemba, amewashuku wananchi kwa kuendelea kulipa

NA ABDI SULEIMANA, PEMBA.

MKUU wa Mkoa wa Kusini Pemba Mattar Zahor Massoud, amewashuku wananchi kwa kuendelea kulipa kodi zao kwa serikali, kwani kodi hizo ndizo zinazopelekea kutekelezwa miaradi mbali mbali ya maendeleo.

Alisema wananchi wameona na kufahamu kuwa mjenga nchi ni mwananchi mwenyewe, kwani nchi zote zinazoendelea zinazingatia mapato ya ndani ya nchi na sio misaada kutoka nje ya nchi.

Alisema ili tufikie huko mashirikiano ni kitu mihimu katika suala zima la ulipaji wa kodi, pamoja na mapato ambayo yamezunguruka katika maeneo mbali mbali.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu Mkoa huyo, Mkuu Wilaya ya Chake Chake Abdalla Rashid Ali, mara baada ya kumalizika kwa matembezi maalumu ya Wiki ya Shukurani kwa walipakodi Pemba, yalioambatana na kauli mbiu “Kodi Yetu, Maendeleo Yetu, Tuwajibike” yalyoandaliwa na TRA Pemba.

Alisema kodi zote zinazokusanywa na TRA Zanzibar zinatumika Zanzibar, kwa ajili ya kuleta maendeleo kwa taifa na kuondoa changamoto za kukosekana kwa huduma muhimu kwa jamii.

“Mashirikiano ni kitu mihimu katika ulipaji wa kodi, kodi hizi ndizo tunazotumia katika shughuli za maendeleo ikiwemo uimarishaji wa huduma za afya, elimu miundo mbinu na shughuli nyengine za kijamii,”alisema.

Aidha aliwataka wananchi kuendelea kushirikiana na mamlaka hiyo,  ambayo imewekwa maalum katika kuisaidia serikali na kuweza kupatikana mapato ambayo yatasaidia kuimarisha huduma nchini.

Alisema mlipaji kodi ni mtu muhimu katika nchi, aliwataka wananchi kuendelea kushirikiana ili kufikia malengo ya viongozi wa Taifa, ili kuwafanya wananchi kuwa na maisha bora.

Hata hivyo aliwataka wenye dhamana za ukusanyaji wa kodi, kutambua kuwa wananchi, wafanyabiashara ni wenzao na kutumia lugha nzuri wakati wakukusanya kodi na sio kutumia nguvu.

Mapema Kaimu meneja wa mamlaka ya mapato Tanzania TRA Mkoa wa kikodi Pemba, Suleiman Nuhu Suleiman alisema lengo la kuandaa wiki maalum kwa jili ya mlipa kodi, ni kurudisha shukrani kwa wananchi pamoja na kuirudisha kodi hiyo katika jamii .

Alisema kila ifikapo Novemba ya kila mwaka, ni kawaida kwa TRA kuandaa wiki maalum kwa jili ya mlipa kodi, ikiwemo kugawa zawadi kwa waliofanya vizuri katika ulipaji kodi, kujenga majengo na miundombinu ambayo yatasaidia huduma za kijamii, Pamoja na kugawa vifaa katika maeneo ya upatikanaji wa huduma muhimu za wananchi ikiwemo skuli.

Akitoa neno la shukurani kwa wananchi, wanavikundi vya mazoezi kutoka maeneo mbali mbali, viongozi wa serikali wafanya kazi pamoja na watendaji wa TRA,  meneja msaidizi  orodha mkoa wa kikodi Pemba Suleiman Abdalla Said, alisema mamlaka hiyo itaendelea kushirikiana na kuwa karibu na wananchi na kuifikia jamii katika kutatua changamoto mbali mbali zinazowakabili.

MWISHO