Waziri wa Ujenzi ,Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar Mhe. Khalid Salum Mohamed amewataka wananchi wa Wiliya Kusini Unguja kutoa ushirikiano kwa wakandarasi wa kampuni ya IRIS ili kukamilisha ujenzi wa barabara zilizopangwa kujengwa.
Waziri Dk. Khalid ametoa wito huo wakati akizungumza na viongozi pamoja na wananchi wa Makunduchi kupitia kikao kilichofanyika katika Afisi ya Mkuu wa Wilaya ya Kusini.
Mhe. Waziri amesema wizara ya ujenzi inaendelea na utekelezaji wa ahadi za Mhe. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi juu ya ukamilishaji wa barabara za ndani.
Amesema tayari Serikali imekamilisha ujenzi wa barabara za wilaya ya kati Unguja na sasa inahamia wilaya ya Kusini ili kukamilisha ujenzi huo.
Waziri Dk. Khalid ameeleza kuwa kwa upande wa wilaya ya kusini Serikali imepanga kuzijenga barabara za Jambiani Kibigija-Jambiani Mfumbwi (km5), Muungoni Skuli –Pwani Duta( km2-6), Bwejuu Viamboni – Kwa lila (km1.9) Kajengwa Koba – Kinandi ( km 6)
Nae, Mwakilishi wa jimbo la Makunduchi ambae pia ni Waziri wa Nchi Afisi ya Rais ,Katiba sheria Utumishi na Utawala bora Zanzibar.Mhe Haroun Ali Suleiman ameipongeza Wizara ya Ujenzi kwa kazi nzuri wanayoifanya na amewataka wananchi wa Jimbo hilo kuachana na maneno ya propaganda yanayotolewa na baadhi ya watu .
Akitoa salamu kwa niaba ya wazee wa Makunduchi Bw. Mwita Masemo ameahidi kuwapatia ushirikiano wakandarasi katika kazi zao za ujenzi wa barabara.
Imetolewa na Kitengo cha Habari (WUMU).
Novemba 27, 2023.